Meseji za komredi Lowassa zanaswa | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Meseji za komredi Lowassa zanaswa

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by nngu007, Mar 8, 2012.

 1. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #1
  Mar 8, 2012
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 56
  Trophy Points: 145
  Mwandishi Wetu - RaiaMwema

  [​IMG]


  Siyoi Sumari


  CHADEMA kumng'oa mgombea ubunge CCM, mikakati yasukwa

  Wengine kortini, meneja kampeni asema ‘nilijua tu'


  WAKATI Chama cha Mapinduzi (CCM) kikiwa kimempitisha mgombea wake wa ubunge Arumeru Mashariki, Siyoi Sumari, kwa kuegemea kigezo cha manufaa ya kisiasa (political expediency) badala ya misingi ya kanuni za maadili (principles), upepo umegeuka kwa mgombea huyo na sasa, anaweza kuenguliwa katika kinyang'anyiro hicho kwa njia mbili, ama kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za rushwa au kwa pingamizi katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Raia Mwema, limeelezwa.

  Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambacho kimemsimamisha mwanachama wake, Joshua Nassari, sasa kinaendelea kukusanya ushahidi wa matumizi ya rushwa yanayoelekezwa kwa Sumari, ili kumuwekea pingamizi NEC, ambako, mgombea anaweza kuenguliwa kama anahusishwa na tuhuma za rushwa.

  Kwa mujibu wa taratibu za NEC, pingamizi huwekwa mara baada ya tume hiyo kuteua rasmi wa wagombea wa vyama kwa kuzingatia majina yaliyowasilishwa kwao na vyama husika.


  Kuhusu mkakati huo wa CHADEMA, Mkurugenzi wa masuala ya Bunge na Halmashauri wa chama hicho, John Mrema, amemueleza mwandishi wetu kwamba chama chake kinakusanya ushahidi na kikijiridhisha, kitaweka pingamizi.


  Lakini wakati hali ikiwa hivyo kwa CHADEMA kuvizia kumuwekea pingamizi Sumari (baada ya tume kufanya uteuzi rasmi wa wagombea), taarifa zaidi zinaeleza kuwa Takukuru inaweza kuwafikisha mahakamani baadhi ya wanachama wa CCM, wanaohusishwa na matumizi ya rushwa wakati wa mchakato wa upigaji kura za maoni ndani ya CCM, Arumeru Mashariki.


  Katika taarifa hizo za Takukuru, mgombea Sumari naye anahusishwa katika uwezekano wa kufikishwa mahakamani pamoja na baadhi ya wanaCCM wanaotajwa kuwamo katika harakati za kumsaidia kushinda.


  Meneja wa Kampeni za CCM Arumeru Mashariki, Mwigulu Nchemba, amelieleza Raia Mwema; "Tunatarajia mambo matatu katika uchaguzi huu. Kwanza, tutawekewa pingamizi, hasa na CHADEMA, si kwa sababu mgombea wetu ana matatizo bali kwa wao kuhofia kushindwa.


  "Pili, tunataraji kushinda na tatu, tunajua wao watakwenda mahakamani kufungua kesi ya kupinga matokeo kwa sababu ni kawaida yao, wagombea wengi walioshindwa wamekuwa wakifungua kesi."


  Juu ya taarifa za yeye kuhojiwa na Takukuru kuhusu sakata la rushwa linalohusishwa na Sumari na wenzake, Mwigulu alisema: "Nimehojiwa kwa dakika kati ya 40 na 60 lakini na mimi pia nimewahoji baadhi ya mambo nikiwa kama kiongozi wa kampeni. Lakini najua mgombea wetu hana tatizo kama hao anaohusishwa nao ni wao, hakuna jambo linalomuunganisha nao kwamba aliwaelekeza kufanya hivyo."


  Katika hatua nyingine, mawasiliano ya ujumbe mfupi wa simu za mkononi yaliyonaswa na vyombo vya dola wakati wa mchakato wa kura za maoni CCM, Arumeru Mashariki "yamewaumbua" baadhi ya vigogo wa juu wa chama hicho, namna walivyoshiriki vitendo vya rushwa kumpitisha mgombea Siyoi Sumari.


  Mawasiliano hayo ni ya vigogo na makada wanaoelezwa kuwa ni wa mtandao wa Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond, Edward Lowassa, ndani ya CCM, ambaye anadaiwa kumuunga mkono Siyoi Sumari, ambaye pia ni mkwe wake.


  Imedaiwa kuwa mawasiliano hayo yalifanyika kati ya Februari 20 na Machi mosi, mwaka huu, ikiwa ni kipindi ambacho kulikuwa na mchakato wa kumpata mgombea wa ubunge kupitia chama hicho.


  Taarifa zinasema miongoni mwa mawasiliano hayo ni kati ya Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Wilaya Monduli, Ezekiel Joseph Mollel, ambaye alinaswa na Takukuru katika baa ya Levis, iliyoko eneo la Maji ya Chai, wilayani Arumeru, akiwa katika harakati zinazodaiwa ni za kutoa rushwa kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa wilaya.


  Kwa mujibu wa Kamanda wa Takukuru Arusha, Mbengwa Kasumambuto, pamoja na Mollel, wengine waliotiwa mbaroni kwa tuhuma za rushwa ni aliyekuwa mgombea wa nafasi ya ubunge Arumeru Mashariki, Elirehema Kaaya ambaye ni katibu mwenezi wa CCM, wilaya ya Nyamagana, Mwanza, na diwani wa kata ya Mbuguni ambaye ni mfanyabiashara maarufu wa madini ya tanzanite Thomas Mollel "Askofu" na katibu wa hamasa wa UVCCM, wilaya ya Arumeru, John Nyiti.


  Kasumambuto alisema Takukuru bado inaendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine zaidi ya watatu waliokimbia na kutelekeza pikipiki walizokuwa wakizitumia baada ya kukurupushwa na wenzao wakakamatwa, ambao majina yao yanahifadhiwa ili kuepuka kuingilia uchunguzi.


  Wana-CCM ambao simu zao zimenaswa katika mtandao wa mawasiliano hayo ni pamoja na Hussein Bashe; mwenyekiti UVCCM Arusha, James Millya, katibu UVCCM Arusha Abdalah Mpokwa, katibu UVCCM Monduli, Ezekiel Mollel na Siyoi Sumari mwenyewe, pamoja na makada wengine.


  Taarifa lilizopewa Raia Mwema kutoka vyanzo kadhaa zinaoonyesha kuwa kwa nyakati tofauti, kati ya Februari 20 hadi alipokamatwa, katibu huyo wa UVCCM Monduli amekuwa na mawasiliano na baadhi ya makada ambao wengine si wakazi wa Jimbo la Arumeru Mashariki kupitia simu yake (namba inahifadhiwa).


  Taarifa hizo zilidai kuwa katibu huyo ambaye kituo chake cha kazi ni Monduli alikwenda Arumeru kwa maelekezo ya kinachodaiwa kuwa mtandao wa Lowassa kusaidia kumpitisha Siyoi.


  Moja ya mawasiliano ya ujumbe wa simu unaodaiwa kutoka kwa James Millya kwenda kwa katibu huyo unaeleza: "Pole sana nipo Nairobi lakini hebu onana na Mheshimiwa (jina linahifadhiwa) umwambie haya mambo atakusadia. Ninakupa namba zake muda huu, Yeye ni mtu anafanya kazi serikalini na ana uwezo wa kusaidia kama jambo hili lina uonevu wa aina Yo yote".


  Ujumbe huo wa Millya ambao hata hivyo haukuweka bayana ni msaada upi Katibu huyo wa UVCCM alikuwa anauhitaji, ulirekodiwa Februari 26 saa 8:46 mchana, na baada ya dakika mbili, Millya alituma ujumbe wa kumpelekea namba ya simu ya ofisa huyo wa Serikali ambaye anafanya kazi katika moja ya idara nyeti.


  Mawasiliano mengine ambayo yanaelekeza kumpa maelekezo Katibu huyo ni kutoka kwa mtu anayeitwa "Comrade Lowassa" ambaye alifanya mawasiliano ya ujumbe mfupi (sms) Februari 29 saa (9:45).


  Ujumbe huo kutoka simu (namba inahifadhiwa) ulisomeka: "COMRADE hatuna muda tena wa kupoteza. Kuna mambo mawili makubwa, moja kuendelea kuwapanga vijana, kuomba kura na kuwahamasisha wajumbe kuendelea kujitokeza mkutanoni."


  Ujumbe huo uliendelea: "Mbili kuhamasisha vijana wengi wa kutosha kujitokeza kesho maeneo ya ukumbini kulinda kura kwa sababu wamejipanga kuchakachua.Naomba wewe unipe mpango-kazi sasa hivi"


  Mawasiliano hayo yanaoonyesha kuwa siku hiyo hiyo saa 9:53 "Comrade Lowassa" alituma ujumbe: "Sawa, kiasi gani? Mpokwa anasemaje? (Mpokwa ni katibu wa UVCCM mkoa wa Arusha) na saa 11:04 alituma ujumbe mwingine uliosomeka; "Usimweleze Mpokwa, endelea na kazi"


  Aidha, katika ujumbe mwingine "Comrade Lowassa" anamtahadharisha katibu huyo wa UVCCM kuhusu kuwapo maofisa wa Takukuru ambao walikuwa wanamfuatilia mgombea Siyoi Sumari na ujumbe huo ulisomeka: "Maafisa wa Takukuru waliopo Arumeru Mashariki kwa kumfuatilia Siyoi ni Adam Bwana, Seleman Mtunda, wafupi weusi, na Jacline Kapile"


  Mawasilaino hayo yanaoonyesha zaidi kuwa katibu huyo pia aliwasiliana na mtu anayedhaniwa kuwa ni naibu waziri Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Aggrey Mwanri na ujumbe wa mwanri ulisomeka: "Kaka, suala lako ni zito, na kuna viongozi wenzangu wa mkoa huu. Ungekuwa Moshi sawa. Na suala lenyewe ni la siasa, lingekuwa lako binafsi pia ungeweza. Unataka kunitia kitanzi?" Ujumbe huo wa Mwanri ulitumwa Februari 20 saa 9:15.


  Aidha, katibu huyo katika simu yake sehemu ya kutuma ujumbe (sent) inaonyesha kuwa alimtumia ujumbe mtu anayeitwa "Comrade Lowassa" na H.BASHE kuhusu hatua mbalimbali walizofikia katika mchakato wa uchaguzi huo hasa kuwafikia wajumbe wa mkutano mkuu.


  Ujumbe kwenda kwa "Comrade Lowassa" Februari 28 unasomeka: "Comrade nakushukuru sana kwa kunisadia simu, Bananga ameniambia umenitumia 150,000 japo bado nadaiwa 80,000 iliyotumika.


  Na tarehe 29 alituma tena ujumbe kwa "Comrade Lowassa" akieleza kuwa: "Nimewasiliana na Nyiti (katibu hamasa wa Vijana wilaya ya Arumeru) pamoja na kundi lake wapo 10. Wanasubiri, wameniambia wanahitaji mafuta ya pikipiki sita na hadi sasa kata sita ndiyo korofi ila Mbuguni nitakwenda na Nyiti.


  Ujumbe mwingine ulisomeka: "Pili amenipa 500 (500,000)? Na tumekubaliana mimi nimbane Nyiti, Je niwaeleze akina Mpokwa au niendelee na mchakato kaka?" na baada ya muda mfupi alituma ujumbe mwingine "Niko na Nyiti na wenzake tunapeana maelekezo nikimaliza nitakujulisha.


  Aidha ujumbe mwingine ulitumwa kwa H.BASHE (Hussein Bashe?) mwenye simu (namba inahifadhiwa) na ujumbe huo ulisomeka: "Hadi sasa kata za Kikwe, Ngarenanyuki, Songoro, Leguruki, Nkoaranga ndizo zinazonitesa."


  Akizunguzmia taarifa hizo, Kamanda wa Takukuru Mbengwa Kasumambuto, alieleza kuwa taasisi hiyo bado inafanya uchunguzi kuhusu tuhuma hizo na ni mapema mno kujenga mazingira ya kesi na kupeleka suala hilo mahakamani.


  Mgombea wa CCM anayetuhumiwa, Siyoi Sumari, amekanusha kuwa wanachama wa CCM waliokamatwa walikuwa wanamfanyia kampeni katika uchaguzi huo.


  "Nawashangaa wanaonihusisha mimi na suala hilo la rushwa. Mimi kama Siyoi sijawahi kupanga wala kumtuma mtu yeyote kumshawishi ye yote kwa fedha ili anifanyie kampeni. Hayo ni mambo yanayozushwa kwa lengo la kuniharibia kwa wananchi," alisema Siyoi.


  Uchaguzi wa marudio kumpata mgombea wa CCM katika jimbo hilo ulifanyika Machi Mosi kwa mgombea Siyoi Sumari kupata kura 761 na kumtupa mbali mpinzani wake, William Sarakikya aliyepata kura 361.
   
 2. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #2
  Mar 8, 2012
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 56
  Trophy Points: 145
  Wow Labda ndio Maana Lowassa yuko Germany Mgojwa...
   
 3. Mumwi

  Mumwi JF-Expert Member

  #3
  Mar 8, 2012
  Joined: Jan 9, 2011
  Messages: 592
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  Hii toka asubuhi watu walishaichangia sana.
   
 4. d

  dada jane JF-Expert Member

  #4
  Mar 8, 2012
  Joined: Dec 8, 2011
  Messages: 566
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  Mh! Mambo haya. Comrade si yuko kutibiwa jamani.
   
 5. Bumpkin Billionare

  Bumpkin Billionare JF-Expert Member

  #5
  Mar 8, 2012
  Joined: Jan 5, 2012
  Messages: 1,336
  Likes Received: 8
  Trophy Points: 0
  Nilijua wezi hawawezi kukaa kimya bila kuibakitu mwaka mzima
   
Loading...