Mwakalebela:Timu hazijishughulishi kupata wadhamini
Sunday, 23 January 2011 20:48
Allan Goshashy
KATIBU Mkuu wa zamani wa Shirikisho la soka Tanzania TFF, Frederick Mwakalebela amesema klabu za soka zinazoshiriki Ligi Kuu zinashindwa kupata udhamini kwa sababu hazijishughulishi kuhakikisha zinapata wadhamini.
Amesema viongozi wa klabu zinazoshiriki ligi kuu hawawezi kuandika mapendekezo (proposal) ya kutafuta wadhamini kwa sababu hazina uwezo wa kuwashawishi wadhamini.
Mwakalebela alisema hayo baada ya kufanya mahojiano maalum na Mwananchi, huku akisisitiza hata klabu za Simba na Yanga zilipata udhamini wa TBL baada ya kusaidiwa na TFF.
"Mdhamini anataka taarifa za benki(bank statement), kanuni za fedha (financial regulations), akaunti zilizokaguliwa (audited account),Mipango ya biashara (Business plans), lakini mimi sijawahi kusikia klabu yoyote inajitokeza kifua mbele kudai mahesabu yao yamepitiwa na kampuni ya ukaguzi ambayo inaheshimika,"alisema Mwakalebela.
Alisema,"Pia klabu za soka za ligi kuu zimejaa migogoro hivyo wadhamini wanaogopa kuweka fedha zao kwa sababu wanaona hakuna viongozi bora na utawala bora."
Mwakalebela alisema baada ya TFF kugundua tatizo hilo waliamua kuzisaidia klabu za ligi kuu na kurahisisha kazi zao ambapo mwaka 2008 waliamua yafanyike marekebisho ya katiba zote za klabu za soka zilizo Ligi Kuu.
Alisema baada ya klabu kufanya marekebisho ya katiba, mwaka 2009, TFF iliamua wachezaji na makocha wote wa Ligi Kuu lazima wawe na mikataba jambo ambalo lilifanyika pia.
Katibu huyo wa zamani wa TFF alisema mwaka 2010 TFF iliamua klabu zote za Ligi Kuu ziwe na watendaji wa kuajiriwa kwa sababu walifahamu klabu ikiajiri katibu mwenye shahada atasaidia zaidi masuala ya utawala na pia klabu ikiwa na mweka hazina ambaye ana shahada atasaidia katika masuala ya fedha ya klabu.
Mwakalebela alisema TFF iliamua mwaka 2011 kila klabu kuhakikisha inakuwa na akaunti ambayo imekaguliwa (audited account) kwa sababu zinao waweka hazina wataalamu, pia kila klabu iwe na ofisi na sehemu maalum ya kufanyia mazoezi siyo kuhama hama.
"Klabu za soka nchini zinahitaji sana wadhamini kwa sababu hazina fedha za kuwaandaa wachezaji wake wawe wazuri na kuwaweka kambini kwa sababu kufanya hivyo ni gharama,"alisema Mwakalebela.
Alisema,"TFF ikisema ligi kuu imekwisha na kambi za klabu zote za soka zinazoshiriki ligi kuu zinavunjwa, suala hilo la kuvunja kambi mapema kwa klabu zinazoshiriki ligi kuu linachangia kudumaza soka ya Tanzania.
Mwakalebela alisema pia ukosefu wa fedha kwa klabu zinazoshiriki ligi pia unasababisha klabu za ligi kuu kushindwa kuanzisha timu za vijana.
"klabu nyingi zimekuwa zikiunda tu timu za kushiriki mashindano ya Uhai ambapo mashindano hayo ya vijana yakimalizika na timu za vijana zinakuwa hazipo tena mpaka mashindano yajayo wanatafutwa wachezaji wengine na ndio maana ni vigumu kusikia klabu imepandisha wachezaji wake wa timu ya vijana kucheza ligi kuu,"alisema Mwakalebela.
Mwakalebela pia amezishauri klabu za Ligi Kuu kuhakikisha zinakuwa na viwanja vya kufanyia mazoezi kama ilivyo klabu ya Mtibwa huku akisisitiza klabu hizo kuwa na umoja ili kuwa na sauti.
Pia alizishauri klabu ziache tabia ya kushirikiana na waamuzi kufanya rushwa katika soka kwa sababu kitendo hicho kinasababisha timu inayoshinda inakuwa haistahili.