Federer, Li watinga fainali
Tuesday, 25 January 2011 20:51
MELBOURNE, Australia
BINGWA mtetezi, Roger Federer ameingia hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Australian Open baada ya kumchapa Stanislas Wawrinka 6-1,6-3,6-3.
Federer ambaye anataka kutwaa taji la tano la Australian Open, jana alitengeneza rekodi ya kucheza mechi 27 za robo fainali katika mashindano ya kuwania mataji makubwa ya Grand Slams, ambapo nusu fainali aliyoingia hivi sasa ni ya nane katika mashindano ya Australian Open.
Kwa upande wa Wawrinka ambaye ni raia wa Uswisi kama alivyo Federer, amewahi kumfunga Federer mara moja katika mechi saba walizowahi kucheza.
Federer na Wawrinka walicheza pamoja na kutwaa medali ya dhahabu katika timu ya Uswisi iliyotwaa medali ya dhahabu katika mashindano ya Beijing, pia huwa timu moja katika amshindano ya kombe la Davis.
"Kwa uwazi kabisa, nimecheza na Stan tofauti kabisa ukilinganisha na wachezaji wengine ambao wangepata nafasi ya kucheza naye wangecheza, kwa sababu haikuwa mechi rahisi kwa Stan, kwa sababu nimecheza hatua nyingi za robo fainali kwa hiyo nafahamu mbinu nyingi,"alisema Federer.
Kwa ushindi aliopata Federer atacheza mechi ijayo na mshindi wa mechi kati ya Novak Djokovic na Tomas Berdych.
Federer alishindwa kutamba katika Grand Slam mbili zilizopita baada ya kufungwa na Berdych katika mashindano ya Wimbledon, pia alifungwa na Djokovic katika mashindano ya U.S. Open. Djokovic pia alimchapa Federer kwenye hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Australian Open na kuingia fainali ambapo alishinda mechi na kubwa bingwa wa Australian opend 2008.
Pia katika mashindano hayo ya Australian Open, Li Na alimchapa Andrea Petkovic 6-2, 6-4 na kuingia hatua ya nusu fainali.
Li ambaye mwaka 2010 alitolewa katika hatua ya nusu fainali na Serena Williams alisema,"Ni jambo zuri kwangu, ni mara ya pili naingia hatua ya nusu fainali ya mashindano makubwa ya Grand Slam, nina matumaini naweza kufanya vizuri mwaka huu na kila mtu ataniona tena mwaka huu,"alisema Li Na.
"Ninafikiri amecheza vizuri, ninafikiri atatwaa taji la Australian Open kwa upande wa wanawake kwa sababu anajua vizuri sana kucheza tenisi,"alisema Petkovic.
Li Na anatarajiwa kucheza mechi ya nusu fainali na mshindi wa mechi kati ya mchezaji namba moja kwa ubora duniani kwa upande wa wanawake Caroline Wozniacki na bingwa wa French Open,Francesca Schiavone.
Juzi mchezaji namba moja kwa ubora wa uchezaji wa tenis duniani kwa upande wa wanaume Rafael Nadal alifika hatua ya robo fainali baada ya kumchapa Marin Cilic 6-2.
Nadal anatarajiwa kupambana na David Ferrer ili kuweza kupata nafasi ya kucheza nusu fainali. Ferrer alimchapa Milos Raonic 4-6, 6-2, 6-3, 6-4.
Andy Murray ambaye naye alimchapa Jurgen Melzer 6-3, 6-1, 6-1 anatarajiwa kucheza na Alexandr Dolgopolov ambaye alimchapa Robin Soderling 1-6, 6-3, 6-1, 4-6, 6-2.
Kwa upande wa wanawake, Kim Clijsters alimchapa Ekaterina Makarova 7-6 (3), 6-2, wakati Vera Zvonareva 6-4, 6-1 Iveta Benesova.
Katika mechi ya robo fainali Zvonareva anatarajiwa kukutana na Petra Kvitova, ambaye alimchapa Flavia Pennetta 3-6, 6-3, 6-3.
Naye Agnieszka Radwanska alimchapa Peng Shuai 7-5, 3-6, 7-5 na atakutana na Kim Clijsters katika hatua ya robo fainali mechi inayotarajiwa kuwa ya kuvutia na kali.