Poulsen, wachezaji waapa kufa na Uganda
Imeandikwa na Amir Mhando, Cairo; Tarehe: 10th January 2011 @ 09:48 Imesomwa na watu: 232; Jumla ya maoni: 0
WACHEZAJI wa Taifa Stars na Kocha Mkuu, Jan Poulsen wamesema watakufa na Uganda kesho watakapokutana nayo katika mechi ya mwisho ya makundi ya michuano ya Bonde la Mto Nile.
Watanzania kwa mara nyingine juzi walitoka vichwa chini kwenye Uwanja wa Polisi mjini hapa baada ya dakika 90 kumalizika ikiwa imefungana bao 1-1 na Burundi.
"Nasikitika kwamba tumeshindwa kuifunga Burundi, tumecheza kadri ya uwezo wetu, lakini tumeshindwa kuzitumia nafasi tulizopata.
"Hili ni tatizo na yatupasa kubadilika, naamini vijana wameona na watabadilika," alisema Poulsen jana.
Stars imepata matumaini ya kufuzu nusu fainali baada ya juzi Misri kuifunga Uganda bao 1-0 lililofungwa dakika ya 90 na Haji Gedo kwenye mchezo uliofanyika Uwanja wa Arab Contractors.
Matokeo hayo yanaifanya Misri kutinga nusu fainali kwani imefikisha pointi sita, ambapo hata kama itafungwa mchezo wake wa mwisho kesho dhidi ya Burundi haitaathirika.
Ili Stars ifuzu nusu fainali itabidi iifunge Uganda kesho, kisha iombee Misri iifunge Burundi
ama itoke nayo sare, vinginevyo kama Burundi itashinda basi itabidi timu hizo ziangalie uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Mpaka sasa Stars imefungwa mabao sita na imefunga mawili, hivyo ina deni la mabao manne, wakati Burundi imefungwa manne na imefunga mawili huku nayo ikiwa na deni la mabao mawili.
Kundi hilo la A linaongozwa na Misri yenye pointi sita na mabao sita ya kufunga ikiwa imefungwa moja, wakati Uganda ni ya pili ikiwa na pointi tatu na mabao manne ya kufunga, ikiwa imefungwa mawili, huku Burundi ikiwa ya tatu na Stars ya mwisho.
Zote zina pointi moja ila tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
"Najua Uganda nayo itacheza kwa nguvu, lakini tutabadilika sana, haitakuwa kama tulivyocheza na Burundi.
Sijui nini kimetokea, lakini dakika 20 za mwisho ndiyo tulizinduka. "Tunahitaji kubadilika sana, mashindano ni magumu, kila timu inacheza kwa nguvu sana," alisema Poulsen.
Nahodha wa timu hiyo, Shadrack Nsajigwa alisema wamepania kuibuka na ushindi na kwamba ama zao Uganda ama Stars.
Pia kipa Juma Kaseja naye alizungumzia mechi hiyo na kusema Waganda wataipata kwani wameshaona uchezaji wao, ingawa wenzao waliibana Misri na kufungwa bao 1-0, wakati Stars ilifungwa mabao 5-1.
Kwa upande wa Kundi B, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), inamaliza kesho na Sudan ambayo mchezo wa kwanza ilifungwa bao 1-0 na Kenya kabla ya DRC kuifunga Kenya bao 1-0.
Kutokana na mazingira hayo, timu za kufuzu nusu fainali kundi hilo bado tata, kwani hata Sudani ikiifunga DRC kesho nayo inaweza kufuzu nusu fainali.
Timu mbili za juu kila kundi zitaingia nusu fainali, ambapo Kundi B lenyewe lina timu tatu wakati A lina timu nne.
Kulingana na ratiba ya michuano hiyo ambayo zawadi kwa bingwa ni kombe na fedha taslimu zaidi ya Sh milioni 200 za Tanzania, washindi wa tatu kila kundi watacheza kuwania nafasi ya tano.