Manesi waongeza makali ya mgomo | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Manesi waongeza makali ya mgomo

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by MziziMkavu, Jan 29, 2012.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Jan 29, 2012
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,607
  Likes Received: 4,599
  Trophy Points: 280
  Waipa serikali siku tatu kutekeleza madai ya madaktari
  [​IMG] Wasema kama haikufanya hivyo wataungana nao
  [​IMG] Tucta yataka kima cha chini Sh. 500,000 kwa mwezi  [​IMG]
  Mgonjwa aliyevunjika nyonga, Anna Mwandosya, akisaidiwa na watoto wake, Issaya Amon (kushoto) na Robert Amon, kutoka kwenye kiti maalum kumpandisha kwenye gari nje ya Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) jijini Dar es Salaam baada ya kukosa huduma hospitalini hapo ili kurejea nyumbani kwao.


  Mgomo wa madaktari umezidi kupamba moto na sasa Chama cha Wauguzi Tanzania (Tanna) tawi la Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kimeipa serikali siku tatu kikitaka itekeleze madai ya madaktari, vinginevyo wataungana nao katika mgomo.
  Tamko hilo lilitolewa na Tanna kupitia Mwenyekiti wake, Paul Magesa, baada ya kufanya kikao chake jana. Alisema ni vyema serikali ikakubali kukaa katika meza ya mazungumzo na madaktari, ili kumaliza mgogoro huo badala ya kuendelea kuvutana, huku wagonjwa wakiendelea kufa.
  Kutokana na hilo, walimuomba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kutumia busara na kuwafuata pale wanapokusanyikia ili akazungumze nao na kufikia mwafaka.
  “Tunamuomba Waziri Mkuu azungumze na madaktari, atumie busara yake tu, awafuate pale wanapokusanyikia ili kuokoa maisha ya Watanzania yanayopotea hivi sasa,” alisema Magesa.
  Aliongeza: “Tunasema hatuwezi kufanya kazi peke yetu bila madaktari. Sisi ni kama mafiga matatu. Tunategemeana. Figa moja likikosekana hakuna kinachoweza kufanyika.” Alisema hadi sasa wanafanya kazi katika mazingira magumu, hususan pale wanapokumbana na wagonjwa wanaohitaji huduma ya haraka kutoka kwa daktari.
  “Kwa kuwa muuguzi ni mtumishi wa karibu sana na mgonjwa kuliko watumishi wengine wa afya, sisi ndio tunaona wanavyoteseka. Hali hii inatuumiza kisaikolojia na kimwili pia, wauguzi tunaonekana wabaya na tayari tumeshaanza kutukanwa na wagonjwa na ndugu zao kwamba wanakosa huduma,” alisema.
  Alisema hali ya huduma imezidi kuzorota na kwamba, itafika wakati hawatamudu majukumu yao japokuwa walisema hawapendi ifikie hatua hiyo.
  Walimuomba Rais Jakaya Kikwete, kufanya mabadiliko ya uongozi katika Wizara ya Afya kwa kumteua Katibu Mkuu mwingine, ambaye atakuwa mtaalamu wa mambo ya afya.
  Pia wameiomba wizara kutatua madai mbalimbali ya wauguzi ikiwa ni pamoja na kuunda kurugenzi ya uuguzi ifikapo Julai, mwaka huu na kupewa fedha za sare sio kushonewa sare hizo kama ilivyo sasa.

  MGOMO WA MADAKTARI WAENDELEA
  Wakati huo huo, madaktari katika Jiji la Dar es Salaam, jana waliendelea na msimamo wao kugoma na kusababisha huduma katika Hospitali za Amana na Muhimbili kusuasua.
  NIPASHE ilitembelea katika Hospitali ya Muhimbili na kujionea hali ya huduma ikiwa mbaya katika wodi ya Mwaisela na Kibasila.
  Hata hivyo, Afisa Uhusiano wa Muhimbili, Aminiel Algaesha, alithibitisha huduma katika hospitali kutokuwa nzuri.
  “Huduma si ya kuridhisha kwa sababu wagonjwa wanapata shida sana kutokana na huu mgomo wa madaktari. Kliniki nyingi hazifanyi kazi,” alisema Algaesha.
  Kadhalika, katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (Moi), hali ilikuwa hivyo hivyo, ambako huduma iliyokuwa ikitolewa ni ile ya dharura pekee.

  HOSPITALI YA KCMC
  Katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, jana mgomo wa madaktari uliingia siku ya tatu baada ya madaktari hao kuendelea kukaa nje ya hospitali na majumbani, wakisubiri Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, atekeleze kauli yake ya kuonana na kamati inayoratibu na kufuatilia maslahi yao jijini Dar es Salaam kwa vitendo.
  NIPASHE ilifika hospitalini hapo jana majira ya asubuhi na kushuhudia misururu mirefu ya wagonjwa, huku baadhi ya madakatari wakiendelea kutoa huduma kwa muundo wa mgomo baridi na madaktari bingwa wakiendelea na huduma kama kawaida.
  Hata hivyo, wakati wengine wakiendelea kugoma, hospitali hiyo ilisema imejipanga kikamilifu baada ya kupata barua kutoka kwa madaktari waliogoma, ambao wameeleza bayana kuwa hawana ugomvi na hospitali wala Shirika la Msamaria Mwema, bali serikali.
  Wakizungumza katika kusanyiko la madaktari hao nje ya jengo la hospitali hiyo, walisema mgomo huo ni endelevu na watatoa huduma kwa wajawazito, ambao wanahitaji huduma ya daktari na wagonjwa mahututi wanaopokelewa katika kitengo cha mapokezi na waliopo kwenye vyumba vya wagonjwa mahututi (ICU).
  Walisema wanasikitishwa na kauli ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda kusema kuwa mishahara ya madaktari hao ni sawa na watumishi wengine.
  Walisema anatoa kauli hiyo bila kuwa na taarifa kamili kutoka utumishi wa umma.
  “Kwa sasa hili suala lilipofika si la waziri au viongozi wengine wa wizara kuliingilia kati maana kabla ya kufika hapa tulishapeleka hoja zetu na hawakutaka kuchukua hatua, kwa sasa tunategemea atatusikiliza na kutupa majibu stahili ni Waziri Mkuu, ambaye hatuwezi kumfuata ofisini kwani anajua madaktari walipo,”alisema.
  Katika kundi hilo la madaktari, kulionekana kuna mgawanyiko kutokana na hofu miongoni mwao kupoteza kazi kutokana na kwamba, wapo madaktari, ambao ni waajiriwa wa Shirika la Msamaria Mwema na walioajiriwa na serikali na ambao wameshamaliza masomo na wapo katika mafunzo ya vitendo (Intern).
  Wakizungumza na NIPASHE, Anna Nkya, ambaye alimleta baba yake kwa ajili ya upasuaji, alisema alikuja jana na kuambiwa hakuna huduma na alirudi na mgonjwa wake nyumbani ambaye hali yake ni mbaya na alimrudisha kwa ajili ya upasuaji ingawa tarehe aliyopangiwa ya Februari 10, mwaka huu, haijafika.
  Alisema amefika eneo la mapokezi tangu saa 12 asubuhi, lakini hajapata huduma na aliambiwa kuwa madaktari wapo kwenye mgomo, hivyo hawezi kusaidiwa, na kwamba anashindwa la kufanya maana mgonjwa hali yake si nzuri.
  Naye, John Mongi alisema ni vyema serikali ikawasikiliza madaktari hao na kukutana nao katika meza ya majadiliano kuliko kuwapuuza, huku wananchi wakiendelea kupoteza maisha, ikiwa ni pamoja na kuwaongezea mishahara kama walivyofanya kwa wabunge kwani hali ngumu ya maisha haipo kwa wabunge pekee bali hata kwa watumishi wengine.
  Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, Dk. Moshi Ntabaye, alithibitisha kuwapo kwa mgomo huo baada ya kupokea barua ya madaktari hao. madaktari hao wanaogoma ni 105, watatu wakiwa ni madaktari bingwa, 63 kati ya 81 waliopo kwenye mafunzo ya vitendo, 30 kati ya 123 wanaosoma shahada ya uzamili na watatu waliosajiliwa.
  Alisema kuna madaktari 75, ambao wapo kazini na kwamba, baada ya kupata barua ya madaktari hao rasmi walifanya kikao na viongozi wa hospitali hiyo na kujipanga kikamilifu katika kutoa huduma na kuhakikisha huduma hazizoroti.
  “Tunachowasihi ni kama kile alichokisema Waziri Mponda kuwa warudi kazini, tumejipanga kutoa huduma bila kuwa na upungufu wowote kwani si kila mwaka hospitali inakuwa na madaktari wa mazoezi wengi kama wa mwaka huu na huduma hazijawahi kusimama...licha ya mgomo, lakini nimepita kwenye wodi na kuwakuta hata wale walio kwenye mgomo wanaendelea na kazi kama kawaida,” alisema.
  Katika barua yao ya Januari 27, mwaka huu, kwenda kwa uongozi wa hospitali hiyo, madaktari hao walidai kuwa wanaunga mkono mgomo wa wenzao nchini.
  Walisema mgomo huo hauna kikomo na umelenga kuishinikiza serikali kutekeleza madai yao yote na kuongeza kuwa wataendelea kuona wagonjwa wa dharura katika idara mbalimbali hospitalini kwa kipindi chote cha mgomo.

  HOSPITALI YA AMANA HALI MBAYA
  Akizungumzia mgomo huo, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Amana, Dk. Meshack Shimwela, alisema hali ni mbaya hospitalini hapo tangu mgomo huo ulipoanza mapema wiki hii.
  Dk. Shimwela alisema mgomo huo umeiathiri hospitali na wananchi kwa jumla na kwamba, hivi sasa wamesitisha huduma ya wagonjwa wa nje.
  “Tunapokea wagonjwa, ambao wako serious kabisa, kwa jumla Hospitali ya Amana hali ni mbaya,” alisema.
  Alisema mgomo huo umekuwapo tangu ulipotangazwa na kwamba, nia ni kutetea maslahi ya madaktari na wananchi kwa jumla kwa kuwa pamoja na mambo mengine nia ya mgomo ni kutaka serikali iboreshe mazingira ya kazi.

  HOSPITALI TEULE TUMBI
  Madaktari katika hospitali ya Teule ya Tumbi mjini Kibaha, mkoa wa Pwani, jana waliendelea na kazi kama kawaida, pamoja na kuendela kwa migomo katika baadhi ya hospitali hapa nchini.
  NIPASHE ilitembelea hospitali hiyo jana na kujionea madaktari na wauguzi wakiendelea na shughuli zao za kutoa huduma kwa wagonjwa licha ya mgomo uliotangazwa na madaktari nchi nzima kuishinikiza serikali kusikiliza madai yao.
  Kaimu Mganga Mkuu wa Hosiptali hiyo, Dk. Sylvester Mkama, alisema hawajaona umuhimu wa kufanya mgomo, kwani masuala yao megi huyamaliza ofisini kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Elimu Kibaha na kupatiwa ufumbuzi.
  “Sisi hatukutaarifiwa kuhusu mgomo, lakini hata tungearifiwa tusingegoma. Hatuna haja ya kugoma. Mwajiri wetu ni Shirika la Elimu Kibaha. Hivyo, kama shirika la umma tunapokuwa na matatizo tunayawasilisha kwa mkurugenzi na yeye uyafanyia kazi kwa kadiri ya taratibu za kazi zilizopo,Alisema Dokta Mkama.
  Naye Mkurugenzi wa Shirika hilo, Cyprian Mpemba, alisema siri ya kutokuwapo kwa mgomo hospitalini hapo ni pamoja na aina ya utendaji wake wa kazi, ambapo amekuwa daima akikutana na wafanyakazi wa idara mbalimbali kutaka kujua matatizo yao na mambo mengine, ambayo ni kikwazo katika utendaji wao wa kazi.
  “Nimekuwa na utaratibu wa kukutana na wafanyakazi kufuatana na idara zao. Na hata sasa hivi naelekea kikaoni kukutana na watenadaji. Na madaktari nilikutana nao wiki iliyopita na tukaelezana mambo mbalimbali yahusuyo idara yao. Hivyo, kwa utaratibu huo sidhani kama wafanyakazi wanaweza kugoma,” alisema.

  WIZARA YA AFYA YANENA
  Afisa Mawasiliano wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris Mwamaja, alisema bado wanaendelea kupokea mrejesho kutoka katika hospitali ili waweze kutolea taarifa madhara yaliyotokea kutokana na mgomo huo wa madaktari.
  Alisema bado wanaendelea na tathimini yao kwani kuna hospitali zinasemwa zinafanya mgomo wakati sio kweli ila wakikamilisha wataandaa ripoti.
  Waziri wa Afya Dk. Hadji Mponda na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Blandina Nyoni, walipotafutwa na NIPASHE jana kuzungumzia suala la mgomo huo, walieleza kuwa bado wapo kwenye kikao kilichokuwa kikijadili suala hilo.
  Hadi gazeti hili linaingia mitamboni, viongozi hao walikuwa wakiendelea na kikao hicho.

  TUCTA YAIBUA MADAI MAPYA
  Nalo Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi Nchini (Tucta), limekumbusha machungu yaliyoanza kusahaulika miongoni mwa wafanyakazi, baada ya kutangaza kuwa mwaka huu limejiandaa kuendesha vuguvugu kabambe kudai kima cha chini cha mshahara kiwe Sh. 500,000 badala ya Sh. 350,000 walichokuwa wakikidai mwaka juzi.
  Akizungumza katika mkutano wa kuchagua viongozi wa Tucta Mkoa wa Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Nicolaus Mgaya, alisema mwaka huu hawatakuwa na mchezo katika kudai kima cha chini cha mshahara kipandishwe kwa wafanyakazi.
  Hata hivyo, Mgaya alisema Tucta bado inafanya mazungumzo na serikali ili kuhakikisha wafanyakazi wanalipwa mshahara mzuri kwa kuwa ghrama za maisha zimepanda
  Aidha, sambamba na hilo Tucta imeitaka serikali kupunguza kodi katika mishahara ya wafanyakazi hadi kufikia ya asilimia 10 kwani hilo nalo ni tatizo linalowasumbua watumishi.
  “Kodi iwe chini ya asilimia 10 kwani hivi ipo juu na hilo tumekuwa tukilizungumza na serikali lakini naona bado hawajatuelewa,”alisema
  Alisema serikali inang’ang’ania kutoza kodi kubwa katika mishahara wakati wafanyabiashara, ambao wanapata faida kubwa wanakwepa kulipa kodi ya mapato.
  “Vita ya kuibana serikali ipunguze kodi vitakuwa endelevu katika mwaka huu ili kuhakikisha wafanyakazi wanapata unafuu wa maisha,” alisema Mgaya. Katika mkutano huo, wajumbe kutoka vyama mbalimbali vya wafanyakazi walichagua viongozi wao, ambao ni mwenyekiti wa Tucta Mkoa wa Dar es Salaam, Mratibu wa Mkoa pamoja na mwakilishi wa wanawake.

  Imeandaliwa na Elizabeth Zaya, Leonce Zimbandu, Beatrice Shayo, Richard Makore (Dar); Salome Kitomari (Moshi), Margareth Malisa (Kibaha)  CHANZO: NIPASHE
   
 2. Sabung'ori

  Sabung'ori JF-Expert Member

  #2
  Jan 29, 2012
  Joined: Jul 19, 2011
  Messages: 2,087
  Likes Received: 149
  Trophy Points: 160
  ...hivi kumbe Tucta(mbayuwayei) wapo?!...
   
 3. nitonye

  nitonye JF-Expert Member

  #3
  Jan 29, 2012
  Joined: Dec 18, 2011
  Messages: 7,167
  Likes Received: 507
  Trophy Points: 280
  Huyo mgaya hana lolote alishanunuliwa zamani
   
 4. Ndebile

  Ndebile JF-Expert Member

  #4
  Jan 29, 2012
  Joined: Sep 14, 2011
  Messages: 3,630
  Likes Received: 1,990
  Trophy Points: 280
  TUCTA pumb@<u zenu! TALGWU nyie ni majambazi tu kama TBS...nyote pamoja ni wachumia tumbo!
   
 5. Dr.Chichi

  Dr.Chichi JF-Expert Member

  #5
  Jan 29, 2012
  Joined: Apr 30, 2008
  Messages: 2,336
  Likes Received: 52
  Trophy Points: 145
  tucta wazushi
   
 6. Babkey

  Babkey JF-Expert Member

  #6
  Jan 29, 2012
  Joined: Dec 10, 2010
  Messages: 4,256
  Likes Received: 2,078
  Trophy Points: 280
  ...tucta=TUTA
   
 7. Nsiande

  Nsiande JF-Expert Member

  #7
  Jan 29, 2012
  Joined: Jul 27, 2009
  Messages: 1,649
  Likes Received: 11
  Trophy Points: 135
  Manesi wakiunga tela Hali itakuwa mbaya kuliko.......na Hao TUGHE sijui TUCTA wanahitaji mabadiliko ya uongozi
   
Loading...