Taifa Stars yaanza kambi
Imeandikwa na Mwandishi Wetu; Tarehe: 27th December 2010 @ 23:55
WACHEZAJI wote 23 walioitwa kwenye kikosi cha timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars waliripoti kambini Dar es Salaam jana.
Stars iko kwenye maandalizi ya michuano maalumu ya mto Nile inayotarajiwa kuanza Januari 5 mjini Cairo, Misri.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kocha msaidizi wa Stars, Silvestre Marsh alisema wachezaji wake wote walifika na wanatarajiwa kuanza mazoezi rasmi leo kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.
"Wachezaji wangu wote wapo leo (jana) tumekusanyika pamoja na kuelezana mawili matatu lakini kesho (leo) ndio tutaanza mazoezi rasmi," alisema.
Kuhusu wachezaji wanaotoka Simba na Yanga ambao viongozi wao walisema hawataki wajiunge Stars kwa vile michuano hiyo inavuruga programu zao, Marsh alisema:
"Mimi hayo siyajui lakini wachezaji wangu wote wapo, ninao hata hao wa Simba na Yanga, sasa labda kama wanasubiri waingie kambini kwanza halafu ndio taratibu za kuwazuia zifuate," alisema.
Naye Kaimu katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Sunday Kayuni alisema hana taarifa kama Simba na Yanga hawataki wachezaji wao wajiunge kambi ya Stars.
"Mimi niliwaandikia barua viongozi wote kuwajulisha kuwa tunawahitaji wachezaji, sasa kama wao hawataki wanatakiwa waandike barua pia, na si kuzungumza kwenye vyombo vya habari, mimi huwa sifanyii kazi taarifa za kusikia," alisema.
Wachezaji wanaocheza soka ya kulipwa walioitwa kwenye timu hiyo tayari walishafika jijini tangu juzi ambao ni Henry Joseph anayecheza Kongsvinger ya Norway, Saidi Maulidi ‘SMG' anayecheza Bravos Do Maquis ya Angola, Nizar Khalfani anayecheza Van Couver Whitecaps ya Canada, Athumani Machuppa anayecheza Vasalund IF ya Sweden na Idrissa Rajabu anayecheza Sofapaka ya Kenya.
Kikosi kamili cha wachezaji wanaounda timu hiyo ni Makipa: Juma Kaseja (Simba), Shaaban Kado (Mtibwa) na Said Mohamed(Majimaji).
Walinzi ni Shadrack Nsajigwa, Stephano Mwasika , Nadur Haroub ‘Canavaro'(Yanga), Aggrey Morris, (Azam), Kelvin Yondani, Jumma Nyosso, (Simba).
Viungo: Idrissa Rajabu (Sofapaka, Kenya), Nurdin Bakari, Abdi Kassim ‘Babi', (Yanga), Shaaban Nditti (Mtibwa), Henry Joseph, (Norway), Jabir Aziz.
Washambuliaji ni Salum Machaku (Mtibwa), Mrisho Ngassa (Azam), Nizar Khalfan, (Canada), Godfrey Taita (Kagera Sugar), Athuman Machuppa, (Sweden), Jerry Tegete, (Yanga) Said Maulid (Angola) na Ali Ahmed Shiboli (Simba).
Stars inatarajiwa kwenda Misri Januari 2, mbali na Tanzania, nchi nyingine zinazoshiriki katika michuano hiyo inayoshirikisha nchi zilizo ukanda wa ziwa Victoria na mto Nile ni Kenya, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Eritrea, Ethiopia, Sudan na wenyeji Misri.
Lengo la michuano hiyo ni kuhamasisha kutunza vyanzo vya maji kwa ajili ya vizazi vijavyo. Kwa mujibu wa ratiba, Stars itaanza kufungua dimba la michuano hiyo dhidi ya wenyeji Misri Januari 5 saa moja jioni, kabla ya mechi hiyo Kenya itacheza na Sudan saa kumi jioni.
Stars itacheza mechi nyingine dhidi ya Sudan Januari 11 kabla ya kumenyana na Kenya Januari 14 na kisha itamaliza na Uganda Januari 17.