Ligi Mbeya kuanza kesho
Imeandikwa na Mwandishi Wetu, Mbeya; Tarehe: 12th January 2011 @ 23:35
BAADA ya kusuasua kwa muda mrefu, Chama cha Soka mkoani hapa (MREFA) kimetangaza rasmi tarehe ya kuanza kutimua vumbi kwa Ligi ya Taifa ngazi ya Mkoa.
Chama hicho kimesema ligi hiyo itaanza rasmi Januari 14 na itashirikisha timu 18, zitakazocheza katika makundi matatu A, B na C ambayo kila mmoja itakuwa na timu 6.
Kila kundi litatoa washindi wawili watakaoshiriki hatua ya Sita Bora. Kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti wa MREFA, John Mwamwaja, Kundi A linajumuisha timu za Bondeni FC, Eagle FC, Tembo Saruji, Zaragoza FC, Ilongo Shooting Stars na Chuo Magereza.
Kundi B lina timu za Mbalizi Super Stars, Ibara SC, Airpot Rangers, Super Marine FC, Tukuyu Stars na Chipukizi, huku Kundi C litaundwa na Eleven Boys FC, Kijiwe FC, Vijana FC, National Ntaba FC, Wenda FC na Buffalo FC.
Mwamwaja amevitaja viwanja tisa vitakavyotumika kuendesha ligi hiyo kuwa ni Vwawa wilayani Mbozi, Uwanja wa Kyela, Tukuyu wilayani Rungwe, Sokoine, Magereza, na Uhasibu vilivyopo Mbeya mjini, Mbalizi Mbeya Vijijini na Rujewa na Ilongo vilivyopo wilayani Mbarali.
Makamu Mwenyekiti huyo alisema maandalizi yote kwa ajili ya ligi hiyo yamekamilika. Lakini alikiri kuchelewa kuanza kwa ligi hivyo kutishia kuchelewa kumalizika tofauti na kalenda ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
"Maandalizi ya ligi yetu yamekamilika japo tumechelewa kuanza na mkoa wetu ni miongoni mwa mikoa iliyo na timu nyingi kutokana na uwingi wa wilaya zilizopo hivyo tutachelewa pia kumaliza.
Lakini tumechelewa kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wetu," alisema Mwamwaja.