Baridi yaitesa Simba Comoro
Imeandikwa na Mwandishi Wetu; Tarehe: 27th January 2011 @ 07:24
TIMU ya Simba iliwasili salama jana Visiwa vya Comoro huku kukiwa na hali ya hewa ya baridi, ambayo imeanza kuwasumbua baadhi ya wachezaji.
Akizungumza kutoka Comoro jana, Kocha Mkuu wa timu hiyo Patrick Phiri alisema licha ya kuwepo baridi, lakini ana matumaini makubwa ya vijana wake kufanya vizuri.
"Dar es Salaam hali ya hewa ni joto kali, lakini huku sasa ni baridi kiasi kwamba inatubidi tuizoee, lakini kwa vile tumewahi kufika tuna matumaini makubwa mambo yatakuwa mazuri.
"Si baridi kali sana, lakini inatutesa, huwezi ukalinganisha na hali ya Dar es Salaam, " alisema Phiri na kuongeza kuwa kikosi chake kipo imara kwa mchezo dhidi ya Elan Club de Mitsoudje Jumapili katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Nahodha wa timu hiyo, Nico Nyagawa alisema, licha ya kuwepo baridi, lakini pia jana mvua kubwa ilinyesha na kuwa leo wataanza rasmi mazoezi kujiandaa na mchezo huo.
Jana Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu' alikaririwa na gazeti hili akisema wanaelekeza nguvu zao kwenye mechi hiyo na kuwa wamesahau masuala yanayohusiana na mchezo wao na Azam Jumapili, ambapo Simba ilifungwa mabao 3-2.
Kabla ya kufungwa na Azam, pia Simba ilifungwa na mabingwa wa Zambia, Zesco katika mchezo wa kirafiki na kufungana bao 1-1 na Clube Atletico Paranaense ya Brazil katika mchezo mwingine wa kirafiki.
Wachezaji waliopo Comoro ni Juma Kaseja na Ali Mustapha, wakati mabeki ni Haruna Shamte, Juma Jabu, Juma Nyoso, Kelvin Yondan na Meshack Abel.
Viungo ni, Abdulhalim Humuod, Rashid Gumbo, Nico Nyagawa, Mohamed Banka, Jerry Santo, Hilary Echesa, Amri Kiemba, Patrick Ochan. Washambuliaji ni: Mbwana Samatta, Emmanuel Okwi, Ali Ahmed Shiboli, Shija Mkina na Mussa Hassan.
Kama Simba ikifanikiwa kuwatoa Wacomoro itakumbana na timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ‘DRC', ambayo ni bingwa mtetezi wa michuano hiyo.
Wakati huohuo, Kocha Mkuu wa Yanga, Kostadin Papic aliyetangaza kujiuzulu kuinoa timu hiyo juzi, jana asubuhi aliwaaga wachezaji wa timu hiyo.
Habari zilizopatikana kutoka kwa wachezaji wa Yanga na kuthibitishwa na Ofisa Habari wa klabu hiyo, Luios Sendeu ni kuwa Papic alifika kambini na kuwatakia kila la heri wachezaji hao katika mechi yao ya Kombe la Shirikisho Jumamosi.
"Ni kweli Papic amefika kambini na kuwaaga wachezaji, lakini mpaka sasa sijapata taarifa kama ameshawasilisha barua yake ya kuachia ngazi kwa Mwenyekiti au la.
"Kama itakuwa hivyo, sisi tutaendelea na mambo yetu na timu itakuwa chini ya Fred Minziro kwa mechi ya Jumamosi," alisema Sendeu.