Mambo kumi (10) muhimu ya kufanya ili mwaka 2016 uwe bora sana kwako

Makirita Amani

JF-Expert Member
Jun 6, 2012
1,915
3,407
Habari rafiki yangu?

Najua mwanzo huu wa mwaka umeshaambiwa na kujiambia mambo mengi sana ya kufanya. Najua wewe mwenyewe umeshajiahidi vitu vingi sana, ambavyo huenda usiweze kufanya hata nusu yake.

Na mimi tena nakuja na mambo mengine kumi!

Kwa nini ufuatilie mambo haya mengine kumi wakati umeshaweka yako na wengine wameshakuambia mengine mengi zaidi?

Nakusihi uzingatie haya kumi kwa sababu moja kubwa, kwa sababu NAJUA UNAPENDA KUWA NA MAISHA BORA. Najua popote ulipo sasa ungependa kuwa na maisha bora zaidi ya hapo ulipo. Ungependa kufurahia zaidi maisha yako na pia ungependa kuwa muhimu kwa wengine pia.

Uzuri ni kwamba yote hayo yanaanza na wewe mwenyewe, yaani ni maamuzi yako mwenyewe ndiyo yanakuletea maisha bora na ya mafanikio na utakayoyafurahia.

Na ndio sababu nakuletea mambo haya kumi, ambayo kama ukianza kuyafanya, nina hakika maisha yako hayatabaki hapo yalipo. Kwa sababu mimi nayafanya haya na maisha yangu yanazidi kuwa bora kila siku.

Kama upo tayari kwa mambo haya kumi, karibu ujifunze na uchukue hatua mara moja;

1. Soma vitabu vingi zaidi ya ulivyosoma mwaka 2015.

Mafanikio ni zao la maarifa na maarifa yanapatikana kwa kusoma. Na sio kusoma tu, bali kusoma vitabu na makala zenye mafunzo ya kukupatia wewe maarifa unayoweza kutumia kufanikiwa.

Mwaka huu 2016 soma vitabu zaidi ya ulivyosoma mwaka jana. Kama mwaka jana ulisoma kitabu kimoja, mwaka huu soma viwili, kama ulisoma vitatu mwaka huu soma vitano. Na kama hukusoma kabisa anza kusoma sasa. Ongeza maarifa zaidi na tumia yale unayojifunza, hutajutia hilo.

Kama huna kitabu cha kusoma, ijumaa ya wiki hii nitatuma kitabu kizuri sana kwa mwaka 2016 kwa wale waliojiunga na AMKA MTANZANIA na wanapokea email. Kama bado hujajiunga bonyeza hapa na ujaze taarifa zako. Kama umeshajiunga angalia email yako na utaona makala za AMKA MTANZANIA. Kama unatumia gmail angalia kwenye updates, promotions na spam utaziona email.

2. Punguza nusu ya muda unaotumia kuangalia tv.

Iwe unapenda kuangalia tamthilia, kufuatilia michezo au kuangalia habari. Kadiri unavyotumia muda mwingi mbele ya tv ndivyo unavyojichelewesha kufikia mafanikio unayotaka.

Hakuna kitu kikubwa utakachoweza kupoteza kwa kupunguza muda unaoangalia tv. Anza kwa kupunguza nusu, chagua vipindi vile ambavyo ni muhimu sana na vina msaada kwako. Vingine achana navyo. Hapo utaokoa muda mwingi zaidi ambao utaweza kuutumia kwenye mambo mengine muhimu kwako.

3. Punguza nusu ya muda unaotumia kwenye mitandao ya kijamii.

Mitandao ya kijamii ina faida zake, ila hasara kwa sasa zimekuwa kubwa kuliko faida. Imekuwa inanyonya muda wa wengi na hata kuwasababishia wengine msongo. Kama upo facebook, twitter, instagram, na kwingineko, na kila baada ya muda unaingia kuangalia ni nini kinaendelea, utabaki nyuma sana. Anza sasa kutenga muda maalumu na mfupi sana kwa siku kuangalia mitandao hii, isizidi saa moja ndani ya masaa 24 na kwa mitandao yote. Na utakapopunguza muda huo hakuna kikubwa utakachokosa, na badala yake utapata muda mwingi wa kufanya yale ambayo ni muhimu zaidi kwako.

4. Nunua uhuru wako kutoka kwenye simu yako.

Changamoto ya karne hii zimebadilika sana. Moja wa maadui wetu wakubwa ni simu zetu za mkononi, maarufu kama smartphones. Kwa bahati mbaya sana simu hizi zimekuwa na akili kutuzidi. Wacha nikuulize swali, unaweza kukaa dakika ngapi bila ya kuangalia simu yako? wengi wetu macho yamegandishiwa kwenye simu hizi. Kila baada ya dakika tano unaibonyeza.

Sasa mwaka huu nunua uhuru wako kutoka kwenye simu yako. kwanza ondoa kabisa kelele za simu hii namaanisha notifications, halafu mara nyingi zima mtandao. Na hakikisha unaweza kukaa muda bila ya kuangalia simu yako. simu isikulazimishe wewe uache unachofanya ili kuiangalia, bali jipangie muda maalumu wa kuangalia simu yako.

5. Endelea kujilipa wewe kwanza.

Nasema endelea kujilipa wewe kwanza kwa sababu najua umeshaanza kujilipa. Na kama hujaanza kujilipa au huelewi nazungumzia nini hapa, fungua makala hii usome; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutajirika Kwa Kuanza Na Shilingi Elfu Moja.

Na kama ulianza halafu ukaishia njiani, ni wakati wa kuendelea kujilipa, ni muhimu sana kwako kuzingatia hilo.

6. Fanya.

Kama kuna kitu chochote unataka kwenye maisha yako, kifanyie kazi. Acha kupiga kelele kwamba unataka kufanya hiki au unataka kufanya kile. Wewe anza kufanya. Kama ni biashara anza, kama ni kuboresha kazi yako anza.

7. Kuwa makini na afya yako.

Hii ndio rasilimali muhimu sana kwako. Ukiwa kwenye kitanda cha hospitali, hakuna chochote kati ya hivi tumejadili hapa kitakuwa muhimu kwako. Afya ni muhimu, ipe kipaumbele namba moja.

8. Endelea kusema hapana.

Hapa pia nasema endelea kwa sababu najua umeshaanza, kama bado hujaanza kusema hapana unapoteza. Na mwaka huu 2016 utapoteza zaidi. Soma makala hii kujua jinsi ya kusema hapana; Mambo 30 Ya Kusema HAPANA Mwaka Huu 2015…

9. Timiza unachoahidi.

Hii ni silaha itakayokusaidia sana kwenye ulimwengu wa sasa ambapo mambo yanakwenda kwa kasi sana, muda umekuwa adimu na kuna mengi ya kufanya. Kwenye kazi yako au biashara yako, hakikisha unatimiza kile unachoahidi, hata kama ni kidogo kiasi gani. Dunia ya sasa imebadilika sana, uaminifu una mchango mkubwa sana kwenye mafanikio yako, jenga uaminifu kwa wengine na ulinde sana.

10. Jiunge na KISIMA CHA MAARIFA.

Kama mpaka sasa hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA unakosa mengi. Ndani ya kisima unapata makala nzuri za mafanikio kwenye kazi, biashara, uchambuzi wa vitabu na pia unapata nafasi ya kuwa kwenye kundi la wasap. Ndani ya kundi hilo kuna kila sababu ya wewe kuwa chanya kila siku na kubadili kabisa maisha yako. na yote hayo unayapata kwa gharama ya tsh elfu 50 tu ambayo ni ada ya mwaka. Kama ungependa kujiunga nitumie ujumbe wasap kwenye namba 0717396253.

Nakutakia kila la kheri kwa mwaka huu 2016, ukawe mwaka wa mafanikio makubwa sana kwako kwa sababu wewe mwenyewe umechagua mafanikio.

Nakuahidi tutaendelea kuwa pamoja, na tegemea makubwa sana kutoka AMKA CONSULTANTS.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani.

makirita@kisimachamaarifa.co.tz
 
thanks mkuu. Nimejifunza.

Nitaingia kwenye hizo mada uloweka. Ubarikiwe na kheri ya mwaka mpya
 
Back
Top Bottom