Poulsen visingizio kibao
Imeandikwa na Evance Ng'ingo; Tarehe: 21st January 2011 @ 08:36
KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars Jan Poulsen amesema safu yake ya ulinzi haikuwa ya kuridhisha ndiyo maana walifungwa mabao mengi katika michuano ya Bonde la Mto Nile iliyomalizika Jumatatu wiki hii mjini Cairo, Misri.
Poulsen aliyasema hayo alipozungumza na waandishi wa habari jana juu ya safari ya Misri, ambapo Stars ilifungwa mabao 5-1 na Misri, ikatoka sare ya bao 1-1 na Burundi na Uganda kabla ya kufungwa mabao 2-1 na Sudan.
"Nashangazwa na magoli mengi tuliyofungwa yalikuwa ni ya kichwa hali inayoonesha kuwa beki haikuwa ya kuridhisha," alisema.
Alisema kuwa tofauti na mwaka jana ambapo walishinda mechi sita, kutoka sare mechi mbili na kupoteza mechi mbili pia, lakini mwaka huu wamefungwa michezo miwili, sare mbili na hawakushinda katika michezo minne waliyocheza.
Poulsen alisema, kingine kilichowafanya waboronge kwenye michuano hiyo ni maandalizi madogo waliyoyafanya.
Alisema kuwa tofauti na michuano mingine kama vile Chalenji iliyofanyika mwishoni mwa mwaka jana timu yake hiyo iliandaliwa vyema na iliweza kushinda lakini michuano ya Mto Nile maandalizi yalikuwa ni ya kushtukiza.
Alisema kuwa ili timu hiyo kuweza kujiandaa vyema na michuano mingine mikubwa inatakiwa kupata michezo mingi hasa kutoka timu za bara la Ulaya na America ili kujifunza aina nyingine ya mchezo.
Alisema, kwa muda mrefu maandalizi yao yamekuwa ni kujipima na nchi za Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi lakini ni vyema wakajipima zaidi kwa Brazil na nchi nyingine kubwa.
Alifafanua kuwa kwa sasa anajiandaa kuifundisha timu namna ya kuikabili Jamhuri ya Kati katika mechi itakayofanyika Machi mwaka huu ambapo anatafuta video za michezo ya timu hiyo.
Akizungumzia suala la mabadiliko ya wachezaji ayafanyayo kama yana athari kwa timu, alisema kuwa wachezaji wanafundishwa fomula ya mchezo hivyo haoni kama kuna tatizo katika kuwabadilishabadilisha.
Kuhusu mchezaji Gaudensi Mwaikimba, Poulsen alisema kuwa mchezaji huyo amepewa nafasi mara mbili na kushindwa kuonesha uwezo hivyo sio busara kuendelea kumuita.
Pia alifafanua kuwa kwa sasa inatakiwa nguvu zaidi kuwekezwa kwa wachezaji wa timu ya vijana kwa kuwa ndio watakaoweza kuibeba timu ya Taifa.
" Mfano ni kama kwa timu ya Rwanda ambao inafanya vyema sana nchini kwao ikilinganishwa na timu ya vijana ya nchi nyingi kwa sasa, tuwekeze huko zaidi ili tufanikiwe," alisema.