esther mashiker
JF-Expert Member
- May 29, 2018
- 616
- 555
Dk. Leonard Chamuriho, ametaja, ununuzi wa ndege, maboresho ya viwanja vya ndege, ujenzi wa reli mpya ya kisasa na uboreshaji wa reli ya zamani, pamoja na mpango wa serikali kumiliki rada nne za kisasa ni vitu vya kujivunia kwa kila mtanzania ndani ya kipindi kifupi cha uongozi wa Rais Dk John Magufuli
Amesema vitu hivyo vinaweza kubaki katika kumbu kumbu ya muda mrefu ndani ya wizara yao kama mafanikio ya haraka yanayopaswa kuenziwa kwa gharama ya kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha vinaendelea kuwanufaisha watanzania kwa muda mrefu ujao
Akizungumzia upande wa uchukuzi wa anga alisema serikali ya awamu ya tano iliingia madarakani kukiwa na ndege moja,na kwa kipindi kifupi imeweza kununua ndege saba.
Alisema serikali imepanga kununua rada nne kubwa, huku moja moja kati ya hizo ikiwa imekwishanunuliwa hali itakayosaidia kuongeza usalama wa safari za anga na kuvutia ndege nyingi kupita katika anga la Tanzania.
Aliongeza kuwa vituo vya utabiri wa hali ya hewa vimeimarishwa na kufanya utabiri kuwa wa uhakika kwa asilimia 80.
Pia alisema serikali imenunua mtambo wa kuongozea ndege kwaajili ya Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume uliopo Zanzibar.
“Mtambo huu utawezesha ndege kutua katika hali yeyote ya hewa kwani rubani hatalazimika kuuona uwanja ndipo atue. Mtambo huu utakuwa wa tatu ukijumuisha na zile za Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere(JNIA) na Kilimanjaro (KIA),” alisema Dk. Chamuhiro.
Katika maboresho ya viwanja vya ndege Dk Chamuriho, alisema serikali imepiga hatua katika kupanua uwanja wa ndege wa Dodoma kwa kuongeza urefu wa njia ya kuruka na kuwezesha ndege kubwa kutua tofauti na ilivyokuwa awali.
Kuhusu uchukuzi upande wa reli alisema serikali ya awamu ya tano imeandika historia kwa kujenga reli yake ya kisasa (SGR) na kuanza ujenzi huo kwa kutumia fedha zake yenyewe.
Alisema hatua hiyo inaifanya Tanzania kuwa nchi ya pekee Afrika kwa kuwa na reli ya aina hiyo.
“Kuwa na reli yenye uwezo wa kutembea kwa spidi ya kilomita 120 kwa saa kwa upande wa mizigo na spidi 160 kwa saa kwa treni ya abiria ni mafanikio makubwa kwetu ni sisi tu tutakuwa wa kwanza kuwa na treni hii,” alisema
Alisema serikali pia imefanya vizuri kwa kuamua kufufua reli ya kati ya zamani ambayo imejengwa kwa kiwango cha Mita Gauge sambamba na ujenzi wa reli mpya.
“Tumepata fedha milioni 300 kutoka Benki ya Dunia kufanya ukarabati wa reli ya zamani na tayari mkandarasi yupo ‘site’ kwa kipande cha kutoka Dar es Salaam hadi Isaka kilomita 970 ukiondoa kipande cha Kilosa,”alisema.
Aliongeza kuwa ukarabati pia umeanza kipande cha Kaliua-Mpanda ambayo ni reli ya njia ya Tabora –Kigoma pamoja na ukarabati wa kipande korofi cha Kilosa.
Alisema shirika la reli Tanzania (TRC) limeanzisha mfumo wa kufuatilia mizigo ili kuongeza imani kwa wateja wa kusafirisha mizigo kwa njia ya reli.
Aliongeza kuwa pia mradi wa treni ya Dar es Salaam Commuter Train, upo katika hatua nzuri za upembuzi yakinifu.
Kwa upande wa uchukuzi wa majini alisema serikali imefanya mabadiliko makubwa kwa kuanza ujenzi wa meli mpya na kufufua meli zilizokuwa zimesimama kutoa huduma kutokana na kutofanyiwa ukarabati.
“Tulishuhudia hivi karibuni uzinduzi uliofanywa wa kujenga meli mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 1200 na tani 400 za mizigo pamoja na cherezo chenye urefu wa mita 100 chenye uwezo kubeba tani 4000, kitakacho tumika kwenye ujenzi wa meli mpya na ukarabati wa meli,” alisema Dk. Chamuriho.
Aliongeza kuwa ufufuaji wa meli unafanyika kwa kuanza ukarabati mkubwa wa MV Viktoria na MV Butiama ambazo kwa uda mrefu zimekuwa hazitoi huduma katika ziwa Viktoria.
Kwa upande wa bandari alisema serikali imefanya juhudi kubwa na tayari upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam umeanza na utahusisha ujenzi wa gati ya meli za magari na upanuzi wa gati namba moja hado saba.
Kazi za ujenzi, upanuzi na ukarabati huo zitafanyika katika gati namba 1 hadi gati namba 7 ambazo zinaendeshwa na zitahusisha kujenga gati hizo, kuongeza kina cha bahari kwa kuongeza urefu kutoka wastani wa mita 12 hadi kufikia mita 15.5 na kukarabati miundombinu wezeshi ya bandari.