Zanzibar wauona mwaka mpya kwa filamu
Imeandikwa na Mwandishi Wetu, Zanzibar; Tarehe: 31st December 2010 @ 23:30
WAKAZI wa Zanzibar jana waliingia katika pilikapilika za mwaka mpya kwa staili tofauti na moja, ikiwa ni kuangalia sinema zilizotengenezwa hapa nchini na mastaa mbalimbali akiwemo akina Kanumba.
Kwa usiku wa jana sinema mbili zilioneshwa katika Mji Mkongwe kwenye ukumbi wa wazi wa sinema. Sinema hizo ni This is it ya Kanumba na Huba ya Ahmed Olutu.
Sinema hizo mbili ni sehemu ya tamasha la sinema za Bongo ambalo washindi wake wawili watapata nafasi ya kuonesha filamu hizo katika tamasha la Fespaco huko Burkina Faso.
Tamasha hilo dogo lililoandaliwa na Zanzibar International Film Festival (ZIFF) pia limelenga kutoa muamsho kwa Tamasha kubwa la ZIFF litakalofanyika kuanzia Julai 2-10 mwaka huu.
Tamasha hili dogo linalojumuisha filamu za kitanzania peke yake (Bongo Films) ili kuendelea kutoa mwamko kwa watengenezaji filamu wa Tanzania kufanya vyema katika tasnia hii, limelenga kuonesha filamu sita kwa nafasi.
Kama ilivyo ada ya Tamasha la Filamu la Nchi za Majahazi, usiku kulikuwa na burudani ya muziki.
Katika siku za tamasha hilo dogo makundi mbalimbali ya wanamuziki akiwamo Mwasiti, Marlaw, Mataluma, Amin, Barnaba, Pipi, THT Dancers watakuwepo kutumbuiza.
Kwa mujibu wa meneja wa tamasha Daniel Nyalusi leo kutakuwa na sinema mbili za Don't Cry ya Haji Adam na Divorce yaVincent Kigosi.