Stars nje Kombe la Nile
Tuesday, 11 January 2011 19:56 newsroom
Na Mwandishi Maalum, Cairo
TAIFA Stars imetupwa nje ya michuano ya kuwania Kombe la Nile inayoendela mjini hapa, baada ya kushindwa kutinga nusu fainali
kwa kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Uganda. Stars ilianza mechi hiyo kwa matumaini makubwa ambapo katika dakika za mwanzo ilifanya mashambulizi makali langoni kwa Uganda, ambayo ilionekana kubabaika kutokana na kasi ya Stars.
Mashambulizi hayo yalizaa matunda katika dakika ya 24 ambapo Athumani Machuppa anayecheza soka ya kulipwa nchini Sweden,
aliandika bao la kuongoza kwa shuti kali.Bao hilo lilijenga matumaini kuwa Stars ingeweza kuwamudu Waganda na kushinda mchezo huo, lakini hali iligeuka katika dakika ya 71, wakati Yudah Mugalu wa Uganda, alipoisawazishia timu yake alipofunga kwa kichwa kufuatia mpira wa kona. Mapema katika kipindi cha kwanza timu hizo zilishambuliana kwa zamu, ambapo Daniel Wagaluka nusura aipatie Uganda bao katika dakika ya 10, alipowatoka mabeki wa Stars na kupiga shuti kali lililoishia mikononi mwa kipa wa Stars, Juma Kaseja. Dakika mbili baadae, Kaseja aliokoa hatari katika lango la Tanzania kutokana na shuti jingine la Derick Walulya.
Baada ya Uganda kwenda mapumziko ikiwa nyuma kwa bao moja, kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo timu hiyo ililisakama lango la Stars kwa dakika 10 za mwanzo, lakini washambuliaji wake walishindwa kulenga lango la Stars. Kocha Jan Poulsen kuona hivyo, alifanya mabadiliko kunusuru jahazi lake kwa kuwatoa Salum Machaku na Saidi Maulidi, na nafasi zao kuchukuliwa na Mrisho Ngasa na Idrissa Rajabu.
Mabadiliko hayo hayakuisaidia Stars, ambayo ilicheza vibaya na kuifanya Uganda kutawala karibu sehemu kubwa ya kipindi hicho,
hali iliyomlazimisha Poulsen kufanya mabadiliko mengine ya kuwatoa Machuppa na Shaaban Nditi, na nafasi zao kuchukuliwa na Jabir
Azizi na Ally Ahmed ëShibolií, lakini hakukuwa na mafanikio ya kupata bao la ushindi. Matokeo hayo yanaifanya Uganda iungane na Misri kucheza nusu fainali, wakati Stars ikisubiri Burundi ifungwe na Misri, ili ipate fursa ya kuwani nafasi ya tano. Lakini matumaini hayo yatapotea ikiwa Burundi itashinda kwani itakuwa imeshika mkia katika kundi lake.
Stars: Juma Kaseja, Shadrack Nsajigwa, Stephano Mwasika, Juma Nyoso, Aggrey Morris, Nurdin Bakari, Salum Machaku/Mrisho Ngasa, Shaaban Nditi/ Ally Ahmed ëShibolií, Nizar Khalfani, Athumani Machuppa/Jabir Azizi, Saidi Maulidi/Idrissa Rajabu.