TFF, klabu kujadili maazimio ya Bagamoyo
Thursday, 27 January 2011 21:02
Clara Alphonce
SHIRIKISHO la Soka Tanzania, TFF, limesema kuwa limepanga kukutana na klabu zote 12 zinazoshiriki Ligi Kuu ya Bara kwa ajili ya kupitia maazimio ya Bagamoyo.
TFF, na klabu pamoja na Shirikisho la Soka la Kimataifa, FIFA, walikutana na klabu hizo mwaka juzi na kukubaliana mambo kadhaa ambayo yalitakiwa kutekelezwa na klabu kwa ajili ya maendeleo ya soka.
Moja ya maazimio ambayo walikubaliani ni kila klabu kuwa na makatibu, maafisa habari pamoja na wahazini wa kuajiriwa kwa ajili ya kufanya klabu hizo kwenda na wakati kwa kila mtu kufanya kazi yake.
Pia walikubaliana klabu zote kufanya ukaguzi wa akaunti zao kwa ajili ya kuwawezesha wadhamini kuwekeza katika klabu hizo pamoja na kila klabu kuwa na uwanja wake wa kufanyia mazoezi ambao unajulikana kuliko kuhamahama.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema jana kuwa wamepanga kukutana na klabu hizo wiki ijayo kuzungumzia hayo na kutathimi maazimio hayo ya Bagamoyo na kuona wamefikia wapi.
Alisema kwa kuwa walishapanga kuwa mwaka huu ndio utakuwa mwisho wa malengo hayo basi pia watapanga mikakati ya kuakikisha wanafanikiwa kwa kila klabu kutimiza malengo hayo.