Bilionea Asigwa
JF-Expert Member
- Sep 21, 2011
- 16,515
- 28,487
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Philip Mangula, amekosoa kauli ya Msemaji wa chama hicho, Christopher ole Sendeka ya kupambana na vyama vya upinzani kwenye majukwaa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika Tamasha la Kigoda cha Mwalimu Nyerere lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema siasa ina wakati na mahali pake.
“Hata msemaji wetu alikosea kusema CCM ingeenda kupambana nao huko huko barabarani. Hatuwezi kufanya kitu kama hicho kwa sababu haijengi badala yake inabomoa, wakati huu ni wakati wa kujenga nchi.
“Siasa ina muda na wakati wake…tulifanya siasa za majukwaani wakati wa kampeni na uchaguzi na ule ulikua wakati wake lakini hivi sasa kuna Bunge ambalo linajadili suala muhimu la bajeti ya Serikali halafu mtu badala ya kukaa bungeni atoe mchango wa kujenga na kuboresha anataka kwenda kusimama kwenye majukwaa, suala ambalo halitasaidia kitu,” alisema Mangula.
Hivi karibuni, Sendeka alizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam akilaani operesheni okoa demokrasia iliyoanzishwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Akizungumzia kuhusu uongozi wa Mwalimu Nyerere na ule wa sasa, alisema tatizo linalosumbua ni watu kununua uongozi huku wapiga kura wakiomba kununuliwa.
Alisema CCM imekuwa ikijitahidi kupambana na tatizo hilo kwa kuwaondoa wale wanaobainika kununua uongozi.
“Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 katika majimbo manne tuliwaondoa wagombea wa ubunge waliokuwa wameshinda nafasi ya kwanza na ya pili na kuteua walioshika nafasi ya tatu kwa sababu ya rushwa.
“Pia katika majimbo 10 tuliteua wagombea walioshika nafasi ya pili na kuwaacha waliokuwa wameshinda baada ya kubaini kuwapo vitendo vya rushwa,” alisema.
Alisema watu wasiojua nini kinachoendelea wamekuwa wakilalamika kuwa chama hicho hakina demokrasia suala ambalo si kweli.
Chanzo: Mtanzania