Mwape awapa raha Yanga
Imeandikwa na Evance Ng'ingo; Tarehe: 25th January 2011 @ 08:10
DAVIES Mwape jana alifunga mabao yaliyoipa Yanga ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Polisi Dodoma katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Mabao hayo ambayo moja alifunga kila kipindi yamemfanya aanze kuonesha umuhimu wake uliomfanya Kocha Mserbia Kostadin Papic kumsajili kwenye dirisha dogo mwezi uliopita aimarishe safu ya ushambuliaji ya Yanga.
Mabao hayo ya jana yanamfanya afikishe mabao matano katika mechi mbili alizocheza, ambapo ya kwanza ilikuwa Ijumaa iliyopita alipopachika mabao matatu katika ushindi wa mabao 6-1, ambao Yanga iliupata dhidi ya AFC Arusha.
Mwape raia wa Zambia sasa ameanza kuwapa tumbo joto washambuliaji wa Tanzania wanaofukuzia ufungaji bora katika ligi hiyo, ambapo anayeongoza ni Gaudence Mwaikimba wa Kagera Sugar mwenye mabao nane na Mrisho Ngasa wa Azam mwenye mabao saba.
Jerry Tegete wa Yanga anashika nafasi ya tatu akiwa na mabao sita, huku Mussa Mgosi wa Simba na Revocatus Maliwa wa Ruvu Shooting wenyewe wakiwa na mabao matano mkononi sawa na Mwape.
Kutokana na ushindi huo wa jana, Yanga sasa imefikisha pointi 31 na kuendelea kuongoza ligi hiyo ikiwa mbele kwa pointi nne dhidi ya mtani wake wa jadi Simba ambaye anashika nafasi ya pili baada ya juzi kufungwa mabao 3-2 na Azam katika mchezo mwingine wa ligi hiyo.
Katika mchezo wa jana Polisi ilijitahidi kucheza kwa nguvu na kuwabana washambuliaji wa Yanga wakiongozwa na Tegete, Idd Mbaga na Mwape, lakini safu yao ya ushambuliaji yenyewe ilishindwa kutumia nafasi ilizozipata.
Baada ya kosakosa za hapa na pale, yanga ilipata bao la kuongoza dakika ya 43 mfungaji akiwa Mwape kwa shuti lililompita kipa Salum Kondo.
Washambuliaji wa Yanga waliendelea kuliandama lango la Polisi Dodoma inayonolewa na Kocha John Simkoko, lakini umaliziaji ulikuwa dhaifu.
John Kanakamfumu, Elias Mashaka na Salmin Kissy wa Polisi walipata nafasi kadhaa za kufunga, lakini nao walishindwa kuzitumia. Mwape alifunga bao la pili dakika ya 80 kwa shuti la mbali, lililoibua shangwe kwa mashabiki wa Yanga waliokuwa wakiimba wakitaja jina lake.
Mchezo huo uliingia dosari katikati ya kipindi cha pili baada ya mchezaji wa Polisi Elias Maftah kuzimia uwanjani baada ya kuanguka katika harakati za kuokoa mpira, hivyo kulazimika kupatiwa huduma ya kwanza na kisha kukimbizwa hospitali.
Kocha Mkuu wa Yanga, Kostadin Papic ambaye jana alikaa benchi pamoja na Kocha Msaidizi Fred Minziro ambaye alikuwa hamtaki, alisema baada ya mchezo kuwa ulikuwa mzuri na kwamba vijana wake walicheza mchezo wa kuvutia.
Kwa upande wake Simkoko alisema vijana wake walicheza vizuri, lakini bahati haikuwa yao na watajipanga kwa michezo mingine.
Wakati huohuo, katika tukio la kushangaza jana mwamuzi wa akiba alikuwa akibadilisha wachezaji kwa kutumia karatasi badala ya vibao kama ilivyozoeleka.
Tukio hilo lilifanya kila wakati mchezaji alipokuwa akitaka kuingia uwanjani mashabiki kuzomea huku wakiimba: "TFF TFF", ambalo ni Shirikisho la Soka Tanzania.
Licha ya karatasi hizo kutoonekana namba zake kwa mashabiki, lakini pia hata wachezaji wenyewe walikuwa hawazioni na kushindwa kutambua kwa haraka nani anayetoka.