Ronaldo afunga mawili Real amkimbia Messi
Tuesday, 04 January 2011 20:40
BARCELONA, Hispania
WINGA Cristiano Ronaldo amefunga mabao mawili na kuiwezesha Real Madrid kushinda kwa mabao 3-2 dhidi ya jirani zao Getafe katika mchezo wa Ligi Kuu ya Hispania.
Idadi hiyo ya mabao imemfikisha Ronaldo kileleni akiwa nayo 19 msimu huu baada ya mechi 17 na kumwacha mpinzani wake, Lionel Messi wa Barcelona mwenye mabao 17.
Ushindi huo umeiacha Real chini yaJose Mourinho ikiwa nyuma ya Barca kwa tofauti ya pointi mbili.
Katika mchezo huo baina ya wapinzani wa jiji la Madrid, Real waliongoza kwa mabao 2-0 hadi mapumziko kupitia kwao, Ronaldo na Mesut Oezil, lakini Daniel Parejo aliipa Getafe bao moja.
Ronaldo aliongeza jingine kwa Real Madrid mwanzo wa kipindi cha tatu na kuonyesha kuwa mchezo huo ulikuwa umekamilika kwa timu yake.
Kiungo Kaka alichezeshwa kwa mara ya kwanza tangu mwezi Agosti alipofanyiwa upasuaji baada ya fainali za Kombe la Dunia.
Hata hivyo, Madrid walijikuta wakipunguzwa kasi kwa kutolewa Alvaro Arbeloa kwa kadi nyekundu, kitendo ambacho kiliizindua Getafe na kupachika bao la pili kupitia kwake Jorge Angel Albin, dakika ya 84.
Lakini, Real walishikilia hapo na kumaliza mchezo kwa matokeo hayo ambayo yametibua rekodi ya ushindi ya Getafe ya mechi nne za ligi.
Mourinho alieleza baada ya mchezo huo kuwa hakufurahishwa na mchezo wa vinana wake.
"Sikupenda jinsi timu yangu ilivyocheza," alisema Mourinho. "Kwa kawaida Real imekuwa ni imara, lakini si katika mchezo wa jana. Timu yangu inatakiwa kujilinda vizuri zaidi, hiki ndicho kinachoitambulisha timu."
Kwa muda mwingi wa mchezo Getafe walijaribu kuwazuia Real, lakini mashambulizi ya Ronaldo, Oezil, Angel Di Maria na Karim Benzema yaliwasambaratisha.
Ronaldo, pia alifunga mabao mawili katika mechi dhidi ya Getafe kwenye Uwanja wa Alfonso Perez na alikaribia kufanya hivyo baada ya kufunga la awali kwa timu yake mwanzo wa mchezo kwa penalti, dakika ya 11.
Winga Di Maria alizawadiwa mkwaju huo baada ya kuzuiwa kwa mkono na beki Jose Manuel "Mane" Jimenez.
Dakika nane baadaye , Di Maria alimtengenezea chumba safi Oezil akiwa katikati ya walinzi wa Getafe na kiungo huyo Mjerumani alitumia pasi hiyo kumtungua kipa Jordi Codina.
Wakiwa chini kwa mabao mawili, Getafe walicharuka, wakamiliki mpira na kuitesa ngome ya Madrid. Waliweza kujibu kwa bao la dakika ya 29 la Parejo likitokana na juhudi binafsi.
Kiungo huyo wa zamani wa Madrid aliwachana mabeki wawili kabla ya kutumbukiza mpira wavuni.
Uhai huo wa Getafe haukuwazuia Madrid ambao walionekana kuwa hatari zaidi katika mashambulizi wakimtumia Benzema ambaye alikuwa akimpa pasi murua Ronaldo, aliyekaribia kufunga bao dakika tano baadaye.
Kasi ya Real haikupungua kipindi cha pili na katika dakika ya 57, Oezil alinasa mpira na kumpa pasi Benzema ambaye alimsogezea Ronaldo ambaye alifunga bao lake la 27 msimu huu kutokana na mechi 25 alizocheza.
Kaka, ambaye alicheza kwa dakika 15 za mwisho, alisema alikuwa mwenye furaha kwa kuweza kurudi uwanjani na kuonyesha kuwa ameanza kupata nafuu.
"Kwa sasa hofu yangu imeisha, nilidhani sitaweza kucheza tena mpira, sasa ninaweza kuendelea na mpango wangu wa kupona," alieleza kiungo huyo wa Brazil.
Zikiwa zimebaki dakika nane, Arbeloa alitolewa kwa kadi ya pili ya njano baada ya kudaka mpira na Albin, ambaye alikuwa ameingia uwanjani kipindi cha pili alitumia makosa kwenye safu ya ulinzi na kuipa Getafe bao la pili, hata hivyo halikutosha kuwapa pointi.
Mapema , Villarreal iliilaza Almeria 2-0 kwenye mchezo mwingine wa ligi na kuzidi kushika nafasi ya tatu.
Beki wao (Villarreal) Jose Manuel Catala alifunga bao la dakika ya 22 kwa kichwa kutokana na mpira wa adhabu ndogo wa Bruno Valero, ambaye alifunga la pili kwa Villarreal, dakika ya 58.
Kocha Juan Carlos Garrido aliisifu ngome yake ambayo imeiwezesha Villarreal kupata ushindi wa nane kwenye mechi tisa zilizopita kwenye Uwanja wa El Madrigal . Villarreal wameizidi Valencia kwa pointi tano.
Matokeo mengine , Mallorca3-0 Hercules, Atletico Madrid 0-0 Racing Santander na Zaragoza2-1 Real Sociedad .
Kwa matokeo hayo, Mallorca imekaribia kukata tiketi ya kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao huku kikiwa kipigo cha kwanza kwa Hercules kwa wiki tatu zilizopita.
Jumapili, Barcelona iliilaza Levante 2-1, Valencia iliifunga Espanyol 2-1. Deportivo La Coruna ikaiadhiri Athletic Bilbao 2-1, Sevilla ikaishinda Osasuna 1-0 na Malaga ilipata ushindi wa 2-1 dhidi ya Sporting Gijon.