Mashindano ya Umisseta kuanza kesho | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mashindano ya Umisseta kuanza kesho

Discussion in 'Sports' started by Balantanda, Jun 27, 2009.

 1. Balantanda

  Balantanda JF-Expert Member

  #1
  Jun 27, 2009
  Joined: Jul 13, 2008
  Messages: 12,322
  Likes Received: 1,039
  Trophy Points: 280
  MASHINDANO ya Umoja wa michezo wa shule za sekondari Tanzania (Umisseta) baada ya kutofanyika kwa takribani miaka saba yanaanza kutimua vumbi kesho katika viwanja vya shule ya sekondari Kibaha mkoani Pwani. Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Hamisi Dihenga mashindano hayo ambayo yatashirikisha mikoa yote ya Tanzania iliyogawanywa katika kanda nane,yanatarajiwa kufunguliwa rasmi na Waziri Jumanne Maghembe.

  Dihenga alibainisha hayo jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na vyombo vya habari kwa niaba ya Waziri wa wizara hiyo Jumanne Maghembe juu ya kuanza kwa michuano hiyo baada ya michuano ya majaribio ya kurejeshwa kwa Umisseta iliyofanyika mwaka juzi kuonyesha mafanikio makubwa. Dihenga amezitaja kanda hizo nane ambazo zitashiriki mashindano hayo yanayomalizika Julai 6 kuwa ni Dar es Salaam, ambayo inajumuisha mikoa ya kimichezo ya Kinondoni, Ilala na Temeke.

  Kanda nyingine ni Kaskazini Magharibi zenye mikoa ya Arusha na Manyara, Kaskazini Mashariki (Kilimanjaro na Tanga), Kusini (Ruvuma, Lindi na Mtwara), Mashariki (Morogoro na Pwani, Ziwa (Kagera, Mwanza na Mara), Nyanda za Juu (Mbeya, Iringa na Rukwa) na Zanzibar ambayo itajumuisha mikoa ya Unguja na Pemba.

  “Kutokana na mafanikio ya mashindano hayo ya majaribio sasa wizara imeamua mashindano hayo katika ngazi mbalimbali yafanyike mwishoni mwa wiki na katika muda wa mapumziko marefu na mafupi ya mihula,” alibainisha Dihenga. Kwa mujibu wa muongozo wa wizara kila kanda inatakiwa kwenda Kibaha ikiwa na viongozi sita na wanamichezo 120 ambao watachuana katika michezo ya netiboli, mpira wa wavu, kikapu, meza, soka na riadha.

  “Tunatarajia mashindano hayo yatajumuisha watu takribani 1500 wakiwemo wadau wengine kutoka vyama mbalimbali vya michezo, waandishi wa habari na waamuzi. Aidha Dihenga alisema, mbali na kufikia uamuzi huo wizara pia imeiomba ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi kupitia Halmashauri za wilaya, miji na manispaa kupanga taratibu za kuendesha michuano ya shule za msingi kwa gharama nafuu pamoja na kutayarisha muongozo wa uendeshaji wa mashindano hayo.

  Kutokana na kurejeshwa kwa michuano hiyo mashuleni, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imeeleza kuwa gharama za uendeshaji za michuano hiyo katika shule za sekondari na vyuo vya ualimu itatoka kwenye sehemu ya ada watakazolipa wanafunzi na wanachuo. Pia Wizara imebainisha kuwa michuano ya ngazi ya taifa itakuwa ikigharimiwa na wizara pamoja na wadau mbalimbali kwa kutoa huduma muhimu katika kituo cha mashindano ambacho kitakuwa kimechaguliwa.

  Pamoja na hayo Wizara pia imetoa maelekezo kwa waandaaji wote wa michuano hiyo kutoa malazi yenye staha kwa wanafunzi wa jinsi zote, chakula chenye ubora unaokubalika, usalama wa uhakika pamoja na kutoa huduma za afya za kuridhisha pamoja na kuwa na viwanja na vifaa vitakavyotumika kwenye michuano hiyo vyenye viwango na ubora. Wanamichezo bora watakaopatikana kutokana na michuano hiyo ya Kibaha wataunda vikosi vya michezo mbalimbali vya Tanzania ambavyo vitakwenda kushiriki michuano ya Afrika Mashariki iliyopangwa kufanyika Agosti mwaka huu.
  Source: Gazeti la Habari Leo
   
Loading...