Papic: Yanga isitafute mchawi
Imeandikwa na Mwandishi Wetu; Tarehe: 1st February 2011 @ 09:14 Imesomwa na watu: 59
ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa Yanga, Kostadin Papic amesema ni vyema timu hiyo ikajipanga kiufundi na si kuanza kushutumu wachezaji ama watu wengine kuwa waliihujumu kwenye mchezo wao wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Dedebit ya Ethiopia Jumamosi.
Yanga Jumamosi ilifungana mabao 4-4 na Dedebit katika mchezo wa kwanza hatua ya awali ya michuano ya Kombe la Shirikisho uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, huku Yanga ikisubiri hadi dakika za majeruhi ndipo ikasawazisha bao la nne.
Papic hakuwepo benchi kwenye mchezo huo baada ya kutangaza kujiuzulu wadhifa huo Jumanne iliyopita, ikiwa ni siku chache kabla ya Yanga kuivaa Dedebit, akipinga Fredy Minziro kuteuliwa kuwa Kocha Msaidizi wa timu hiyo.
Lakini baada ya mchezo huo, baadhi ya wadau wa Yanga wamekuwa wakiyahusisha matokeo hayo na hujuma na wanawatuhumu baadhi ya wachezaji walicheza chini ya kiwango kwa nia ya kuivuruga timu.
Pia baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti kwamba kumekuwa na kutuhumiana ndani ya Yanga kuhusiana na mchezo huo, kwamba baadhi ya wachezaji waliamua kucheza chini ya kiwango kwa sababu ya mgogoro uliopo ndani ya Yanga.
"Hakuna mchezaji anayeweza kucheza chini ya kiwango ili timu ipate matokeo mabovu, Issac (Boakye), ni mchezaji mzuri tena wa kimataifa, anajua anachokifanya, Berko (Yaw) anajua nini anakifanya, hivyo kuwashutumu ni kutowatendea haki.
"Ni ujinga watu kuanza kujadili mambo ya kuhujumiana, zinatakiwa ziangaliwe sababu za kiufundi si hayo mambo ya kuharibiana majina, ama unanishutumu mimi ni ujinga, mimi ni kocha mzoefu ninayetambua vyema kazi yangu, hivyo Yanga waachane na mambo haya," alisema Papic.
Pia Papic aliyejiunga Yanga mwishoni mwa mwaka 2009, alisema hawezi kubaki timu hiyo na kuwa ataondoka Dar es Salaam wakati wowote kuanzia leo licha ya kuwa anaidai kiasi kikubwa cha fedha.
Hakupenda kutaja kiasi hicho anachodai kwa maelezo kuwa kwa sasa fedha si jambo la msingi kwake zaidi ya yeye kuondoka na kuwa anaelekea Afrika Kusini ambako kuna timu anafanya nayo mazungumzo.
Alieleza kuwa kama timu hiyo ambayo pia hakutaka kuitaja wataelewana naye ataanza kazi ya kuinoa msimu wa mwaka 2011/2012.
"Ningeweza kubaki Yanga, lakini wamenidharau, walikuwa na nafasi ya kunibakisha lakini kwa sasa haiwezekani, naondoka," alisema Papic.
Baada ya Yanga kupata sare hiyo ambayo kama inahitaji isonge mbele italazimika ishinde mchezo wa marudiano ama sare ya kuanzia mabao 5-5, baadhi ya wadau wa Yanga wamekuwa wakiwashutumu baadhi ya wachezaji kwamba walicheza chini ya kiwango makusudi.
Baadhi ya wanaotajwa ni Issac Boakye na kipa Berko ambaye alitoka mapema kipindi cha kwanza baada ya kuumia, wakati Boakye alitolewa kabla ya mapumziko ikiwa ni baada ya kusababisha bao la kwanza la Dedebit dakika ya 24 kutokana na kutoa pasi fupi iliyonaswa na Damit Tikadu aliyepachika mpira wavuni.
Minziro kwa upande wake akizungumza baada ya mchezo wa Jumamosi, pamoja na mambo mengi ya kiufundi, pia alisema kuna haja Yanga kuwa na umoja kwani mgogoro uliopo baina ya viongozi una madhara makubwa kwa timu kwa vile humjui nani adui na nani mwenzako.