Viongozi wa matawi Yanga walidanganywa
Imeandikwa na Mwandishi Wetu; Tarehe: 22nd January 2011 @ 23:57
VIONGOZI wa matawi ya klabu ya Yanga wamejutia kitendo chao ya kukutana Alhamisi iliyopita na kudai kuwa walifanywa hivyo kwa kudanganywa.
Viongozi hao wa matawi walikutana juzi na kutoa maelezo kwa Kamati ya Utendaji ikutane haraka ili imsimamishe Mwenyekiti wa klabu hiy Lloyd Nchunga mpaka hapo mkutano mkuu utakapoamua vinginevyo.
Aidha, viongozi hao walidai kutomtaka mfadhili wao Yusuf Manji kwa madai kuwa mfadhili huyo amekuwa akiwaendesha na kwamba anataka kuinunua Yanga.
Lakini badala yake viongozi hao jana walikutana na kutoa tamko la pamoja kwamba walifanya hivyo bila kufanya uchunguzi lakini baada ya kufanya utafiti wao waligundua kuwa walidanganywa.
Katika taarifa ya viongozi hao wapatao 30, ilisema: "Sisi wanachama tuliohudhuria kikao cha tarehe 21 mwezi wa Januari 2011, katika kikao hicho tulidanganywa mambo mengi, na baadae tulifanya utafiti wetu na kugundua kuwa kikao kile kilifadhiliwa na adui yetu mfanyabiashara mmoja ambaye tulimfukuza Yanga".
"Eti kikao gani cha ndani ya Yanga kinafanyika na waandishi wa habari wakiwa ndani? Tena mwandishi wa adui yetu anakuwa msemaji katika kikao hicho eti ofisa mmoja ambaye alifukuzwa na mfadhili wetu baada ya sisi kumshauri amfukuze tulipogundua anashiriki kuiba mali ya Yanga na ni msaliti wa klabu yetu, ndio anatumika kuwavuruga wanayanga," ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilisema, mkutano huo wa viongozi hao wa matawi ulielezwa kuwa lengo la Manji lilikuwa kuanzisha kampuni kitu ambacho waligundua si kweli kwani suala la kampuni lipo kwenye Katiba ya Yanga na hakuna kitu chochote kipya kilichokuwa kinaanzishwa.
"Barua ya Nchunga kwa Kifukwe (Francis mdhamini wa Yanga) ilikuwa ikitekeleza matakwa ya Katiba na pia ni jambo lililozungumzwa katika mkutano wa Kamati ya Utendaji iliyokutana Novemba 30 mwaka jana na wajumbe wakahudhuria na kupokea posho, wajumbe hao nao wanasema mkutano huo haukuwa halali tunawashangaa,"ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Baadhi ya viongozi hao waliotoa tamko hilo ni Shaaban Uda Omar, Kondo Kipwata, Thomas Mdeka, Selemani Kato, Mikidadi Jagalaga, Masoud Saad na Ally Buto.
Naye Evance Ng'ingo anaripoti kuwa Wazee wa klabu ya Yanga wamewataka wanachama wa klabu hiyo wasiomtaka Manji kujiondoa uanachama.
Akizungumza kwa niaba ya wanachama 21 waliozungumza na waandishi wa habari jana katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo, Yusuph Mzimba alisema kuwa wanachama hao wanatumiwa.