25 watinga fainali za Kisura wa Tanzania
Imeandikwa na Mwandishi Wetu; Tarehe: 19th January 2011 @ 23:35
WASICHANA 25 kutoka mikoa mbalimbali nchini, wamefanikiwa kutinga katika hatua ya fainali ya shindano la kumsaka Kisura wa Tanzania 2011, baada ya mchujo uliofanyika kwa miezi miwili.
Mchakato wa kuwapata wasichana hao, ulianza Desemba 11, mwaka jana na kumalizika mapema mwezi huu, ukihusisha mikoa ya Mwanza, Mara, Kagera, Shinyanga, Tabora, Dar es Salaam, Arusha, Manyara, Dodoma, Iringa, Mbeya na Ruvuma.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti na Mwanzilishi wa mradi wa Kisura wa Tanzania, Juliana Urio kutoka Kampuni ya Beautiful Tanzania Agency (BTA), alisema kuwa warembo hao 25 ni miongoni mwa zaidi ya 1000 waliojitokeza katika mchakato huo kwa mikoa yote.
Alisema kuwa waliopitishwa kutinga fainali, ni wale waliokidhi vigezo vinavyotakiwa, baada ya mchujo na usaili uliofanywa katika mikoa husika.
"Wapo ambao tuliwapitisha katika mchujo wa awali, lakini baadaye majina yao yalienguliwa kutokana na kuzidiwa vigezo na wengine tuliokutana nao katika mikoa mingine," alisema Urio.
Urio alivitaja vigezo vilivyokuwa vikizingatiwa katika shindano hilo kuwa ni urefu wa sentimita 174, mapaja 36, kiuno 25, kifua 36 na umri ni kati ya miaka 18-27, bila kujali kama mshiriki ameolewa, kuzaa au la.
"Kwa ujumla mwitikio wa wasichana katika shindano letu, ulikuwa ni mkubwa sana, hii imetuonesha kuwa shindano letu limekubalika, lakini pia imetuonesha kuwa kuna wasichana wengi sana wenye kiu ya kufanya mambo ya uanamitindo, ila wanakosa nafasi ya kuonesha vipaji vyao," alisema Urio.
Alisema kuwa mwaka huu wameongeza wasichana watano zaidi mbali na kiwango chao cha awali cha kuchukua wasichana 20 na hii ni kutokana na mdhamini wao Kiromo View Resort kutupa nafasi ya pekee ya kuongeza wasichana watano zaidi.
Aliendelea kusema iwapo ingewezekana, wangechukua hata wasichana zaidi ya hapo, lakini hali haiwaruhusu kufanya hivyo.
Urio aliwataja wasichana waliotinga fainali, tayari kwa kambi itakayoanza Januari 30, mwaka huu katika Hoteli ya Kiromo Resort, iliyopo nje kidogo ya Mji wa Bagamoyo ni Neema Methew na Silipa Swai toka Mwanza, Lilian Bussan na Gaudencia Joseph toka Mara, Beatrice James wa Kagera, Monica Fikiri na Anjel Mombeki wa Tabora; Suzana Manoko,Winfrida Sabega, Rita Swai, Lethina Christoper, Jocye Joseph, Happyness Salimenya, Grace David kutoka Dar es Salaam, Dotinata Soro, Neema Kilango, Neema Seley, wa Arusha, Kipoyane Laibon toka Manyara, Mariam Kissa Isaack, Asha Hamisi, Flavian Makungwa, Lucy Charles John, wa Dodoma na Queen Kabisama kutoka Ruvuma.
Mdhamini mkuu wa shindano hilo ambalo linafanyika kwa mara ya tatu sasa ni Family Health International (FHI), wakati wadhamini wengine ni TBC1, Kiromo View Resort, TanFoam (Arusha), SBC Limited, Flare Magazine, Hugo Domingo, BASATA, GRM Production, Clouds FM, ATCL na MJ Records.