Mwananchi
Nusu wafeli mtihani darasa la saba,445,954 waenda kidato cha kwanza
Na Leon Bahati
WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imetangaza matokeo ya mtihani wa darasa la saba yanayoonyesha kuwa zaidi ya nusu ya wanafunzi watahiniwa wa mwaka huu, wamefeli huku 445,954 wakichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani.
Matokeo hayo yaliyotolewa jana yanaonyesha kuwa kati ya wanafunzi 999,070 waliofanya mtihani huo, wanafunzi 505,737 ambao ni sawa na asilimia 50.6 wamefeli na wanafunzi 493,333 ambao ni sawa na asilimia 49.4 wamefaulu.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, wasichana 285,374 na wavulana 220,363 wameshindwa mtihani huo kwa kupata chini ya alama 100 za jumla ya masomo yote. Kwa mujibu wa wizara, jumla ya alama za masomo yote ni 250 na kiwango cha juu cha ufaulu ilikuwa ni alama 235.
Akitangaza matokeo hayo jana, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Magembe alisema kati ya waliofaulu, wasichana ni 217,250 sawa na asilimia 43.3 na wavulana ni 276,083 sawa na asilimia 55.7.
Waziri alisema miongoni mwa waliofaulu tayari 445,954 wamechaguliwa kwenye awamu ya kwanza ya watakaojiunga kidato cha kwanza katika sekondari za serikali mwaka ujao.
"Wanafunzi 445,954, sawa na asilimia 89.5 ya waliofaulu, wamechaguliwa kuingia kidato cha kwanza katika sekondari za serikali," alisema Profesa Magembe.
Alibainisha kuwa awamu ya pili ya kuchagua watakaojiunga na sekondari hususan zile mpya za kata, unaendelea na matokeo yake yanatarajiwa kutangazwa wakati wowote.
Profesa Magembe alizitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha wanafunzi waliofaulu wanapata nafasi za kujiunga na kidato cha kwanza.
Kwa mwaka huu, waziri alisema alama ya juu ya ufaulu kitaifa kwa wavulana ni 235, wasichana 233 wakati ya chini kwa wote ni 100.
Akizungumzia kuhusu kiwango cha ufaulu, Profesa Magembe alisema mwaka huu umeshuka kwa asilimia 3.3 ikilinganishwa na mwaka jana.
Pamoja na hali hiyo, alisema mkoa wa Dar es Salaam ndio unaoongoza kwa kufaulu huku Shinyanga ikishika mkia wakati watahiniwa 579 wamefutiwa matokeo kutokana na tuhuma za kufanya udanganyifu.
Kwa mujibu wa takwimu za matokeo hayo zilizotolewa jana, Dar es Salaam inaongoza katika mikoa iliyofanya vizuri, ikifuatiwa na Arusha, Iringa, Manyara, Ruvuma, Kagera, Tanga, Pwani, Morogoro, Mwanza na Kilimanjaro.
Mikoa iliyoshika mkia, inaongozwa na Shinyanga, Singida, Tabora, Kigoma, Dodoma, Lindi, Mara, Mtwara, Mbeya na Rukwa.
Profesa Magembe alisema wanafunzi 1,024,488 walitarajiwa kufanya mtihani huo uliofanyika Septemba 9 na 10, lakini wanafunzi 25,418 walishindwa kufanya mtihani huo kutokana na sababu mbalimbali.
Ingawa sababu hizo hazikuwekwa wazi, waziri alisema kwamba tofauti na miaka mingine kigezo cha mwanafunzi kuzuiwa kwa sababu ya mimba hakikuwepo.
"Tangu mwaka jana, tuliagiza kwamba hata kama mwanafunzi atakuwa mjamzito, aruhusiwe kufanya mitihani," alisema Profesa Magembe.
Katika hali nyingine, Profesa Magembe alisema kwamba tatizo sugu la wanafunzi nchini kufanya vibaya katika masomo ya Kiingereza na hisabati, limeendelea kujirudia.
Katika somo la Kiingereza walifaulu kwa asilimia 35.4 na hisabati asilimia 21 hali ambayo Profesa Magembe alisema imepanda kidogo ikilinganishwa na mwaka jana.
"Ukilinganisha na mwaka jana utaona ufaulu wa masomo ya hisabati na Kiingereza, umepanda kutoka asilimia 31 hadi 35 na hisabati kutoka asilimia 18 hadi 20," alisema Magembe.
Pamoja na hali hiyo, Profesa Magembe alisema tatizo sugu la wanafunzi wa shule za msingi kutofaulu masomo hayo linatokana na msingi mbovu walio nao walimu wanaofundisha masomo hayo.
Alisema wizara imekusudia kuweka mkakati wa kuwapiga msasa walimu waliopo na nguvu kubwa zaidi itapelekwa kwenye vyuo vya walimu.
Ufaulu wa mwaka huu kwa kila somo alisema, Kiswahili ni asilimia 69.1, sayansi 53.4 na maarifa 59.5.
http://www.mwananchi.co.tz/newsrids.asp?id=16581