Kudo
JF-Expert Member
- Nov 2, 2017
- 1,821
- 6,122
MDUNGUAJI WA GOMA:2
NA; BAHATI K MWAMBA
SIMU; 0758573660/0658564341.
1.
Zilikatika dakika thelathini bila mjumbe wa mwisho kuingia kwenye kikao cha dharura, simu zake hazikuwa zikipatikana na hata namba yake ya nyumbani haikupokelewa, jambo ambalo liliwafanya wajumbe wawili waliokuwa wamewahi kufika kwenye chumba cha mikutano, kuingiwa na wasiwasi. Kila walichojaribu kufikiria hakikuwashawishi kuendelea kusubiri zaidi ijapokuwa, hawakujua wafanye nini ili wasiendelee kungoja. Wote wawili walijikuta wakikigeuza chumba cha mkutano kama uwanja wa mazoezi ya kutembea, mmoja alitoka kushoto kwenda kulia huku akiburuza ulimi wake na kutoa sauti ya mfyonzo, mwingine akitoka kulia kwenda kushoto huku nae akiburuza ulimi wake mithili ya kinyonga amezae supu ya nzi. Kutembea kwao ndani ya kile chumba halikuwa zoezi pekee la kushughulisha miili yao, walitembea huku wakirusha mikono huku na huko kama mwalimu wa kwaya. Kiyoyozi kilichokuwa kikifanya kazi ya kupooza joto la miili yao ni kama kilikuwa likizo licha ya kuwa kilikuwa kikifanya kazi yake ipaswavyo, lakini hekaheka za wale mabwana zilificha kazi yake, miili yao ilitoa jasho la hofu, jasho la kiwewe na kihoro.
“Kwa mara ya kwanza Boys among men tumetikiswa na tumekubali kutikisika.” Hatimae mmoja wa wale mabwana alipata kauli iliyopenya kwenye ngome za masikio ya mwenzake, wote wakasimama huku kila mmoja akitazama upande wake bila kujali kama walikuwa ni wao ndani ya kile chumba.
‘Kiukweli tumetikiswa na tumetikisika ndani ya ngome yetu wenyewe, tumeruhusu mgeni aguse mikia yetu.” Mwingine nae aliunga hoja huku akimalizia kwa kusonya mithili ya mtu avutae uroto kwenye mfupa wa kuku wa kienyeji.
“Kama Omega' aliaga kwake na akatuthibitishia yupo njiani, lakini ghafla hapatikani na muda wa mkutano umelika kwa dakika zaidi ya arobaini, bila shaka kuna jambo na jambo laweza kuwa kubwa.” Yule alieanza kuongea awali, aliongea tena huku wakati huu akipitisha mkono wake wa kuume kwenye kichwa chake kilichootesha nywele chache zilizochangamana na mvi za kurashia, umri wake ulisogea karibu na miaka hamsini na saba au tisa kwa makadirio, mzee huyu mara nyingi alipenda kujiita Alpha’one na alikuwa ni kiongozi ndani ya kundi lao la watu watatu waliojiita, Boys among men. Kundi ambalo kilikuwa ni la kifedhuli na ujanja mwingi ndani na nje ya nchi, waliishi kwa kupora mali halali na zisizo halali ili mradi akaunti zao ziendelee kutuna na wao kuishi maisha ya anasa na starehe za kidunia. Wote watatu walikuwa ni wastaafu wa jeshi la wananchi, lakini ukwasi wao haukuwa sawa na viinua mgongo vyao wala vyeo walivyokuwa navyo jeshini. Siri ya utajiri wao waliijua wao na siri hiyo ilichagizwa zaidi na safari yao ya kutumikia jeshi la kulinda amani chini ya mwamvuli wa kulinda amani huko nchini Congo, nafasi hiyo waliitumia vema, waliiba madini na kuuza silaha haramu kila walipopata nafasi wakishirikiana na baadhi ya wanajeshi wa nchi ya Congo, ambao nao walikuwa watu wa kibaba hakijai bila kujazwa, watu wa michongo. Lakini siku zote watu husema, madini yana laana na mara nyingi wanaojihusisha nayo kwa njia haramu, huishia kubaya; kuuana ama kuzuliana chuki huwa ni laana ya kwanza kwa watu wa aina hiyo na ndivyo ilivyokuwa kwa hawa Boys among men. Wakiwa katikati ya kuhujumu nchi zao huku wakijitahidi kufua na kutakatisha pesa zao, walijikuta kwenye mgongano wa kimasilahi baina yao na kundi la wahujumu wa nchini Congo. Mgongano huo ukazua vita kubwa baina yao, lakini Boys among men wakaamua kukubali kushindwa na walifanya hivyo kwa sababu walikuwa nje ya nchi yao, wakachukua walichibakiza na kurejea nchini baada ya mkataba wao kumalizika, wakajiwekea himaya yao huku wakiendelea kutanua mikono yao haramu, walipohakikisha wamepata nguvu mpya na wanaukwasi wa kutosha, wakaamua kurejea nchini Congo kupambana na wabaya wao, lakini urejeaji wao haukuwa wa wao kupanda ndege na kutua kwenye ardhi ya Congo, walimtuma mtu, mtu wakazi ambae alienda kufanya walichomtuma mabwanyenye wale. Katikati ya kazi hiyo kuna kosa moja lilifanyika, kosa ambalo si huyo mammluki ama wao Boys aliyeligundua na wakaliacha bila kuwa na shaka na kosa hilo na hapo ukazuka ule usemi maarufu wa watu wa kale ambao ulisema; kisasi cha damu humaliza vizazi. Wahenga waliona mbali lakini kwa wakati huu haikuhitaji urithi wa vizazi, ilikuwa ni kisasi kwa walioanza kufanya na waliofanyiwa. Ilihitaji akili kutatua na kumaliza uhasama ulioanza kuota mizizi, lakini nani atabutua kopo na kuibuka mshindi wa jumla? Ikabaki kuwa kombolela ya wasichana na wavulana, kula na kula na kuliwa.
“Lakini bado sina hakika kama amejaa mtegoni.” Jamaa mwimgine ambae umri wake ulikuwa kati ya miaka hamsini na tano hadi hamsini na nane, mara nyingi wenzake walimuita Rich'one.
“Ngoja nipige simu yake kwa mara nyingine tena.” Alpha’one alisema huku akiingiza mkono kwenye moja ya mifuko ya suruali yake na kutoa simujanja, alibonyeza hapa na pale na kuweka sikioni na muda mfupi baadae aliitoa huku uso wake ukionekana kukunjamana kwa sononeko.
“Hapatikani!” Alisema huku akirejesha simu mfukoni mwake.
“Lakini kwa nini tuhofie vitisho?” Rich'one aliuliza huku akijikuna shavu lake la kushoto.
“Wasiwasi ndiyo akili lakini hivi si vitisho tu, kazi yao umeiona na hadi sasa tumepata hasara ya zaidi ya bilioni kumi na ushee, wamedhamiria haswaa!”
“Lakini swali la msingi kwa wote, ni kina nani hawa watu? Kwa nini wameamua kulenga sehemu tulizowekeza pesa nyingi?”
“Unachojiuliza ndicho ninachojiuliza pia, lakini kikubwa ni kuchukua tahadhari wakati tukiendelea kufuatilia kwa kina kilichonyuma ya haya yote na ni adui wa upande gani ambae ameamua kuja na fitina kubwa kiasi hiki.”
“Duh! Ila inani….!” Rich'one hakumalizia kauli yake, mlango wa chumba chao cha mkutano ulisukumwa kwa nguvu na sekunde chache baadae, mtu mmoja mfupi na mnene kiasi aliingia huku mwili wake ukionekana kutota kwa jasho, uso wake ulijaa wasiwasi mkubwa. Yule bwana alipoingia aligeuka na kuusukuma mlango nyuma yake, kisha akaufunga kwa komeo huku akihema kama mwanariadha aliyeshindwa kumaliza mbio. Muda wote wenzake walikuwa wakimtazama bila kusema neno.
“Tunawindwa!” Ilikuwa kauli ya kwanza kutoka kwa yule mtu, kauli ambayo iliwafanya wenzake wawe makini kusikia kauli nyingine ambayo ingeliwapa la kusema.
“Wakati natoka nyumbani nilihisi kuna kitu hakipo sawa, wakati nipo njiani shaka yangu ikatimia, kulikuwa na pikipiki ikinifuatilia kila nilipoenda na hata nilipojaribu kutumia uzoefu wa kulijua jiji, lakini bado mfuatiliaji hakukoma.” Jamaa alisema huku akichukua chupa ya maji iliyokuwa mezani na kuginda funda kadhaa za maji ili kutuliza koo.
“Kwa nini hukutoa taarifa ili abananishwe?” Rich'one alimuuliza.
“Niliamua kuzima simu zangu baada ya kuhisi alikuwa akitumia GPS kunifuatilia, maana kila kona niliyopiga na kuhisi nimempoteza, nilishangaa akiibuka nyuma yangu kama mzimu.”
“Ulifanya kosa kubwa sana bwana Omega'one, hatuishi hivyo. Toa taarifa kisha zima simu zako na ukiwa na uhakika ya kuwa kuna msaada unakufuata. Siku nyingine usifanye hivyo.” Alpha'one alimuonya.
“Kwa kuwa hamjui hali niliyokuwa nayo na…”
“Wewe ni mwanajeshi mstaafu, unatetereka vipi kirahisi namna hiyo?”
“Nilishindwa kujizuia baada ya kuhisi ubaya wa mtu aliyekuwa nyuma yangu na mtu yule alikuwa akinipa ujumbe kupitia mavazi yake, ndiyo sababu nikawa na wenge ndugu zangu.”
“Ujumbe? Ujumbe gani?”
“Ujumbe kutoka Congo, ujumbe wa kifo!”
“Umejuaje ni ujumbe wa kifo! Umejuaje ni ujumbe kutoka Congo?”
“Yule bwana alivaa jezi ya timu ya taifa ya Congo, kifuani kukiwa na picha ya bastola!.”
Chumba kikawa kimya kwa sekunde kadhaa, hakuna aliyesema wala kuguna, tafakari ikabaki vichwani mwao na hawakuwa tayari kupuuzia ujumbe kutoka kwa Omega'one ambae aliingia akiwa mwingi wa wasiwasi.
“Lakini inaweza kuwa ni vazi lake la kawaida.” Rich'one alisema huku akivutavuta mkia wa tai yake.
“Mh! Haiwezi kuwa ni kawaida, tangu lini jezi ya taifa ikaambatanishwa na picha ya silaha?” Alpha alihoji huku akimtazama Omega.
“Yule mtu ni mjuzi sana wa kutumia pikipiki, haonekanai kuwa kanjanja wa mjini.” Omega aliendelea kusisitiza shaka yake juu ya mtu aliyekuwa akimfuatilia tangu alipotoka nyumbani kwake.
“Huyu mtu alitutumia ujumbe wa vitisho usiku wa jana, tusisahau ni siku mbili visima vya kuhifadhia mafuta yetu kule Kigamboni vililipuliwa na bomu la kurusha kwa mkono, tumekula hasara kubwa na imetuacha na deni kubwa kwa kampuni zilizokuwa zimeshalipia kiasi kikubwa cha mafuta, kiukweli hatuhitaji kupuuza lolote hata kama linatoka kinywani mwa mtoto mchanga.” Alpha alisema huku akijikuna kichwa chake.
“Lakini tujiulize swali moja, kwa nini hajatudhuru hadi sasa?” Rich alichombeza swali huku macho yake yakiwatizama wenzake.
“Kwanza tuondoe kumtafsiri kama nafsi moja kwa sababu hatujui ni mmoja, wawili au ni zaidi ya idadi tunayoitabiria. Kama ni mmoja basi atakuwa ni profesheno wa kufanya kazi yake, anataka kutupa mateso ili atuwinde kirahisi lakini kama wapo wengi, mipango yao ni kuhakikisha wanajua maficho yetu kwa muda wote wanaotuwinda na mwisho watafanya walichokusudia.” Alpha alijibu kwa namna alivyokuwa akihisi.
“Lengo lake au tuseme lengo la kuwindwa kwetu ni nini? Hili ni swali ambalo tunapaswa kujiuliza kabla ya kuwaza njia ya kujiokoa.” Omega aliongea huku akikaa kwenye kiti kilichokuwa kando yake.
“Kama ulimuona mtu akiwa na vazi la nchi ya Congo, huko ndiko kunakotokea haya mashambulizi. Watu wanataka mali tuliyopora au pengine wanataka kulipiza kisasi kwa kile alichokifanya mamluki wetu.” Alpha alisema.
“Lakini si tulifagia wajinga wote?”
“Kuna mjinga mwingine aliachwa na pengine ndiye anaeweza kuwa anatuhujumu.”
“Nani?”
“Zibuabanda!"