Fedha za kusaka urais ni bilioni 5/-.
Ni mara tano ya pendekezo la Tendwa
Ubunge nao sasa ni Sh. milioni 50
Vyama vyawasilisha mapendekezo
Mwenyekiti wa United Democratic Party UDP), John Cheyo
Hatimayep; mvutano kati ya vyama vya siasa na Msajili wa vyama hivyo nchini kuhusu fedha anazopaswa kutumia mgombea urais kuanzia mchakato wa kuteuliwa na chama hadi kampeni wakati wa Uchaguzi Mkuu, umefikia tamati baada ya kukubaliana kwamba, zisizidi Sh. bilioni tano.
Makubaliano hayo, ni moja ya maazimio kadhaa yaliyofikiwa katika mkutano wa pamoja kati ya Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa na vyama hivyo uliofanyika kwa siku mbili mfululizo, jijini Dar es Salaam, kuanzia Jumatatu wiki hii.
Wanasiasa hao walikutana na Tendwa katika siku hizo kwa lengo la kujadili rasimu ya kanuni na taratibu zitakazotumika wakati wa uchaguzi kwa mujibu wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi iliyotiwa saini na Rais Jakaya Kikwete Machi 17, mwaka huu.
Habari zilizopatikana baadaye zinaeleza kuwa mara baada ya majadiliano marefu, Tendwa na wanasiasa hao walikubaliana kimsingi, kwamba mgombea urais atumie fedha zisizozidi Sh. bilioni tano, kuanzia mchakato wa kuteuliwa na chama hadi kampeni wakati wa Uchaguzi Mkuu.
Kabla ya makubaliano hayo kufikiwa, Tendwa alipendekeza kuwa mgombea wa urais asitumie zaidi ya Sh. bilioni moja, lakini pendekezo hilo lilipingwa na vyama vya siasa, kwa maelezo kuwa kiasi hicho ni kidogo na kwamba hakiwezi kumwezesha mgombea kumudu gharama za kumfikisha katika maeneo yote ya nchi.
Kwa mujibu wa maazimio kati ya Tendwa na vyama vya siasa, fedha anazopaswa kutumia mgombea wa kiti cha ubunge zimegawanywa kulingana na jimbo.
Katika mgawanyo huo, wadau hao wamekubaliana kuwa mgombea atakayewania kiti hicho katika majimbo yaliyoko makao makuu ya mkoa, fedha atakazotumia zisizidi Sh. milioni 50.
Atakayewania kiti hicho katika majimbo yaliyoko katika mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza zisizidi Sh. milioni 40.
Kuhusu majimbo mengine, itategemea na wananchi, kilisema chanzo chetu mara baada ya kikao hicho.
Chanzo hicho kimefafanua kuwa maeneo yenye wananchi kuanzia 150,000 hadi 300,000, fedha anazotakiwa kutumia mgombea wa kiti hicho zisizidi Sh. milioni 45.
Pia maeneo yenye wananchi kuanzia 100,000 hadi 150,000, fedha anazotakiwa kutumia mgombea ubunge zisizidi Sh. milioni 35, wakati wananchi walio chini ya idadi hiyo, ni Sh. milioni 25.
Hata hivyo, kiwango anachopaswa kutumia mgombea udiwani hakikuweza kubainishwa katika makubaliano hayo, lakini awali Tendwa alipendekeza zisizidi Sh. milioni 10.
Chanzo hicho kimeeleza kuwa baada ya mkutano huo wa siku mbili kuhitimishwa jana, Tendwa na wadau hao watakutana tena Aprili 6, mwaka huu kwa ajili ya kutoa baraka za mwisho makubaliano yaliyofikiwa.
Habari zinasema kuwa baada ya hapo, rasimu ya makubaliano hayo itapelekwa kwa Waziri Mkuu kwa ajili ya kutiwa saini ili kuwa kanuni.
Awali, wakikosoa mapendekezo ya Msajili wa Vyama vya Siasa yaliyotaka mgombea urais asitumie zaidi ya Sh. bilioni moja, viongozi wa vyama vya siasa walisema kiasi hicho ni kidogo na hakiwezi kumwezesha mgombea urais kufika mikoa yote 26.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Matson Chizii, alipendekeza angalau kiasi hicho kiongezwe hadi kufikia Sh. bilioni 10 ili zimwezeshe mgombea kuwafikia wananchi katika maeneo yote ya nchi.
Aliongeza kuwa Sh. bilioni moja haziwezi kutosha kukodisha magari na mafuta ya kuzunguka mikoa yote 26 na kwamba kiasi hicho kwa mtu anayegombea urais kinaweza kukatika kwa kampeni za mikoa miwili tu.
Mwenyekiti wa United Democratic Party UDP), John Cheyo, alisema ingawa ni vigumu kufanya makadirio ya gharama halisi za mgombea urais, kiasi kilichotajwa na Tendwa ni kidogo sana kwa kuwa kugombea nafasi hiyo ni jukumu zito.
Alisema kutokana na miundombinu mibovu, inakuwa vigumu kuwafikia wananchi, hivyo baadhi ya wagombea hulazimika kutumia helikopta ambayo ni gharama kubwa kuikodisha.
Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika, alisema kwa gharama ya Sh. bilioni moja haiwezi kuwa rahisi kwa mgombea urais kwani gharama za maisha zimepanda kwa kiwango kikubwa.
Alipendekeza angalau kiwekwe kiwango cha Sh. bilioni tano kwa mgombea urais na Sh. milioni 50 kwa wagombea wa ubunge.
Mwakilishi wa NCCR-Mageuzi, Beati Mpitabakana, ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho, alisema kiasi hicho hakitoshi na alipendekeza kiongezwe hadi kufikia angalau sh. bilioni tano.
Rais wa Tanzania Democratic Alliance (Tadea), John Lifa Chipaka, alisema kiasi hicho ni kidogo sana na kupendekeza kiongezwe hadi kufikia Sh. bilioni tano.
Mwenyekiti wa Chama cha Ustawi Tanzania (Chausta), James Mapalala, alisema Sh. bilioni tano hazitoshi kwa mgombea urais ambaye chama chake ni kipya na hakijawa na mtandao mkubwa wa nchi nzima.
Hata hivyo, Mbunge wa Karatu (Chadema), Dk. Willibroad Slaa, alitofautiana na wenzake kwa kusema kiasi hicho (cha sh. bilioni moja) kinaweza kutosha kama vyama hivyo havitahonga wapiga kura na alitoa mfano kuwa mwaka 2005, Chadema ilitumia sh. milioni 700 katika kampeni zake.
Naye Tendwa alisema ofisi yake ilitoa mapendekezo hayo ili wadau wayajadili, lakini kiasi hicho si uamuzi wa mwisho kama baadhi ya watu walivyotafsiri.
CHANZO: NIPASHE