Masharti ya kozi za afya yatazamwe upya. | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Masharti ya kozi za afya yatazamwe upya.

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by BGG, Apr 8, 2012.

 1. B

  BGG Senior Member

  #1
  Apr 8, 2012
  Joined: Apr 5, 2012
  Messages: 136
  Likes Received: 6
  Trophy Points: 35
  Hivi karibuni, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeangaza vigezo na masharti mapya ya kujiunga na kozi mbalimbali za afya gazi ya cheti na stashahada. Kwa mujibu wa taarifa ya katibu mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupita tovuti yake, waombaji wa mafunzo ya afya kwa mwaka wa masomo 2012/2013· Ngazi ya cheti ni lazima ufaulu wao uwe wa kiwango kisichopungua (minimum) pointi 28 na alama ‘D’ (kidato cha nne) kwa masomo ya biologia, kemia na fizikia. Ufaulu wa kiingereza na hisabati ni kigezo cha ziada. · Ngazi ya stashahada : ufaulu wa ‘C’ mbili katika masomo ya biologia na kemia, na alama ‘D’ kwa somo la fizikia (kidato cha nne) au ufaulu wa alama ‘E’ (kidato cha sita) katika fizikia, biologia na kemia. Ufaulu wa kiingereza na hisabati ni kigezo cha ziada. Kwanza kabisa, tunapenda kuipongeza Wizara ya afya na ustawi wa jamii na hasa kitengo cha maendeleo ya rasilimali watu kwa sekta ya afya na wadau wote waliohusika kubadili vigezo vilivyokuwepo awali vya udahili. Ambavyo vilitoa nafasi kwa kozi za afya ngazi ya cheti na stashahada kwa wale tu, waliofaulu masomo yote ya msingi (kemia, biolojia na fizikia) katika kikao kimoja cha baraza la mitihani. Pia vigezo vya awali havikuzingatia masomo mengine ya ziada kama vile hisabati na kiingereza. Masharti(vigezo) vipya vya udahili tafsiri yake ni kwamba, wanafunzi waliofeli kidato cha nne somo la fizikia na wamefaulu biolojia, kemia na masomo ya ziada, hawawezi kupata fursa ya kusoma kozi za afya hata kama wamemaliza na kufaulu kidato cha sita katika michepuo ya kemia, biolojia na lishe (CBN), kemia, biolojia na jografia (CBG) au kemia, biologia na elimu (CB-Ed) wanakosa fursa ya kusoma kozi za afya kwa sababu tu wamekosa kigezo cha fizikia. Hata hivyo uamuzi huo wa wizara umepokewa kwa hisia tofauti na wadau mbalimbali wa sekta ya afya nchini kwa madai kuwa haukuzingatia mazingira na hali halisi ya vijijini na sekondari za kata.
  Mmoja wa walimu wa chuo cha maafisa tabibu cha Mtwara Clinical Officers Training Collage, Dr. Raphael Mwita anaona kuwa kuweka ulazima wa kufaulu somo la fizikia ni kupingana na malengo makuu ya mafunzo ya maafisa tabibu (Clinical officers).Dr. Mwita anayataja malengo ya mafunzo ya maafisa tabibu kuwa ni pamoja na kufanikisha mpango wa serikali wa kuboresha huduma za afya vijijini hivyo kuwa na ulazima wa kupata wanafunzi wanaotoka maeneo hayo ambao ni rahisi kurudi kutoa huduma katika maeneo yao. “Kuna uhaba mkubwa wa walimu wa somo la fizikia katika sekondari za kata hasa zile za vijijini. Kule shule nyingi hazina walimu wa fizikia, hivyo serikali ingeona busara ya kubakiza masomo ya msingi kuwa kemia na biolojia. Fizikia kubaki katika masomo ya ziada pamoja na hesabu, kiingereza na kiswahili kama ilivyo kwa wezentu wa jumuiya ya afrika mashariki (kenya na Uganda). Anasema kuwa ni rahisi kumpeleka mtu aliyezoea mazingira ya kijijini kufanya kazi huko kuliko waliozoea maisha ya mijini ambao wengi hulalamikia mazingira magumu na kuishia kuripoti tu na kurudi mijini.Naye Mkurugenzi wa shirika la Tandabui Health Access Tanzania (THAT)/Afya Radio
  ambaye pia ni daktari kitaaluma, Dr. Joseph Kavit anasema kuwa maamuzi ya wizara yanapaswa kuangaliwa upya ili kuwatendea haki watanzania.
  Dr. Kavit anatoa mfano wa mpango uliokuwa ukitumika zamani kwa waganga wasaidizi vijijini (RMA) ambao wengi wao walikuwa darasa la saba au kidato cha nne na hawakusoma masomo ya sayansi au kufaulu fizikia, lakini walipoendelezwa wakawa na ufanisi mkubwa katika kazi zao.“Wanganga hawa wa RMA wengi wao walijiendeleza hadi kufikia kuwa madaktari bingwa. Mifano ipo, hivyo tunaiomba serikali isipoteze fursa hizo bali iangalie uwezekano wa kupanua wigo ili kuwe na uwiano mzuri kati wataalamu wa sekta hiyo na wateja wanaopaswa kuwahudumia” Anasema Dr. Kavit. Pia aliongeza kwa kusema “ndio maana, hata jopo la wataalamu wa wizara ya afya, NACTE na wengine walipokaa kutengeneza mitaala ya kozi za utabibu ngazi ya cheti (NTA level 4: 2009 version) na ngazi ya stashahada (NTA Level 6: 2009 version) waliliona hili. Nakuweaka ufaulu wa msingi kuwa katika somo la biolojia na kigezo cha ziada kuwa somo la kiingereza”.
  Taarifa kutoka ndani ya wizara hiyo zinasema kuwa uamuzi huo umefikiwa kutokana na ufaulu wa wanafunzi kuwa mkubwa sana ukilinganisha na nafasi zilizopo katika vyuo vya afya na hivyo kukabiliana na changamoto hiyo kwa kuweka kigezo cha fizikia kama la lazima ili kuweza kujiunga na kozi za afya. Aidha, wananchi wanahoji ni kwavipi sharti hili liwepo kwetu na hasa katika kipindi ambacho Tanzania inashika nafasi ya mwisho kati ya nchi 52 za kiafrika kwa kuwa na uwiano wa madaktari wawili kwa wagonjwa 100,000 sawa na Malawi. “Serikali haikupaswa kuweka masharti yanayolenga kuwanyima wanafunzi fursa ya kujiunga na mafunzo ya afya kutokana na uhaba wa nafasi za vyuo , bali iweke utaratibu mzuri wa kuwadahili kupitia chaguo la kwanza, chaguo la pili na la tatu” Anasema Katongole Danstan mkazi wa Isamilo mjini Mwanza.Pia iendelee kuimarisha na kuendeleza kasi ya utekelezaji ya mkakati wake wakuongeza vyuo vya sekta ya afya vyenye ubora stahiki.
  Hata hivyo, utafiti uliofanywa na mwandishi wa makala haya umebaini kuwa vyuo vingi vya taasisi za kidini vinavyotoa mafunzo ya afya katika mikoa ya Kanda ya Ziwa vina idadi kubwa ya wanafunzi kutoka nchi jirani ya Kenya. Hivyo kupingana na hisia za wizara kuwa wanafunzi ni wengi kuliko uwezo wa vyuo vyake.

  Hivyo badala ya kuweka nguvu katika vigezo vya kupunguza idadi ya watanzania wanaopenda kujiunga na tasnia ya utabibu, ni bora mkazo huo ukawekwa katika kusimamia upanuzi, ujenzi na ubora wa vyuo vilivyopo ili kuweza kukidhi matakwa ya Mpango Mkakati wa Taifa wa Kuongeza Rasilimali Watu na Kuboresha viwango vya huduma katika Sekta ya Afya kama ulivyobuniwa mwaka 2008 na Mpango wa Maendeleo wa Afya Msingi (MMAM, 2007-2017).
  Mipango na mikakati hiyo mizuri ya serikali, inategemea kwa kiasi kikubwa utashi wa wizara husika ikishirikiana na NACTE ambayo kimsingi haipaswi kuwa kikwazo kwa kuweka masharti magumu yanayolenga kuongeza uhaba wa wataalamu hata wa kiwango cha stashahada na cheti badala yake kutakiwa kubuni njia mbadala ya kuwapa fursa wenye wito wa kuwahudumia watanzania wenzao pasipo kutanguliza maslahi binafsi.Pia, Wizara inapaswa kutambua kuwa taifa linapokuwa na uhaba wa watoa huduma za muhimu kama matibabu, huzaliwa tatizo la rushwa na kuzorota kwa huduma kwani unapokuwa na uwiano mkubwa wa wagonjwa wanaong'ang'ania kupewa huduma na mtaalamu mmoja, kanuni ya Uchumi ya ‘ugavi na mahitaji’ huchukuwa nafasi yake, ambapo mwenye pesa huweka dau ili apewe huduma kwa upendeleo. Mungu ibariki Tanzania!


   
 2. Nyakageni

  Nyakageni JF-Expert Member

  #2
  Apr 8, 2012
  Joined: Feb 1, 2011
  Messages: 13,946
  Likes Received: 1,272
  Trophy Points: 280
  duh! Inabidi Physics liwe somo la lazima! Wangeweka na mfumo wa kutoa diploma evening prog ningewaona wa maana
   
 3. v

  vngenge JF-Expert Member

  #3
  Apr 8, 2012
  Joined: Apr 19, 2011
  Messages: 366
  Likes Received: 34
  Trophy Points: 45
  Ndivyo walivyo huwa hawapendi kufikiri. Wao watafuta majibu ya stort cut kama yale ndio maana hata mitihani ya hesabu siku hizi ni ya kuchagua. Badala ya kutanua wigo wao wanaufinya. Sugueni vichwa ndo maana mmewekwa hapo tumewaani msitake kutushtua kuwa ndio mwisho wa uwezo wenu wa kufikiri ulipogota. Binafsi nilifikiri kuwa mmeona output ni hafifu kwa kiyo mmeamua kuongeza vigezo kumbe mmeshindwa namna ya kukabiliana na changamoto la ongezeko la wanafunzi!... Haya basi huko mmepata njia ya kudhibiti, tupeni basi na solution ya ongezeko la uhitaji wa huduma za afya kwa watanzania na takwimu ndo hizo tunaburuta mkia katika Afrika ina maana hata Ka Rwanda kametushinda. Uvivu wa kufikiri!!! ndo umetujaa tunachangamkia per di em tu na kutengeneza madili ya pesa kuboresha ufanisi na kukabiliana na changamotoa zerooooooooooo! kama haya ndo mawazo ya think tank la taifa basi tuna matatizo makubwa katika nchii hii kuliko hata tunavyofikiria.
   
Loading...