Shindano la kuibua nyota wapya wa muziki laja
Monday, 06 December 2010 21:27
Zaina Malongo
SHINDANO maarufu la kusaka wanamuziki nyota wapya wa muziki wa dansi linatarajiwa kufanyika mwakani nchini kote.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, mratibu wa shindano hilo, Suleiman Matthew ambaye ni mmiliki wa Kampuni ya Makukwe Entertaiment alisema lengo lao ni kusaka vijana wapya wenye uwezo wa kuimba muziki wa dansi.
Kama walivyokuwa Dk Remmy Ongala (ambaye kwa sasa anaumwa), Hassan Rehani 'Bitchuka', Mzee Makassy, Muhidin Gurumo (pia ni mgonjwa) au kina Marijani Shaaban, John Kijiko na Mbaraka Mwinshehe (marehemu).
"Kuna vijana wengi wanapenda kuwa wanamuziki, lakini ni wachache wanaotambua aina ya muziki ambao wanaufanya kwa amaani hiyo tumeamua kuwakutanisha vijana kwa njia ya shindano la kusaka vipaji,"alisema Matthew
Matthew, ambaye ni mwanamichezo mstaafu nchini alisema kuimba muziki ni jambo dogo, lakini ugumu wake unakuja kuwa pale ni muziki gani unaoimbwa na kama unakubalika kwa watu.
Alisema shindano hilo litafanyika katika hatua ya kwanza au mchujo Desemba 21 na itawahusisha vijana wa Dar es Salaam pekee.
Alisema wameamua kuanzia Dar es Salaam ambapo kwa hatua ya pili kama tutapata wadhamini wataenda mikoani.