Magaidi waitia doa Russia Kombe la Dunia
Wednesday, 26 January 2011 20:38
MOSCOW, Russia
MAGAIDI wameonyesha wazi nia yao kutaka kuharibu maandalizi ya Fainali za Kombe la Dunia baada ya kuushambulia kwa mabomu Uwanja wa Ndege wa Moscow, Domodedovo, na kusababisha watu 35 kufariki na wengine 100 kujeruhiwa.
Moscow ni mji mkuu wa Russia, ambao Desemba 2 mwaka jana, FIFA iliupasisha kuwa taifa la kwanza la Ulaya Mashariki kuwa mwenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia 2018 nchini hiyo iliyokuwa inajulikana kama Umoja wa Ki-Soviet.
Tukio hilo la kushambulia Uwanja wa Domodedovo limekuja ikiwa ni saa 24 baada ya mkutano wa mwanzo wa kuweka mikakati ya fainali za 2018 na FIFA, ikiwemo kuunda Kamati ya Maandalizi (LOC) kwa kushirikiana na Umoja wa Soka wa Russia (FUR).
Wakuu hao wa soka walikutana na kuingia mkataba wa kuanza maandalizi, lakini kikubwa ilikuwa kuihalalisha rasmi nchi hiyo kuwa mwenyeji wa fainali hizo.
Katika hafla hiyo ya kutia saini iliyofanyika Jumapili kwenye mji wa Saint-Petersburg, Russia, alikuwepo Rais wa FIFA, Sepp Blatter aliyetia saini kwa niaba ya FIFA, wakati Waziri wa Michezo wa Russia, Vitaly Mutko na Alexei Sorokin, walitia saini na kutangazwa kuwa ndiyo watakaoongoza kamati ya Maandalizi, Russia 2018.
Wengine waliotia saini ni Sergei Fursenko na Nikita Simonyan, ambao ni Rais na Makamu wa Rais wa FUR.
Tukio la kushambuliwa Uwanja wa Domodedovo linafanana na shambulizi la lililofanywa katikati ya mji wa Moscow lililosababisha watu 52 kufariki na kuacha majeruhi kadhaa wakati nchi hiyo ikifikiriwa kupewa nafasi ya kuandaa Michezo ya Olimpiki katika miaka ya karibuni.
Kuona hivyo, Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa, IOC, iliitolea nje Russia na nafasi hiyo kupewa jiji la London litakaloandaa michezo hiyo mwakani.
Imeelezwa kuwa, mashambulizi ya mabomu yamefanywa na magaidi kwa lengo la kuharibu sura ya nchi hiyo kupata heshima ya kuandaa Fainali za Kombe la Dunia.
Na mbaya zaidi ni kwamba bomu lilitupwa kwenye maeneo ya wafanyabiashara na zaidi walikuwa raia wa Uingereza na inasadikiwa kuwa kazi hiyo imefanywa na kikundi cha al-Qaeda wanaoshirikiana na wanajeshi waasi wa nchi hiyo huku wakitamba kuwa wanaweza kuilipua nchi hiyo kwa njia yoyote na zaidi ni kutumia treni za ardhini.
Walijigamba kusema kuwa, kwa kuanzia wameishambulia Domodedovo kwa kuwa ndiyo uwanja maarufu kwa wafanyabiashara mbalimbali ikiwemo raia wa Russia.
Maafisa wa usalama wa Russia waliiambia Sky News juzi baada ya tukio hilo kuwa, kiasi cha asilimia 60 ya wafanyabiashara hao waliokuwepo uwanjani hapo wakati wa mlipuko, walikuwa raia wa kigeni.
"Magaidi wametekeleza kazi yao na walikuwa wakilenga maeneo muhimu. Wakati wa mlipuko huo, kulikuwa na wafanyabiashara wengi waliokuwa uwanjani hapo," lieleza taarifa moja ya mtaalam wa mabomu.
Itakumbukwa, mwaka 1972 kundi la magaidi waliokuwa wanjiita Black September waliingia kwenye kijiji cha michezo na kuua wanariadha 11 wa Israeli na kocha.
Katika siku za karibuni, Magaidi wamekuwa wakiumiza vichwa mataifa yanayokuwa wenyeji wa michezo mikubwa.