Mambo ya siasa | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mambo ya siasa

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by Jumakidogo, Oct 2, 2010.

 1. Jumakidogo

  Jumakidogo R I P

  #1
  Oct 2, 2010
  Joined: Jul 16, 2009
  Messages: 1,859
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 0
  kuelekea uchaguzi mkuu,ubaguzi wa rangi,udini na ukabila vipigwe vita


  Na JUMA KIDOGO


  Kwanza kabla ya yote nitakuwa mchache wa fadhila kama sinta mshukuru Mungu ambaye ameniwezesha leo hii kuwa hai tena huku nikiendelea kuvuta hewa na pumzi hii ambayo amenipa bure. Baada ya kupotea kwa kitambo kirefu katika ulimwengu huu wa makala kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu. Sasa nimerudi tena ugani, nimerudi nikiwa na afya njema kabisa.


  Nimerudi wakati muafaka, huu ni wakati ambao ile ligi maarufu ya kuwania madaraka imeanza rasmi, ligi ambayo itadumu kwa kipindi cha miezi miwili kisha bingwa rasmi atapatikana. Bingwa ambaye atadumu na kombe kwa miaka mingine mitano npaka ligi nyingine mpya itakapofanyika. Kabla sijaendelea mbele, naomba niwatoe hofu wasomaji na watanzania kwa ujumla kwa kuwaambia kuwa wasiwe na wasiwasi. Mimi ni mtanzania halali wa kuzaliwa kwa upande wa baba na mama.


  Mimi siyo Msomali wala Mrundi, mimi ni Mnyamwezi halisi, tena kutoka Urambo, kule Magharibi mwa mkoa wa Tabora. Tena ni mtukuu wa yule Mtemi maarufu wa Wanyamwezi aliyekuwa akiishi hukohuko Urambo.


  Ndugu watanzania wenzangu,parapanda limelia na kampeni kuelekea uchaguzi mkuu sasa zimeanza rasmi, huu ni wakati wa mambo mengi kutokea, vijembe, dharau, chuki na masimango kutoka kwa mgombea huyu hadi mgombea yule, wa chama hiki na chama kile, huu ndiyo wakati wake sasa. Huu ni wakati wa “mchaka mchaka chinja,halimselema halija”.


  Wakati mchaka mchaka na mbio za kuelekea uchaguzi mkuu zimeanza, mambo mengi sana yatajitokeza, ukiachilia mbali yale ambayo tumeyashuhudia katika chaguzi mbali mbali ndani ya vyama vya siasa. Hasa macho ya wengi yalikuwa yameelekezwa katika kura za maoni zilizokuwa zikiendeshwa na chama tawala, yaani “CCM” chama cha mapinduzi, siku kadhaa zilizopita.


  Kabla sijaingia katika mantiki na maudhui ya makala yangu haya. Nami napenda kuwa miongoni mwa watanzania mbali mbali waliotoa na wanaoendelea kutoa pongezi zao kwa zoezi lile la kura za maoni. Uchaguzi ambao kwa mara ya kwanza tulishuhudia hofu ya vizito ya kutetea nafasi zao huku wengine wakitumia mbinu chafu za kuwanunua wanachama ili wawapigie kura. Uchaguzi huo wa aina yake umetufumbua macho kwa kiasi kikubwa sisi wananchi mbumbumbu mzungu wa reli kuwa utaratibu uliokuwa ukitumiwa kuchagua viongozi kwa kura za maoni katika chaguzi zilizopita ulikuwa siyo wa kidemokrasia na ulikuwa ukiwanyima haki ya msingi raia waliokuwa na hamu ya kugombea uongozi katika nafasi za Ubunge na Udiwani katika majimbo na kata zao.


  Kura za maoni katika uchaguzi wa mwaka huu zimewaacha uchi wakongwe wengi wa siasa katika chama hicho hali inayofanya tuamini kuwa nyakati zile walikuwa wakitumia mbinu chafu kuhakikisha wanabaki madarakani na kuendelea na utawala wao mbovu usiokuwa na maslahi kwa wananchi wa majimbo yao na taifa kwa ujumla. Baada ya kudokeza hayo machache sasa nianze kurudi na kupenya taratibu kwenye mlango wa kuingilia kule nilikokuwa nimedhamilea kuingia. Nimedhamilia kuingia katika ukumbi uliohifadhi mambo makuu matatu khususan katika kipindi hiki cha npito kuelekea uchaguzi mkuu.Mambo hayo ni tofauti ya rangi kati ya raia na raia, udini na ukabila miongoni mwa watanzania.
  Haya ni mambo ambayo wakiachwa baadhi ya watu waendelee kuyashabikia na kuyabebea bango la kuyapigia Debe yanaweza kuchafua na kutingisha nguzo imara na misingi bora ya amani iliyoachwa na viongozi wetu waliokuwepo huko mwanzo.


  Hakuna asiyefahamu kuwa tangu enzi ya uhuru taifa letu limekuwa na raia wa rangi mbalimbali, limekuwa na makabila tofauti zaidi ya 120, limekuwa na raia wenye dini na imani tofauti tofauti waliopewa haki na uhuru wa kuabudu kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Raia wote wa nchi hii wanapewa haki sawa ya kugombea nafasi za uongozi bila kuangalia tofauti ya rangi zao.


  Hakuna asiyefahamu kuwa raia wenye rangi nyeusi ni wengi zaidi kuliko wale wa rangi nyingine, lakini katika masuala ya uongozi na utawala hatuangalii rangi ya mtu, tunachopaswa kutizama hapa ni uwezo wa utendaji kazi wa mtu mwenyewe bila kujali rangi na dini yake pia.


  Mimi siyo shabiki sana wa siasa, wala si mwanachama wa chama chochote. Yatosha tu kusema kuwa mimi ni shabiki wa maendeleo ya nchi yangu. Ni shabiki wa kiongozi yeyote anayepigana kuleta maendeleo ya nchi yangu, ni shabiki wa viongiozi wa aina hiyo bila kujali tofauti zao za rangi, udini, na ukabila kwa ujumla. mtashangaa, mtashangaa kwa kuwa nasisitiza sana swala la tofauti za rangi, nasisitiza kwa sababu hapo ndipo waliposimamia sana wachafuzi wasiopenda maendeleo ya nchi yetu. Wale wanaochukia raia wenzao wenye rangi tofauti na zao. Wanasiasa hawa uchwara hawakuwepo enzi zile kabla mfumo huu wa vyama vingi haujaanza. Tangu kuanza kwa mfumo huu aina hiyo ya wanasiasa ikaanza kuibuka taratibu na sera zao za ubaguzi wa rangi.


  Uhuru wa kuwa na vyama vingi katika nchi isichukuliwe kama kigezo cha kuleta ubaguzi wa rangi miongoni mwa raia. Huo ni ujinga, umbumbumbu na upotofu wa fikra sahihi, wenzetu hawa waachwe wapewe madaraka, wapewe uongozi katika majimbo wanayogombea, wapigiwe kura. Wafanye kazi ya kuwaletea maendeleo wananchi katika majimbo yao na taifa kwa ujumla. Miongoni mwa wanaowapiga vita raia hawa weupe ni wasomi, wasomi ambao pengine wangetumia usomi wao kupevuka kisiasa na kujali maendeleo ya nchi yao. Na wala si kutumia usomi wao kupinga uwepo wa watu weupe katika nafasi mbalimbali za uongozi.


  Siasa ni njia mojawapo ya kufika katika tabaka la utawala na kushika nyadhifa mbalimbali katika nchi. Lakini uongozi ni kipaji kutoka kwa Mungu. Unaweza kuchagua kuingia katika siasa kwa ajili ya kujipatia maslahi lakini usiwe na kipaji cha uongozi na utawala. Hapo utakuwa umewanyima raia haki yao ya kutawaliwa na kiongozi bora wa kuwaongoza katika misingi imara. Aina hii ya wanasiasa wapo sana katika vyama vya upinzani. Wananchi wa nchi hii sasa wanafahamu na kuelewa vema ulimwengu unavyokwenda mbele.


  Ni zaidi ya Muongo mmoja sasa vyama hivyo vipo, vipo na viongozi walewale tangu vilipoanzishwa. Lakini ukipima maendeleo ya ndani kwa ndani ya vyama hivyo matokeo yake utapata sifuri. Hakuna chama cha upinzani chenye uwezo wa kumiliki hata bustani ya Nyanya au Mchicha katika kipindi chote hicho cha uhai wao, je ikiwa chama kina umri wa zaidi ya miaka kumi lakini hakina hata jembe la kulimia nyasi zinazoota kuzunguuka katika ofisi zake, kitawaleteaje maendeleo wananchi?


  Binafsi nilitegemea kuwa ndani ya miaka kumi vyama hivi vingekuwa chachu na chachandu ya kuwahimiza wananchi shughuli za maendeleo huko vijijini ili wapiga kura waelewe kuwa kumbe hawa nao wapo.Ingekuwa simulizi ya kuvutia iwapo kama katika kipindi chote hicho tungeshudia Helkopta ya CHADEMA ikinyunyuzia dawa kwenye mashamba ya Serena na tegemeo ili kudhibiti ndege aina ya kwelea kwelea huko Singida, lazima huu sasa ungekuwa wakati muafaka kwa wakulima hao kulipa fadhila kwa kuwapiga kura.


  Tungeshuhudia Helkopta hiyo ikitimua vumbi na kufanya mbwembwe huko Kongwa vijijini kuwatimua Bundi wanaokula na kuharibu karanga za wakulima. Lazima huu ndiyo ungekuwa wakati wao wakulima hao wa kulipa fadhila kwa kuwapigia kura,haina maana kulitumia dege hilo lenye makelele mengi wakati wa kuomba kura tu,uchaguzi ukipita nalo linatoweka.Watanzania si wajinga,wanatambua hilo. Tungeshuhudia pia viongozi wa CUF Lipumba na wenzake wakisaidiana na wakulima kupandikiza mpunga huko Kintinku katika bonde la ufa. Lazima wananchi hao huu ndiyo ungekuwa wakati wao wa kulipa fadhila kwa kuwapa kura viongozi hao. Lakini wanavisikia vyama hivyo na viongozi wao kupitia vyombo vya habari, Redio na Magazeti, labda na bendera zao chache ambazo ni chafu na zilizochakaa. Je hakuna hata wanachama wa vyama hivyo wenye uwezo wa kuchangia hata mbegu za mbogamboga za majani wakapewa wananchi ili walime, wavune, wale wawe na afya bora?
  Katika majimbo yote yanayogombewa na watanznia halali, lakini wenye asili ya kiasia, wananchi wapime uwezo wao kuongoza na wawapigie kura kadri ya uwezo wao ili wawaletee maendeleo katika majimbo yao.Tatizo hili la rangi ni watoto pacha na lile la udini. Yaani rangi ni kulwa, dini ni dotto. Raia wengi huhukumiwa kutokana na tofauti ya rangi na dini pia. Japo dini sintaizungumzia katika makala haya, lakini ipo mgongoni mwa pacha wake “rangi” yaani kulwa. Swala hili la rangi nakumbuka lilijitokeza pia bungeni siku za nyuma.


  Nakumbuka wakati ule wa sakata la RICHMOND, baada ya kukaa na kutafakari kwa kina nikatambua kuwa kuna baadhi ya raia pale bungeni wanachimbwa kutokana na rangi, pia makabila yao. Mh Rostam aliingia katika mkumbo na kusakamwa sana katika wakati ule kutokana na tatizo la rangi, rangi ilikuwa kitanzai kilichokuwa kimeandaliwa kuinasa shingo ya kisiasa ya mtanzania huyo na kumtupa umbali mkubwa nje ya ulingo wa siasa. Lakini kwa kutambua umuhimu wake katika jimbo analoliongoza, wananchi wake wamempa kura na sasa anaendelea kuwa mgombea katika jimbo hilo kwa mara nyingine.


  Huo ni mfano mmoja mdogo katika mchezo mchafu huo wa siasa. Ukiachilia mbali rangi na udini, pia kuna ukabila wa chini kwa chini, ukabila ambao kama mizizi yake itaachwa ikomae karibu na ukuta huu wa amani ipo siku itasababisha nyufa na kufanya ukuta huo ubomoke na kusambaratika vibaya . Tatizo hili lipo, tena lipo katika vyama vyote vya siasa pamoja na chama tawala. Nchi hii imejengwa katika misingi ya umoja na kuifutilia mbali ile dhana ya ukabila. Ndiyo maana watanzania wamechanganyika pote katika nchi yao na si rahisi kujua Wanyamwezi wapo wangapi, Wasukuma wapo wangapi, Wachaga wapo wangapi nk.


  Dhana hii potofu ya ukabila ilianza kujitokeza wazi wazi miongoni mwa watanzania wachache wakati ule Mh Edward Lowasa alipoteuliwa kuwa Waziri mkuu, baadhi ya watu wakaanza kusikika chini kwa chini wakihoji na kulalamika kwa kusema “mbona asilimia kubwa ya Mawaziri wakuu wanatokea mikoa ya kaskazini mwa Tanzania?” Huo ni ujinga, ujinga usiofaa kabisa kuwepo ndani ya kichwa cha mtanzania wa leo. Watanzania wote ni wamoja.Kwa mfano hata kama Spika wa bunge mnyamwezi mugu akamjalia uhai na akakalia kiti hicho kwa miaka mia, ahukumiwe kutokana na uadilifu na utendaji kazi wake ulio bora. Au ahukumiwe pia kutokana na utendaji wake wa kazi usio ridhisha, ahukumiwe kwa haki na wala siyo kigezo cha ukabila.


  Katika lile sakata la RICHMOND Mh Lowasa chanzo cha hukumu yake ilikuwa ni chembechembe za ukabila. Kutokana na fikra potofu za watu wachache waliokuwa wakiamini kuwa Rais alikosea, alikosea kumteua Waziri mkuu kutoka mikoa ya kaskazini.RICHMOND ilikuwa ni sawa na manyasi yaliyounganishwa kati kati ya kinjia hivyo mhe Lowasa alipokuwa akipita katika kinjia hicho akajikwaa na kudondoka kwa bahati mbaya.Lakini hakuumia na ndiyo maana wananchi katika jimbo lake bado wanamuhitaji na wamedhamiria kumrudisha tena bungeni.


  Dhambi ya watu hao haitafutika kwenye orodha ya wenye dhambi katika kitabu cha Mungu. Pia dhambi za watu wanaomkosoa Mungu kwa uumbaji wake wa kuumba watu wa rangi tofauti na kuleta ubaguzi kati yao. Kama ni Waislamu au Wakristo ama Wapagani ghadhabu za Mungu zitawashukia na kuwaangamiza wao pamoja na fikra zao potofu. Watazikwa, watazikwa na kupotelea kwenye makaburi yao yenye kimya na giza la milele.


  mwandishi wa makala haya ni mtunzi wa riwaya pia na simulizi za kusisimua katika magazeti mbalimbali anapatikana kwa 0764-561078, 0712-140720 jumakidogo@yahoo.com kidogo2009.peperonity.com
   
Loading...