MWANAMUZIKI mkongwe wa nyimbo za Injili nchini Faustine Munishi, Jane Miso na Victor Aaron ni miongoni mwa wanamuziki watakaopamba tamasha la aina yake la kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia yatima na wanaoishi katika mazingira magumu.
Tamasha hilo la muziki ambalo limepangwa kufanyika Desemba 26 kwenye viwanja vya Posta Kijitonyama, Dar es Salaam limeandaliwa na taasisi ya kulea watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu ya Keep a child alive ya Dar es Salaam.
Akizungumza na HABARILEO Dar es Salaam jana, Mratibu wa tamasha hilo Petro Magige alisema maandalizi kwa ajili ya tamasha hilo ambalo litafanyika Desemba 26 mwaka huu yanakwenda vizuri.
Magige alisema taasisi yake inakusudia kusaidia watoto wapatao 150 ambao wataanza shule ya msingi januari mwakani.
Mratibu huyo aliwataja wasanii wengine nyota ambao watapamba tamasha hilo kuwa ni Leonida Komba, Martha Mwaipaja na kwaya maarufu Tabata Mennonite ‘Wana kunyatanyata' na New Life in Christ, Tabata ‘Sipati Picha' na vingundi vingine vingi.
"Kutakuwa na waimbaji wengi siku hiyo na wote wapo kwenye maandalizi kuhakikisha tamasha linakuwa la baraka kwa kila atakayehudhuria.
"Tumechagua Desemba 26 kwa sababu ni siku nzuri yenye maana ya kutoa zawadi hivyo, itakuwa siku nzuri kujitolea kwa ajili ya watoto wenye mahitaji hivyo, tunawaalika watu wengi kuja kwa wingi kushiriki tamasha ambalo kiingilio ni Sh 5,000 kwa viti vya kawaida na 10,000 kwa VIP," alisema.
Munishi ni mwanamuziki mkongwe ambaye wimbo wake wa ‘Malebo' umeendelea kutamba kwa miaka kadhaa sasa.