Kifo cha Dr. Remmy chawagusa wengi
RAIS Jakaya Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa familia, ndugu na jamaa wa mwanamuziki mkongwe Remmy Ongala aliyefariki usiku wa kuamkia jana jijini, Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu ilieleza kuwa Rais Kikwete amehuzunishwa na kifo hicho.
"Tumepoteza mwanamuziki mkongwe na mbunifu, Remmy aliipenda na kuiheshimu kazi yake wakati wote, ni huzuni sana kwa wapenda muziki na hasa miziki ya kale," ilisema taaria hiyo.
Rais Kikwete ni mpenzi wa miziki yote ya kale na ya kisasa na hata alipokuwa amelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili alifika kumjulia hali yeye na mwanamuziki mwingine mkongwe Muhidin Gurumo, lakini akakuta Dk. Remmy ameenda kufuatilia matibabu yake katika hospitali nyingine ya jijini.
"Namwombea mapumziko mema na Mwenyezi Mungu amrehemu, tutamkumbuka sana, " alisema Rais Naye Grace Chilongola anaripoti kutoka Mwanza kuwa wanamuziki mbalimbali nchini wameelezea kusikitishwa na kifo cha Dk. Remmy Ongala ambaye jina lake halisi ni Ramadhan Mtoro Ongala.
Dk. Remmy alifariki usiku wa kuamkia jana jijini Dar es Salaam na mwili wake umehifadhiwa hospitali ya Taifa, Muhimbili Dar es Salaam.
Akizungumza jana muasisi wa Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (Chamudata ), Kasim Mapili ameeleza kushtushwa na kifo hicho, na kwamba kabla ya mauti alikuwa akimtembelea marehemu alipokuwa amelazwa Muhimbili.
Kwa mujibu wa Mapili ni kuwa Remmy alipata uraia wa Tanzania mwaka 2000 na kwamba kulingana na taarifa alizopata kutoka kwa family ya marehemu ni kuwa maziko yatafanyika baada ya ndugu na watoto wa marehemu ambao wapo nje ya nchi kuwasili Dar es Salaa.
Naye msanii Mrisho Mpoto alisema Dk. Remmy aliutangaza muziki wa Tanzania ndani na nje ya nchi hivyo pengo lake haliwezi kuzibika kamwe.
Msanii wa maigizo, Jacob Stephen ‘JB' naye alieleza kushtushwa na kifo hicho na kwamba licha ya kuacha kupiga muziki wa kidunia na kugeukia ule wa kiroho, lakini nyimbo zake ziliendelea kutamba maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.
Hata hivyo alieleza kuwa jambo la msingi ni kuwa Dk. Remmy amefariki wakati amegeukia muziki wa kiroho kwa kupiga nyimbo za injili na kuwa funzo analolipata kwa msanii huyo kuwa mbunifu katika kazi na uvumilivu.
Wakati huo hu, bendi ya Orchestra Mlimani Park imeeleza kusikitishwa kwake kufuatia taarifa za kifo cha Dk Remmy.
Mkurugenzi wa habari wa bendi hiyo Jimmy Chika akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya bendi yake, alisema Sikinde inaamini Dk Remmy alikuwa mwanamuziki aliyeliletea sifa taifa la Tanzania katika muziki, hivyo kifo chake kimewagusa wanamuziki wote, uongozi
pamoja na wadau wa muziki kwa jumla.
Chika aliongeza kuwa bendi yake ilikuwa ikifanya kazi ya muziki kwa karibu sana na Dk Remmy kama vile kubadilishana wanamuziki na mambo mengine ya kiufundi hivyo inakichukulia kifo hicho kama ni pigo kwa muziki wa Tanzania.
Alisema enzi ya uhai wake wanamuziki wa bendi ya DDC Mlimani Park ‘Sikinde' ambayo ndiyo imezaa Orchestra Mlimani Park kama vile aliyekuwa mpiga solo marehemu Muhidin Kisukari, na mpiga rythm wa sasa Mjusi Shemboza wamewahi kufanya kazi na Dk Remmy na pia bendi ya Sikinde kwa nyakati tofauti hali inayoonesha ujirani mwem na ushirikiano.
"Sisi Sikinde tunatoa pole kwa familia ya marehemu Dk Remmy kufuatia kifo hicho na tunashiriki kuomba dua zetu kwa Mungu ili awape subira ndugu wote hasa katika kipindi hiki kigumu cha kifo cha mpendwa wao," alisema.
Aliongeza kuwa bendi yake katika kuenzi mchango wa Dk Remmy itakakikisha inaendeleza mazuri yote aliyoitendea fani ya muziki na watakuwa mstari wa mbele kutunga nyimbo zenye maonyo na mafunzo kama alivyokuwa Dk Remmy.
Naye Mwandishi Evance Ng'ingo anaripoti kuwa taratibu za mazishi zinaendelea kufanyika nyumbani kwa marehemu Sinza, Dar es Salaam na kuwa siku rasmi itajulikana baada ya watoto wake waliopo nje ya nchi kuwasili nchini.
Akizungumza na Habari Leo, mtoto wa marehemu Thomas Ongala, alisema mpaka jana bado walikuwa hawajaamua siku ya maziko na kuwataja watoto wanaosubiriwa kuwa ni Jesca aliyepo Dubai, Aziza na Zuhura wanaoishi Uingereza wote wakitarajiwa kuwasili leo.
Akizungumzia msiba ulivyotokea, Thomas alisema Remmy alizidiwa juzi akiwa Mbezi ambako pia ni nyumbani kwake na kukimbizwa hospitalini, ambako alifariki akiwa anatibiwa.
Alisema marehemu ambaye alikuwa na matatizo ya figo, alikuwa na ratiba ya kwenda hospitali ya Regency Dar es Salaam kila Jumatatu, lakini mauti yakamchukua usiku wa kuamkia siku hiyo.
Kwa mujibu wa makala mbalimbali zilizopata kuandikwa kuhusu Remmy na taarifa za mitandao mbalimbali zinaeleza kuwa Dk. Remmy alizaliwa mwaka 1947 katika mkoa wa Kivu na alifika Dar es Salaam mwishoni mwa miaka ya 1970 akitokea Zaire ambayo sasa inajulikana kama Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), ambako ndio kwao.
Alijiunga na bendi ya Orchestra Makassy iliyokuwa ikiongozwa na mjomba wake Mzee Makassy na kutunga vibao mbalimbali ikiwemo Siku ya Kufa.
Mwanzoni mwa miaka ya 1980 alikuwa na bendi yake ya Super Matimila ambayo ndiyo kwa kiasi kikubwa ilimpa umaarufu kutokana na nyimbo mbalimbali zilizogusa jamii, huku mwenyewe akijita mtetezi wa wanyonge.
Baadhi ya nyimbo zilizompa umaarufu ni Kifo, Kilio cha Samaki, Muziki Asili yake wapi, Amisa, Mrema na Mambo kwa Soksi, ambao hata ivyo ulipigwa marufuku.
Marehemu ameacha mke na watoto kadhaa, akiwemo Kally Ongala anayechezea Azam ya Dar es Salaam.