Aibuka bingwa kombe la Mwenyekiti
Imeandikwa na Mwandishi Wetu; Tarehe: 10th January 2011 @ 23:35 Imesomwa na watu: 19; Jumla ya maoni: 0
MCHEZAJI gofu chipukizi kutoka Klabu ya Gymkhana Arusha (AGC), Nuru Mollel juzi aliibuka bingwa wa michuano ya Kombe la Mwenyekiti ambayo ilikuwa ni kiporo cha kalenda ya mashindano ya Chama cha Gofu Tanzania (TGU) ya mwaka 2010.
Michuano hiyo ya siku mbili ya viwanja 36 ambayo ilikutanisha wachezaji kutoka klabu mbalimbali nchini ilifanyika kwenye viwanja vya Klabu ya Gymkhana Moshi, Kilimanjaro.
Nuru, ambaye mwishoni mwa wiki iliyopita pia alipewa tuzo ya mchezaji mdogo zaidi kwenye timu ya taifa, aliibuka bingwa baada ya kukusanya mikwaju gross 147.
Chipukizi huyo alianza michuano akiwa na mikwaju 72 kabla ya kurejea na 75 siku ya pili na kuondoka na Kombe ambalo alikabidhiwa na mwenyekiti wa TGU, Dioniz Malinzi wakati wa sherehe za kutoa zawadi.
Nafasi ya pili kwenye michuano hiyo ilichukuliwa na Hamis Ally kutoka Klabu ya Gymkhana Dar es Salaam (DGC) ambaye alikuwa na mikwaju 148.
Ally, ambaye alianza na mikwaju 71 kabla ya kumaliza na 77, amepata mafanikio yake ya kwanza kwa zaidi ya mwaka katika mashindano hayo ya mwisho.
Nafasi ya tatu ilikwenda kwa mchezaji wa DGC pia Adam Mwanyenza ambaye alikusanya mikwaju 150 (75, 75).
Elisante Lembris alishika nafasi ya nne akiwa na ikwaju 151 (77, 74), nafasi ya tano ilikwenda kwa John Saidi 152 (78, 74) na Jimmy Mollel (79, 74) alishika nafasi ya sita 153 wote kutoka AGC.
Mbali na mpambano huo kulikuwa na makundi mengine yaliyoalikwa kwa upande wa wanaume na wanawake na vijana wadogo.
Kwa upande wa wanawake chipukizi Vailet Peter aliibuka mshindi akiwa na mikwaju nett 136 baada ya kupiga kikwaju 65 siku ya kwanza na 71 siku ya mwisho huku Shazi Myombe akishika nafasi ya pili wote kutoka DGC.
Isaac Anania aliibuka mshindi kwa vijana wenye umri chini ya miaka 18 akiwa na mikwaju gross 163 ( 83,80) na nafasi ya pili kwenda kwa Vincent Gullo (164) 89, 75).
Akizungumza wakati wa hafla ya kutoa zawadi Mwenyekiti wa TGU, Malinzi aliwataka wachezaji kujenga nidhamu hasa kwa wale watakaochaguliwa timu ya taifa.
Alisema wachezaji wengi hawafahamu umuhimu wa kuchezea timu ya taifa hivyo yeyote atakayekamatwa atakuwa amejiondoa na hakutakuwa na msamaha katika hilo.