Simba yapigwa 3 taifa
Imeandikwa na Mwandishi Wetu; Tarehe: 24th January 2011 @ 08:11
MASHABIKI wa klabu ya Simba ya Dar es Salaam, jana walilazimika kulala mapema zaidi baada ya timu yao ya soka kukubali kipigo cha mabao 3-2 kutoka kwa Azam.
Pengine kipa mahiri wa timu hiyo, Juma Kaseja ndiye aliyetoka na uchungu zaidi baada ya kufanya kosa lililozaa bao la tatu dakika ya 54 na kuifanya Simba iwe nyuma kwa mabao 3-1, hivyo kuwa na kazi kubwa ya kusawazisha.
Kaseja alifanya kosa hilo, baada ya kutaka kuuwahi mpira wa juu ambao beki Juma Nyoso alikuwa akiuwania na mshambuliaji John Bocco, lakini baada ya Kaseja kutokea na kuliacha lango wazi Bocco aliinua mpira juu na kutinga wavuni.
Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, Simba ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya nane mfungaji akiwa Mussa Mgosi, baada ya kutokea purukushani, lakini dakika ya 14 Azam inayonolewa na Stuwart Hall raia wa Uingereza, ilisawazisha mfungaji akiwa Bocco kwa kichwa kutokana na krosi ya Ibrahim Shikanda.
Dakika tisa baadaye mpira mrefu uliopigwa na Ramadhan Chombo ‘Redondo' ulimkuta Ngasa aliyeingia kwa kasi ndani ya eneo la hatari, ndipo Kaseja alipoamua kutoka langoni na kujikuta akipigwa chenga na kisha Ngasa kuutumbukiza mpira wavuni.
Simba ilipata bao la pili dakika ya 86 mfungaji akiwa Hillary Echesa baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa Azam.
Simba inayonolewa na raia wa Zambia, Patrick Phiri, itabidi ijilaumu kutokana na kukosa nafasi kadhaa za kufunga kutokana na wachezaji wake kushikwa na kigugumizi cha miguu walipokaribia lango la Azam.
Hali hiyo pia iliikumba Azam ambayo Ngasa, Boco, Redondo na Ibrahim Mwaipopo nao walipata nafasi za kuongeza idadi ya mabao, lakini umaliziaji ulikuwa butu.
Baada ya mchezo huo Phiri alisema makosa yaliyofanywa na safu yake ya ulinzi kwa kuwa na udhaifu wa mawasiliano na kipa kuliiweka pabaya timu yake.
Naye Hall aliwapongeza vijana wake na kusema Simba ni timu ngumu, ambayo ilionesha uwezo wa hali ya juu, lakini timu yake ilistahili kushinda.
Kutokana na matokeo hayo, Simba sasa imetulizwa nafasi ya pili ikiwa na pointi 27 nyuma ya Yanga yenye pointi 28, wakati Azam imefikisha pointi 23.
Timu zote zimecheza mechi 12 na leo Yanga itashuka kwenye uwanja huohuo kuvaana na Polisi Dodoma.