Mbarali, Mbeya: DC asema ni vigumu kutenganisha kodi na maendeleo

beth

JF-Expert Member
Aug 19, 2012
3,877
6,326
Mkuu wa Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, Reuben Mfune, amewaambia wafanyabiashara wilayani humo ni vigumu kutenganisha kodi na maendeleo kwa kuwa maendeleo ya nchi yoyote hutegemea kodi.

Aliyasema hayo wakati wa semina ya wafanyabiashara katika kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendeshwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Semina hiyo ina lengo la kuwaelimisha masuala yanayohusu kodi, kusikiliza changamoto za kikodi, na kupokea maoni ili kuboresha huduma za TRA.

"Kodi huiwezesha serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini. Kwa mfano ujenzi wa barabara za lami, ujenzi wa reli ya kisasa, ujenzi wa zahanati na ununuzi wa dawa na mengine mengi, yote haya yanatekelezwa kwa kutumia kodi zinazolipwa na ninyi wananchi” alisema Mfune.

Alitoa mwito kwa wafanyabiashara hao wawe na tabia ya kulipa kodi kwa hiyari na wazitumie vizuri mashine za kielektroniki za kutolea risiti kwa kutoa risiti kila wanapouza bidhaa au huduma.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wilayani humo, Michael Mwaiteleke, alisema, kampeni hiyo licha ya kutoa elimu ya kodi lakini pia inajenga urafiki kati ya wafanyabiashara na TRA.

"Tunaipongeza TRA kwa kuona umuhimu wa kututembelea kwenye maduka yetu na kutuita kwa ajili ya kutuelimisha masuala ya kodi. Hali hii inajenga urafiki kati yetu sisi na TRA na inatupa hamasa ya kulipa kodi kwa hiari na kwa wakati", alisema Mwaiteleke.

Meneja wa TRA wilayani humo, Elly Jogofu, alikaribisha wafanyabiashara waende ofisini kwake au wampigie simu kutatua changamoto zinazowakabili zinazohusiana na kodi.

Chanzo: Habari Leo
 
Back
Top Bottom