figganigga
JF-Expert Member
- Oct 17, 2010
- 25,658
- 55,487
WAENDESHA pikipiki maarufu kama bodaboda na baiskeli, kuanzia leo wamepigwa marufuku kusafirisha mazao ya misitu kama vile mkaa na mbao kwa kutumia vyombo hivyo, na watakaokiuka watachukuliwa hatua za kisheria.
Imebainika kuwa kutokana na kukithiri kwa usafirishaji wa mazao hayo kwa vyombo hivyo vya usafirishaji, serikali hupoteza jumla ya fedha za maduhuli zinazokadiriwa kufikia Sh bilioni 1.1 kwa mwezi ambayo ni sawa na Sh bilioni 13 kwa mwaka.
Mkakati huo wa kuwakamata watakaokiuka agizo hilo, unatekelezwa na mamlaka tatu ambazo ni Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama wa Barabarani, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
Na kwamba, atakayekamatwa na kubainika kuwa amesafirisha mazao hayo kwa kutumia vyombo hivyo vya usafiri atatozwa faini ya papo kwa hapo ya Sh 30,000, kifungo au vyote kwa pamoja.
Akizungumza Dar es Salaam , Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano TFS, Glory Mziray alisema Sheria na Kanuni za Sheria ya Misitu zinapiga marufuku mazao ya misitu kusafirishwa kwa kutumia pikipiki na baiskeli.
Aidha, alibainisha kuwa kwa mujibu wa Mwongozo wa Uvunaji Endelevu wa Mazao ya Misitu ya Asili wa Mwaka 2015, unaelekeza vyombo vya usafiri vinavyoruhusiwa kusafirisha mazao hayo kuwa ni vile vyenye magurudumu manne.
Alisema mwongozo huo ulizingatia pia sheria nyingine za nchi zikiwemo Sheria za Usalama wa Barabarani na Sumatra, lakini pia kubana mianya ya wizi na ukwepaji mkono wa sheria za usimamizi wa maliasili nchini.
“Kwa upande wa Sumatra kupitia Kanuni ya Leseni za Usafirishaji ya Mwaka 2010, inatambua pikipiki kama chombo cha kusafirisha abiria na si vinginevyo na Sheria ya Usalama Barabarani Sura Namba 168 iliyorejewa mwaka 2002 inatambua pikipiki na baiskeli kama chombo cha usafirishaji kwa ajili ya abiria na si mizigo,” alisisitiza.
Alieleza kuwa tathmini iliyofanyika mwishoni mwa mwaka jana na mwanzoni mwa mwaka huu, iligundua kuwa bodaboda na baiskeli zinachangia uvunaji haramu na usafirishaji wa haraka wa mazao ya misitu hususani mkaa kwa kiasi kikubwa nchini kote.
“Inakadiriwa kuwa bodaboda 20 zikisafirisha mkaa kwa mara moja huweza kusafirisha mzigo sawa na lori moja la tani saba lililojaa mkaa, hivyo kuizuia serikali kukusanya maduhuli…,” alisema Mziray.
Ofisa Leseni wa TFS, Ali Maggid, alisema pamoja na kwamba mazao ya misitu ni biashara halali kama ilivyo biashara nyingine, bado inahitaji udhibiti mkubwa ili kulinda hifadhi na mazingira ya misitu.
Aidha, alisema kwa mujibu wa tathmini iliyofanyika Novemba mwaka jana hadi Januari mwaka huu, katika barabara kuu za Bagamoyo, Kisarawe, Morogoro na Kilwa zinazoingia jijini Dar es Salaam, jumla ya bodaboda 582 zimebainika kubeba mazao hayo ya misitu kinyume cha sheria kila siku, hivyo kuikosesha serikali kiasi cha Sh bilioni 1.1 kwa mwezi.
Chanzo: Habari leo