Papic aihenyesha Yanga
Imeandikwa na Mwandishi Wetu; Tarehe: 28th January 2011 @ 08:04
KOCHA Kostadin Papic ametangaza kujiuzulu kuinoa Yanga, lakini klabu hiyo bado inang'ang'ania kuwa haitambui uamuzi huo kwa vile bado haijapata barua.
Jumanne wiki hii, Papic raia wa Serbia aliuambia uongozi wa Yanga kwamba hataifundisha timu hiyo na ameamua kujiondoa kwa vile uongozi umeshindwa kutekeleza yale aliyokuwa akiyakataa.
Ofisa Habari wa Yanga, Luios Sendeu alikaririwa na vyombo vya habari baada ya kuwepo taarifa za kujiuzulu kwa Papic, akisema ni kweli aliuambia uongozi wa Yanga kwamba ameamua kujiondoa, ila walikuwa wanasubiria barua.
Papic alienda mbali zaidi baada ya juzi kwenda kwenye mazoezi ya timu hiyo na kuwaaga wachezaji wa timu hiyo ambao kesho wana kibarua cha kucheza mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Dedebit ya Ethiopia kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Papic amekuwa katika msuguano wa chini kwa chini na uongozi wa Yanga karibu wiki moja sasa akipinga kupelekewa Fred Minziro awe msaidizi wake, kwani hataki kocha ambaye ametoka kwenye timu ya Ligi Kuu afanye naye kazi.
Kocha huyo Jumanne aliwambia viongozi wa Yanga wakati wa mkutano naye kwamba asingekuwa tayari kufanya kazi na Minziro kama viongozi wataendelea na msimamo wao wa kutaka awe msaidizi wake, jambo ambalo viongozi walisisitiza hawatabadili msimamo wao na kuwa Minziro atakuwa ndiye msaidizi wake.
Minziro alikuwa Kocha Mkuu wa Ruvu Shooting na alianza kazi Jumatatu wakati Yanga ilipocheza na Polisi Tanzania Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam, ambapo wote na Papic walikuwepo benchi wakati timu hiyo ikiifunga Polisi mabao 2-0.
Lakini akizungumza jana na waandishi wa habari, Sendeu alisisitiza kuwa bado wanamtambua Papic ni kocha wao kwani hakufuata taratibu za kuandika barua zaidi ya kuwajulisha kwa mdomo kwamba amejiuzulu.
"Imesikika tu katika vyombo vya habari na yeye amekuwa akisema tu kuwa anajiuzulu, lakini barua sisi hatuna bado, "alisema Sendeu. Papic hakupatikana jana kuzungumzia kuhusiana na suala hilo.
Jumla Maoni (1) Maoni YANGA huwa tuna salaam isemayo DAIMA MBELE,NYUMA MWIKO......ila kwa hali inavyoendelea pale club sijui hatima yake ni nini,na kesho tuna mechi ya kimataifa,ni nani atakuja kulaumiwa na hii hali tete,kwa kipindi kidogo club ilikuwa imetulia lakini sasa ni hali tete,nawasahi viongozi,wanachama,wapenzi,washabiki kukaa chini na kutafakari la sivyo tunaipeleka pabaya club.Mama Karume ingilia kati huu mgogoro.....