Mdakuzi mkuu
JF-Expert Member
- Dec 27, 2016
- 212
- 719
Mhariri wa Mafunzo wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Allan Lawa amelazwa katika Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (Moi) baada ya kujeruhiwa na majambazi waliomvamia nyumbani kwake usiku wa kuamkia leo (Alhamisi).
Mtoto wake, Isack Lawa amesema kwamba baba yake alivamiwa juzi saa saba usiku nyumbani kwake Tabata Bonyokwa na kumkatakata kwa mapanga na kisha kuchukua Sh1.5 milioni zilikuwapo.
“Jana usiku baba alivamiwa, mwenyewe anasema walikuwa ni vijana watatu waliovaa kininja. Walimkatakata kwa mapanga lakini mama yeye alipigwa kidogo hakuumizwa sana. Msichana wa kazi na wajukuu hawakuguswa kabisa,” amesema Isack.
Isack amesema baada ya tukio hilo, alipigiwa simu na majirani saa 8:30 usiku na akawahi nyumbani lakini alikuta baba yake ameshapelekwa Hospitali ya Amana.
Majirani waliripoti katika vituo vya polisi Buguruni na Stakishari.
“Nilifika ndani tu nikakuta vitu vimevunjikavunjika na damu zimetapakaa sebuleni, ikanibidi nielekee huko hospitali. Nilikuta bado yupo mapokezi baada ya muda kidogo akapatiwa huduma ya kwanza,” amesema Isack na kuongeza:
“Baada ya kupewa huduma ya kwanza, tulimhamisha na kumpeleka Hospitali ya Regency, ambako kutokana na hali aliyokuwa nayo, madaktari walishauri tumpeleke Muhimbili.”
Isack amesema, Lawa amejeruhiwa maeneo yote ya mwili lakini zaidi kichwani, kifuani na mikononi ambako kidole kidogo cha mkono wa kushoto kilikatwa kabisa, huku baadhi ya mishipa katika mikono nayo ilikatwa.
Hata hivyo, Isack amesema baada ya kipimo cha X-ray imeonekana hajapata majeraha ya fuvu ila sehemu ya kifua ndiyo iliyodhurika zaidi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni hakupatikana baada ya simu yake kuita bila kupokewa.
Chanzo: MWANANCHI