Kipa huyo anakuwa mchezaji wa pili kuondoka Azam FC katika muda wa wiki moja na nusu baada ya aliyekuwa nahodha wake, Bocco, naye kusaini miaka miwili Simba wiki iliyopita huku kiraka Shomari Kapombe akitarajiwa kumwaga wino Msimbazi hapo dakika yoyote sasa.
Azam ipo katika mipango ya kubana matumizi na imegoma kutoka fedha za usajili kwa wachezaji wake wanaomaliza mikataba. Taarifa kutoka Chamazi zinasema huenda wachezaji muhimu zaidi ya saba wakaondoka katika usajili wa sasa kutokana na mpango huo.
Simba imempata Manula wakati ambao anashikilia rekodi ya kuwa kipa pekee aliyeweza kushinda tuzo ya Kipa Bora wa Ligi Kuu Bara na kisha kuitetea. Kipa huyo aliyeibuliwa na Azam amekubali mkataba wa Sh50 milioni kujiunga na Simba na kuitosa Singida United iliyokuwa imempatia ofa ya Sh60 milioni.
Licha ya kwamba viongozi wa Simba wanafanya siri, lakini Mwanaspoti bila shaka yoyote linafahamu kwamba Manula atavaa jezi nyekundu na nyeupe msimu ujao huku kipa Mghana, Daniel Agyei, akiwa katika harakati za kutemwa.
Sababu kubwa za Manula kuacha fedha ndefu ya Singida na kutua Simba imetajwa kuwa ni timu hiyo kushiriki mashindano ya kimataifa mwakani pamoja na mapenzi yake ya kuendelea kusalia jijini Dar es Salaam kufanya shughuli zake nyingine. Simba itacheza Kombe la Shirikisho.
Manula amekuwa katika kiwango cha juu katika kipindi cha miaka minne sasa ambapo mbali na kushinda tuzo ya Kipa Bora wa Ligi Kuu mara mbili (2016 na 2017), alikuwa kipa namba mbili Kombe la Kagame mwaka 2015.
Pale Azam, Manula amekuwa kipa namba moja miaka mitatu mfululuzo.
Chanzo: Mwanaspoti