Simba, Yanga funga hao
Imeandikwa na Mwandishi Wetu; Tarehe: 28th January 2011 @ 23:59
WAWAKILISHI wa Tanzania Bara kwenye michuano ya kimataifa, Simba na Yanga leo watakuwa kwenye viwanja tofauti kupeperusha bendera ya Taifa.
Kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga itaikaribisha Dedebit ya Ethiopia katika mechi ya Kombe la Shirikisho, wakati Simba itakuwa mjini Moroni, Comoro kucheza na Elan Club de Mitsoudje ya huko.
Kwa upande wa wawakilishi wa Zanzibar, leo kutakuwa na mchezo mmoja, ambapo KMKM itakuwa mwenyeji wa DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) katika mchezo wa Kombe la Shirikisho.
Akizungumzia mechi ya Yanga, Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Fredy Minziro alisema amekiandaa vizuri kikosi chake na ana imani kitaibuka na ushindi.
"Tumejiandaa vizuri na mechi hiyo na tutahakikisha tunashinda ili kujiweka katika mazingira mzuri ya kusonga mbele,"alisema Minziro.
Aidha kocha huyo ambaye amechukua mikoba kutoka kwa Kostadin Papic aliyetangaza kujiuzulu mwanzoni mwa wiki hii, aliwaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu yake.
Naye kocha wa Dedebit Gembremed Haile, alisema haihofii Yanga licha ya kufahamu kuwa ni timu kubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
"Yanga naifahamu, lakini hata sisi tumejiandaa na tutashinda," alisema kocha huyo.
Washambuliaji wa Yanga wakiongozwa na Davis Mwape, Idd Mbaga na Jerry Tegete watakuwa na jukumu kubwa la kupata mabao mengi ili yasaidie mbele ya safari.
Si kufunga mabao mengi, lakini pia kuhakikisha mabeki wakiongozwa na Shadrack Nsajigwa, Stephano Mwasika na Nadir Haroub wahakikishe kipa Yaw Berko hapati madhara.
Kwa upande wa Simba ambayo ipo mjini Moroni katika visiwa vya Comoro, leo itakuwa na kazi nzito dhidi ya timu ya Elan de Mitsoudje ya huko.
Simba iliwasili katika visiwa hivyo tangu Jumanne wiki hii na habari kutoka huko zinasema kuwa wachezaji wote wako katika hali nzuri.
Akizungumza kutoka Moroni, Kocha Mkuu wa Simba Patrick Phiri aliwatoa hofu mashabiki na Watanzania kwa ujumla kwa kuahidi kuwa wanao uwezo wa kufanya vizuri na kuibuka na ushindi katika mechi hiyo.
Phiri alisema pamoja na kwamba anatambua kuwa wapinzani wao ni timu bora, lakini wao wamejiandaa kuibuka na ushindi.
"Tunajua wao wako nyumbani, lakini nimejipanga na kikosi changu na natarajia nitapata ushindi mkubwa,"alisema kocha huyo Mzambia.
Simba itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kufungwa mabao 3-2 katika mchezo wa Jumapili iliyopita Ligi Kuu Tanzania Bara, hivyo kubaki nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo.
Yanga sasa ndiyo inaongoza ligi ikiwa na pointi 31, wakati Simba inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 27.
Yanga imeizidi Simba mchezo mmoja. Washambuliaji wa Simba wakiongozwa na Emmanuel Okwi, aliyerejea uwanjani baada ya kuwa majeruhi akishirikiana na Mussa Mgosi, Patrick Ochan watakuwa na jukumu kubwa la kuhakikisha Simba inapata ushindi wa kishindo.
Ushindi wa mabao mengi utaiweka Simba kwenye nafasi nzuri zaidi kwenye mchezo wa
marudiano wiki mbili zijazo jijini Dar es Salaam, ambapo kama itawaondoa Wacomoro itakutana na mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, TP Mazembe.
Ni vyema safu ya ulinzi ya Simba chini ya Juma Nyoso, Haruna Shamte, Meshack Abel na Juma Jbau nayo ikazidisha umakini kuhakikisha kipa Juma Kaseja hapati madhara.
Nayo KMKM leo ni nafasi nzuri kwake kuhakikisha inapata ushindi mnono ambao utakuwa hazina kubwa zitakaporudiana wiki mbili zijazo nchini DRC.