Tutasahihisha makosa-Poulsen
Imeandikwa na Amir Mhando, Cairo; Tarehe: 6th January 2011 @ 23:59 Imesomwa na watu: 485; Jumla ya maoni: 0
Tanzania ‘Taifa Stars', juzi ilikubali kipigo cha mabao 5-1 kutoka kwa Misri ‘Mafarao' katika mchezo wa Kundi A katika michuano ya nchi za Bonde la Mto Nile uliofanyika Uwanja wa Arab Contractors mjini hapa.
Bao la kwanza lilifungwa na Said Khamdi dakika ya nne, kisha dakika kumi baadaye Mohammed Aboutrika alifunga la pili kabla ya beki Nadir Haroub ‘Cannavaro' kujifunga dakika tisa baadaye.
Said Khamdi alipachika bao la nne dakika ya 57 na la tano lilifungwa na Ahmed Ally dakika ya 74, huku lile la Stars likifungwa na Rashid Gumbo dakika ya 77, ambaye aliingia kipindi cha pili akitokea benchi.
Kesho Stars itacheza na Burundi ambayo nayo juzi ilifungwa mabao 3-1 na Uganda, hivyo ili Stars iweke hai matumaini ya kufuzu nusu fainali italazimika kushinda na kusubiri mchezo wa mwisho dhidi ya Uganda.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Poulsen alisema kipigo kimemchanganya lakini wamejifunza na watasahihisha makosa yao huku akisisitiza wamefungwa na timu bora Afrika.
Alisema Misri ipo katika 20 bora kwenye viwango vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) wakati Tanzania ni ya 116 hivyo kuna tofauti kubwa baina ya timu hizo.
"Misri ni timu nzuri Afrika na dunia kwa jumla, imecheza vizuri,ni mabingwa mara tatu mfululizo Afrika, lakini pia vijana wangu walipambana vilivyo ila walikutana na timu bora, naamini michezo ijayo tutaimarika, tumepata changamoto kubwa," alisema Poulsen.
Kocha huyo alieleza kuwa makosa machache waliyoyafanya wachezaji wake yalitumiwa vizuri na wapinzani wao kufunga na hiyo ilitokana na kucheza bila kuelewana dakika 20 za mwanzo.
"Watanzania tumejifunza mengi kwa mechi ya leo (juzi), faida yake itaonekana mechi zijazo," alisema Poulsen.
Alisema atatumia jana na leo kufanyia kazi dosari zilizojitokeza katika mchezo huo ili kuimarisha kikosi chake kabla ya kuivaa Burundi kesho na kisha Uganda Jumanne.
Naye Kocha Mkuu wa Misri, Hassan Shehata akizungumza baada ya mchezo huo aliisifu Stars kwamba ni timu nzuri, lakini inahitaji marekebisho kidogo na itatisha kwani ina wachezaji wengi chipukizi ambao watacheza kwa muda mrefu.
Alisema mpira ambao Stars ilicheza kipindi cha pili, kama ingecheza hivyo kipindi cha kwanza mchezo ungekuwa mgumu kwao na kusisitiza kuwa timu yake licha ya kupata ushindi mnono, lakini ilikabiliana na upinzani mkubwa.
Akizungumzia kipigo hicho, kipa Juma Kaseja alisema mchezo ulikuwa mgumu na makosa waliyoyafanya wenzao waliyatumia.
"Tuache utani Wamisri wapo vizuri, hata krosi zao wanazopiga si za mchezo, wanapiga mabomba, kwa kifupi wapo juu, lakini kama tunakutana nao mchezo mwingine tutawatuliza," alisema Kaseja ambaye mwezi uliopita aliibuka kipa bora wa michuano ya Chalenji.
Naye nahodha wa Misri, Wael Goma alisema michuano hiyo ya soka kwa nchi za Bonde la Mto Nile ni migumu na kwamba Tanzania si timu ya kubezwa, kwani ina wachezaji wenye miili midogo, lakini wana vipaji.
Michuano hiyo inashirikisha timu saba zilizogawanywa katika makundi mawili, ambapo timu mbili za juu kila kundi zitacheza nusu fainali, wakati timu zitakazoshika nafasi ya tatu kila kundi zitacheza kuwania mshindi wa tano. Bingwa wa michuano hiyo atazawadiwa zaidi ya Sh milioni 200 za Tanzania.