Nchunga anguruma, akataa kung'oka
Imeandikwa na Evance Ng'ingo; Tarehe: 22nd January 2011 @ 08:08
MWENYEKITI wa Yanga, Lyod Nchunga, amesema kikao kilichoitishwa na matawi ya klabu hiyo na kutaka ang'olewe madarakani hakikuwa halali.
Nchunga alisema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu sakata la kutakiwa kuachia madaraka kama ilivyoamriwa na matawi ya klabu hiyo.
Nchunga alisema, kikao hicho kilichofanyika makao makuu ya klabu hiyo Mtaa wa Twiga na Jangwani juzi, kilikiuka katiba ya klabu kwa kuwa hakiwezi kuiagiza kamati ya utendaji kutenda jambo lolote kama ambavyo kilifanya.
Pia alisema kuwa suala ambalo lilikuwa likijadiliwa katika kikao hicho si la kimsingi kwa kuwa tayari lilijadiliwa na Kamati ya Utendaji.
Akifafanua zaidi hoja za kumng'oa madarakani zilizotiliwa mkazo na kikao hicho cha matawi, alisema kuwa kilipotosha.
Ilidaiwa kwenye kikao hicho cha matawi kuwa alimwandikia barua mdhamini wa klabu hiyo Francis Kifukwe akimuagiza kuandaa mchakato wa kuiuza klabu ya Yanga.
Lakini alifafanua zaidi akisema kuwa lengo lake lilikuwa ni kuanzisha kampuni ya kuuza nguo na vifaa vyenye lebo ya Yanga na kuongeza hata hivyo, kamati ya utendaji ilikuwa haijabariki suala hilo.
Rais huyo pia alifafanua kuhusu uteuzi wa Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu kuwa mdhamini wa klabu nalo lilikuwa halijabarikiwa na kamati ya utendaji pia.
Aliongeza kuwa kikao hicho kiliitishwa na wanachama wachache wasiopenda maendeleo ya klabu hiyo na ambao wanatumiwa na wanachama wachache waliokuwa wakijinufaisha na vyanzo vya mapato kutoka klabuni hapo.
Alisema, kwa sasa utaratibu wa ukaguzi wa fedha za klabu hiyo unaendelea na aliahidi kuwachukulia hatua kali wale watakaobainika kuwa walifuja fedha za klabu hiyo.
Pia alikanusha uvumi kuwa anatumiwa na mdhamini wa klabu hiyo Yusuph Manji kwa manufaa yake binafsi ambapo alisema awali aliwahi kuwa mwanasheria wa Manji, lakini kwa sasa hahusiki na mfanyabiashara.
Alisema, uhusiano wao ni katika klabu ya Yanga akiwa mdhamini. Pia alisema bado hajapewa barua na kamati ya utendaji ya kumtaka aachie madaraka na kuongeza kuwa akipata ataamua cha kufanya.
Juzi klabuni hapo kulikuwa na mkutano uliohudhuriwa na matawi 84 ya klabu hiyo, mkutano huo uliongozwa na mwenyekiti wa matawi hayo Mohamed Msumi na kuitaka kamati ya utendaji kumwachisha kazi mara moja Nchunga.