Mawaziri wa Magufuli wananyemelewa na 'gonjwa hatari'

Interest

JF-Expert Member
Apr 11, 2015
3,434
7,067
NCHI inapendeza, viongozi wa serikali wapo ‘bize' kuwahi kutokea. Kila mmoja anafanya kazi kwa kujituma. Matukio ni mengi mno.

Mawaziri waliokula kiapo cha utiifu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, Jumamosi iliyopita, siku hiyohiyo bila kujali wikiendi waliingia ofisini. Hapa Kazi Tu!

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akiwa Hospitali ya Mwananyamala, naibu wake, Dk. Hamisi Kigwangala alikuwa Hospitali ya Amana. Mara akamvamia Dk. Mwaka bila hodi kwenye zahanati yake ya Foreplan. Hakuna anayetaka kuonekana jipu!

Waliambiwa hakuna sherehe, kwa hiyo baada tu ya kutoka kuapishwa, Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga, aliingia ofisini na kuagiza apewe mafaili, akaanza kazi hapohapo!

Mawaziri wa nchi wote, wale wa ofisi ya rais, makamu wa rais na waziri mkuu, inaelezwa hawakutoka Ikulu, kazi ilianza palepale. Upande mwingine wasaidizi wa Rais Magufuli katika maeneo mbalimbali walikuwa wakichangamsha nchi kwa mitindo mbalimbali.

"Nchi imechangamka, kila mtu sasa hivi ni mchapakazi, kila mtumishi wa umma siku hizi kawa jembe, ama kweli Magu siyo mchezo!" nilikiri mwenyewe bila kutoa sauti. Mkononi nilikuwa na gazeti naendelea kusoma.

"Eti sichomoi, kwani nimechomeka nini?" ilikuwa sauti ya Captain Nyambo ambaye alinifanya niache kuweka mkazo kwenye gazeti, nikamtazama.

Captain akaniambia: "Captain Mkuu niamini mimi, JK ni noma sana! Si mlikuwa mnasema hachomoi kutokana na kashfa ya utoroshwaji wa makontena bandarini kipindi cha utawala wake, sasa ameuliza hachomoi kwani alichomeka nini?"

Unajua Captain Nyambo alinivamia tu na maneno yake, hata hakuniandaa nijue anataka kusema nini. Nikabaki nimemtolea macho. Nilitamani kumwambia aondoke aniache niendelee kusoma gazeti lakini nilihofia kumuudhi mtoto wangu kipenzi.

Captain Nyambo bila kujishughulisha kujua kama ananiudhi au ananifurahisha kwa maneno yake, aliendelea:

"JK amesema hajawahi kuchomeka kitu, kwa hiyo hana cha kuchomoa, teh teh teh teh, JK noma sana baba."

"Captain Mkuu eeh," Captain Nyambo aliniita na nilipoitika alisema: "Huu ni mwaka wa tabu, Magu anakaza kule juu, anawapa mshikemshike wasaidizi wake ambao nao wanawakazia watu wa chini. Mwaka huu tutanyooka tu!"

"Utanyooka nini wakati wewe bado mtoto?" nilimuuliza.

"Ni hivi baba, ukishanyooka wewe, mimi nakuwa nimenyooka kabisa," alinijibu na kuongeza: "Baba usije ukalemaa, serikali ya Magufuli kila mtu sasa hivi ni mpenda sifa, kosa moja adhabu ya nguvu."

Nikamuuliza ni kwa nini anasema hivyo? Akanijibu: "Baba wewe huoni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda alivyowaweka mahabusu maofisa wa ardhi? Uliwahi kuiona hiyo katika serika zilizopita? Je, alivyoagiza Saed Kubenea awekwe ndani?"

Nilipomjibu hapana sijawahi kuona, akaendelea: "Baba huo ni moto wa Magufuli, wasaidizi wake wanaona jinsi anavyofanya kazi. Hana starehe, mwendo wa kubana matumizi na kuwashughulikia wazembe na mafisadi.

"Wakuu wa mikoa, wilaya, makatibu wakuu wa wizara na wakuu wa idara tofautitofauti nao imebidi waamke. Wanataka wafanya mambo ya kuonekana na Magufuli aone na akiri kwamba ni wachapakazi. Hapa Kazi Tu ni presha tupu kwa vigogo serikalini."

Kwa mfano kama ni wewe ungekuwa unazungumza na Captain Nyambo hapo ungechangia nini? Maana mtoto anatiririka mwenyewe na pointi zinashuka vizuri kabisa. Kama baba, kichwa changu kinavimba na namkubali kweli mwanangu.

"Captain Mkuu eeh," Captain Nyambo aliniita kwa mara nyingine. Akasema: "Umesikia agizo la Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Paza Mwamlima kuwa mtu akiumwa kipindupindu, akipona anafikishwa mahakamani ajibu mashtaka ya kwa nini amepata kipindupindu. Captain Mkuu huoni kama hiyo ni kiboko?"

Nikamjibu ni kali sana, akaendelea: "Huyu mheshimiwa Mwamlima akiwa Waziri wa Afya, anaweza kuagiza waathirika wote wa ugonjwa wa Ukimwi wakamatwe na washtakiwe kwa nini wamekubali kuambukizwa Ukimwi. Baba hii awamu ya Magufuli ni noma sana!"

"Captain Mkuu eeeh," kama kawaida yake aliniita na nilipoitika akaendelea: "Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Amos Makalla ameagiza watumishi wote wa umma mkoani kwake wasiende likizo kipindi hiki, wafanye kazi kufanikisha agizo la wanafunzi kusoma bure kuanzia Januari, mwakani. Ameagiza pia mmiliki wa kiwanda cha TCCCO akamatwe. Hapa Kazi Tu!"

Akasema: "Ila Captain Mkuu awamu hii ya Magufuli naamini serikali itaingia kwenye migogoro mingi na wanaharakati wa haki za binadamu pamoja na vyama vya wafanyakazi. Si unaona mabishano?

"Suala la ada elekezi limeibuka safari hii kwa hofu ya Magufuli, miaka yote shule binafsi zilikuwa zinajiongezea tu ada kulingana na matakwa ya wamililiki, leo hii ndiyo wameibuka na mkwara mzito. Nchi imekuwa ya mikwara, kila kiongozi amekuwa mchimba mkwara."

Hakika, Captain Nyambo alizungumza kitu ambacho ni halisi kabisa. Sasa hivi ukisikiliza vyombo vya habari tu utasikia kuna kiongozi fulani amechimba mkwara. Mara watu wa haki za binadamu wamejibu, kule vyama vya wafanyakazi vimetoa tamko kupingana na agizo la mamlaka ya serikali. Ni shida!

"Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Aman Mwenegoha amemfukuza kazi Mganga Mkuu wa Wilaya, Dk. Johanes Makobwe. Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Christopher Ngubiangai, amemsimamisha kazi Ofisa Afya wa Wilaya hiyo, James Ndembo. Je, kasi hiyo umewahi kuiona wapi?" Captain Nyambo aliniuliza, nikamjibu naiona chini ya Dk. Magufuli.

Akaendelea na pointi nyingine: "Sasa hivi ukitaka kusababisha kifo cha ghafla cha kigogo wa bandari au TRA ni rahisi sana. Wewe uwe tu na namba yake, subiri muda wa usiku umpigie kisha uige sauti ya Magufuli.

"Yule kigogo akisikia sauti tu ya Magufuli, wala hatasubiri neno lifuate, wewe tu utasikia kishindo kwenye simu tiiiiii. Kesho yake ukifuatilia utaambiwa amepooza mwili wote baada ya kupandwa na presha kutokana na mshtuko wa kiwango cha juu."

"Captain Mkuu eeh," Captain Nyambo aliniita tena, akasema: "Magufuli siyo wa kawaida, Tanzania imebadilika, kutoka taifa la wategeaji na wafanya kazi bila presha na sasa ni kazi tu."

Nikamuuliza Captain Nyambo: "Wewe umejifunza nini kutokana na uchapakazi wa watendaji serikalini?"
Akajibu: "Wanafanya vizuri lakini hawana ubunifu. Mtindo uleule ambao Magufuli ameanza nao ndiyo kila waziri, mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya na wengineo wanataka kwenda hivyohivyo. Wawe wabunifu basi, siyo kila mmoja afanye ziara za kushtukiza. Mimi sipendi kiongozi ambaye anapenda kupita tu njia za bosi wake bila kuonesha ubunifu.

"Ila Captain Mkuu nina shaka kubwa na mawaziri pamoja na wasaidizi wengine wa Magufuli," aliposema hivyo aliniangalia usoni, nilijua tu alitaka nimuulize, nikatii hitaji lake. "Shaka ya nini?"

Akasema: "Wapo wakipimwa watakutwa tayari wanaumwa Anxiety Disorders. Unaujua huo ugonjwa baba?" Haraka sana nilimjibu kuwa siujui.

Akaendelea: "Na wale ambao hawaumwi, basi siku zijazo wataupata. Wengi wananyemelewa."
Mpaka hapo alikuwa hajajibu swali, ndipo alifafanua: "Anxiety Disorder ni tawi la magonjwa ya akili (mental disorders) na chimbuko lake ni tatizo la kisaikolojia.

"Anxiety Disorders ni ugonjwa unaosababishwa na wasiwasi (worry) kwa matukio yanayokuja, vilevile hofu
(fear) ya mambo yaliyopo. Utaona kuwa wasaidizi wa Magufuli wengi wanafanya kazi kwa wasiwasi na hofu kubwa kutokana na kasi ambayo ameanza nayo.

"Vilevile ndani ya Anxiety Disorders kuna tawi linaitwa Social anxiety disorder ambao sababu yake ni hofu na wasiwasi wa kusimamiwa kwa ukaribu, kuhojiwahojiwa na kusumbuliwa mbele za watu. Hili eneo watalikwepaje? Magufuli anafuatilia kweli, maana anataka kuona matokeo."

Nilimwangalia Captain Nyambo kwa jicho la kutoamini, mtoto wangu mwenyewe anazungumza vitu vya kitaalam utadhani daktari. Nikamuuliza: "Mwanangu inabidi uwe daktari, unafaa sana. Tena daktari wa akili. Upo juu."

Akanijibu: "Ngoja kwanza baba, ugonjwa wa wasiwasi (anxiety disorder) chanzo chake ni msongo (stress) kwa mawazo na kufanya kazi kwa shinikizo (under pressure). Kwa hali ninayoiona, watu wengi wataumia sana kipindi cha Magufuli.

"Kuna mwanafunzi mwenzangu baba yake ni daktari, anasema aliambiwa na baba yake kuwa sasa hivi vigogo wengi wanakwenda kupima presha na kisukari hospitalini kwake. Hali ni mbaya baba yangu. Vigogo wananyemelewa na Anxiety Disorder, ukipeenda liite gonjwa la wasiwasi na hofu."

Mshangao wangu kwa mtoto wangu ulikuwa mkubwa mno, naye akanizindua: "Baba mbona leo upo doro sana? Nakuacha nini na huu uchambuzi wangu wa kisayansi na saikolojia?"

Nikamjibu hakika, akaniambia: "Basi ngoja nikwambie baba. Hatari ya wasiwasi na woga, husababisha tatizo la upumuaji ama mtu kupumua kwa shida kidogokidogo chini ya kiwango (hypoventilation) au pumzi kutoka harakaharaka kupita kiwango cha kawaida (hyperventilation).

"Na kwa kawaida hyperventilation husababisha shinikizo la chini la damu (hypotension) au wengine huita presha ya kushuka na hypoventilation huchagiza shinikizo la juu la damu (hypertension)."

Captain Nyambo akaendelea kushusha sayansi: "Matatizo ya presha yanajulikana, ni kifo cha ghafla au hata mtu kupata kiharusi kutokana na ama mishipa ipelekayo damu na oksijen kuziba au kupasuka. Hii ikufanye uone ni kiasi gani mawaziri na wasaidizi wengine wa Magufuli walivyo na hatari kubwa kwa kufanya kazi wasiwasi na hofu."

"Captain Mkuu eeh?" Captain Nyambo aliniita, nilipoitika alisema: "Kama sikosei ulinishauri nijitahidi nisome kwa bidii ili niwe daktari."

Nikamjibu: "Safi kabisa mtoto wangu, umeonesha mwanga mzuri bado mapema, udaktari unakufaa sana."
Captain Nyambo akaniuliza: "Nikishakuwa daktari na ndege ataendesha nani?"

By Luqman Maloto
 
Boring in its best, I must admit. The author is probably turning JF into a punching bag for his novelist career!
 
Back
Top Bottom