Mama Mgwira na nguvu ya mwanamke

Mama Mgwira na nguvu ya mwanamke

mkude kibwana

JF-Expert Member
Joined
Oct 9, 2014
Posts
348
Reaction score
27
Gazeti la Jambo Leo limeandika makala haya kuhusu Mama Anna Mghwira
Mghwira achambua nguvu na maarifa ya mwanamke kiuchumi
Na Celina Mathew
Mwanamke na mwanaume kila mmoja ana nguvu yake ya asili katika kukabiliana na hali ya kiuchumi. Hili ni eneo ambalo siyo kila mtu anaweza kulichambua.


Mgombea Urais wa Chama cha ACT-Wazalendo, Anna Elisha Mghwira anaweza kuchambua kuhusu nguvu ya uchumi wa mwanamke na jinsi ambavyo wanaume wakiwaamini wanawake, jamii inaweza kupata matokeo mazuri.
Mghwira ni mwanasheria aliyetunukiwa shahada yake Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, lakini pia ni msomi wa Theolojia katika Chuo Kikuu cha Makumira, Arusha.


Kwenye Theolojia, Mgwhira pia ni msomi wa ngazi ya shahada. Na ndani ya Theolojia kuna elimu za Saikolojia, Sosholojia, Dini na Lugha za Kigiriki, Kihebrania na Kikatoliki.
Kwa mantiki hiyo, Mghwira ni mwanasaikolojia kutokana na elimu yake ya Theolojia aliyopata Makumira, vilevile mwana jamii (Sosholojia).


NINI NGUVU YA UCHUMI WA MWANAMKE?
Jumatatu ya wiki hii, nilikutana na Mama Mghwira kisha nikapata fursa ya kufanya naye mahojiano kuhusiana na masuala mbalimbali ya nchi, siasa zake kipindi hiki tunapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu 2015.


Katika mambo tuliyojadiliana, tulizungumza kuhusu kitu kinachoitwa nguvu ya mwanamke kiuchumi. Mama Mghwira anasema kuwa ifike wakati jamii iwaamini wanawake kwa sababu wana uwezo mkubwa wa kujenga uchumi imara kwenye nyakati ngumu.


“Kuna kitu lazima watu wakijue, mwanamke na mwanamume kila mmoja ana nguvu yake, ni vizuri jinsia moja ikaiheshimu nyingine,” anasema Mghwira.
Anaongeza: “Mwanamke ni kiungo muhimu kiuchumi hususan pale mambo yanapokuwa magumu. Mwanaume hufanya mambo yake vizuri pale ambapo hali inapokuwa nzuri.”


ANAFAFANUA HOJA HIYO
Mghwira: “Hili litazamwe sana hata kwenye ngazi ya kifamilia, mambo yanapokuwa mazuri ndani ya nyumba, baba anakuwa na nguvu kubwa sana ya kuendesha uchumi wa familia. Atatoka na kurudi bila kuchoka.


“Hali ikiyumba tu, mama huamka na kuushika uchumi wa nyumba. Yaani kipindi ambacho baba hurudi nyuma na kujikunyata kwamba hali ni mbaya, ndipo mama huamka na kujishughulisha kwa hili na lile ili familia iende mbele.


“Ni kipindi ambacho utaona mama anasomesha watoto, analisha familia. Yaani nyakati ngumu baba huwa hajiwezi. Nyakati ngumu mama huchomoza. Mama hababaishwi na kukosekana kwa fedha kama inavyokuwa kwa baba.”


Mama Mghwira anasema kuwa kutokana na ukweli huo kwamba mwanamke huwa na nguvu kubwa kiuchumi kipindi mambo yanapokuwa magumu, ni vizuri watu wakawapa kipaumbele.
“Watu waijue hiyo nguvu ya mwanamke na waiheshimu. Hili suala halipo tu kwenye familia, hata katika taasisi nyingi ikiwemo za kisiasa, kama wanawake wakipewa kipaumbele kwenye uamuzi matokeo yatakuwa mazuri kabisa.


“Kufeli kwa taasisi nyingi ni kwa sababu wanaosimamia maendeleo na ambao ndiyo mikono ya kiuchumi ni wanaume. Utakuta kipindi fedha zinapokuwepo mipango mingi itatekelezwa lakini ugumu wa kifedha unapoingia ni hapo shughuli husimama na wakati mwingine mpaka taasisi yenyewe hufa,” anasema Mghwira.


Anaendelea kufafanua: “Kama taasisi itayumba, mwanamke anapopewa kipaumbele, yeye anaweza kufanya kazi zikaendelea kwa sababu ni asili ya mwanamke kukabili vipindi vigumu vya kiuchumi na ni kawaida kwa mwanaume kufubazwa na hali ngumu.”


Anashauri kuwa wanaume na wanawake washirikiane ndani ya familia, kwenye taasisi za kikazi na hata serikalini kwa maelezo kuwa hiyo ndiyo dawa ya kumudu vipindi vyote vya kiuchumi.
“Nguvu ya mwanaume nimeisema kadhalika na ya mwanamke. Kwa hiyo, kama kutakuwa na ushirikiano kwenye vipindi vyote mambo yatakuwa mazuri sana,” anasema.


NINI MAONI YAKE KWA JUMLA?
“Watu wawachague wagombea wanawake wenye uwezo. Binafsi naweza kwa sababu ninazo sifa nyingi kuliko wenzangu wengine katika ngazi ya urais. Nikichaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nitaweza kuisaidia nchi kiuchumi kwenye nyakati rahisi na ngumu. Mwanamke wa kweli hadumazwi na ugumu wa hali.


“Vilevile chama changu, ACT-Wazalendo, kimesimamisha wagombea wengi wanawake wenye uwezo. Katika majimbo 202 tuliyosimamisha wagombea ubunge, asilimia 25 ni wanawake. Wapigakura wawape kura hao wanawake ili waoneshe nguvu ya mwanamke kiuchumi na nina uhakika watawavusha.


“Ukiniuliza kingine, nitakwambia tu kuwa ACT-Wazalendo ina wagombea ubunge wengi wenye sifa nyingi. Kama wataaminiwa na kuingia bungeni, kwa hakika Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 2015-2020, litakuwa bora mno kuwahi kutokea kwenye historia ya nchi yetu,” anasema Mghwira.
 
Back
Top Bottom