Makundi yatishia kampeni za CCM Arumeru | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Makundi yatishia kampeni za CCM Arumeru

Discussion in 'Chaguzi Ndogo' started by MziziMkavu, Mar 10, 2012.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Mar 10, 2012
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,616
  Trophy Points: 280
  [​IMG]
  Rais mstaafu Benjamin Mkapa​

  MKAPA ATOA SHARTI KUMALIZWA TOFAUTI NDANI YA CHAMA KABLA HAJAZINDUA KAMPENI
  Mussa Juma na Peter Saramba, Arumeru
  RAIS Mstaafu wa awamu wa tatu, Benjamin Mkapa ambaye anatarajiwa kuzindua kampeni za Chama cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki, anadaiwa kutoa sharti la kumalizwa kwanza kwa tofauti za kimakundi ndani ya chama hicho, kabla ya yeye kufanya uzinduzi wa kampeni za uchaguzi huo.

  Mkapa alipendekezwa na Kamati Kuu ya Halmashauri kuu (CC) ya CCM kuzindua kampeni hizo, katika kikao chake cha Machi mosi ambacho pia kilifanya uteuzi wa mwisho wa mgombea ubunge wa jimbo hilo ambaye ni Siyoi Sumari baada ya kufanyika duru ya pili ya kura za maoni kati ya mgombea huyo na aliyekuwa mpinzani wake, William Sarakikya.

  Awali ratiba ilikuwa ikionyesha kwamba CCM ilipaswa kuzindua kampeni zake leo lakini, ghafla ratiba hiyo ikabadilishwa na sasa uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika, Jumatatu Machi 12.

  Habari za uhakika kutoka ndani ya chama hicho zilisema mabadiliko ya ratiba ya uzinduzi wa kampeni za CCM, yanatokana na sharti la Mkapa ambaye ametaka kwanza makundi ambayo yalitofautiana kutokana na kura za maoni yakutanishwe ili kuondoa tofauti zao.

  Mpasuko huo katika kura za maoni jimboni Arumeru Mashariki ni zao la msuguano wa makundi ya urais ndani ya CCM kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015 ambayo kila moja lilitaka kumweka mgombea wake.

  Mmoja wa makada wa CCM kutoka mkoani hapa, aliliambia Mwananchi kwamba, “Nadhani ni uamuzi mzuri tu wa Mkapa kutaka kwanza makundi yakutanishwe. ”

  Hata hivyo, Mkuu wa Kitengo cha Uchaguzi wa CCM Makao makuu, Matson Chizi, licha ya kukiri kampeni za CCM zitazinduliwa Machi 12 lakini, hakuwa tayari jana kueleza kama Rais mstaafu Mkapa atahudhuria au la.

  Chizi alisema, "Tutazindua kampeni zetu Machi 12 ila kuhusu Rais mstaafu kuja au la bado tunatazama ratiba yake."

  Chizzi pia alizungumzia tuhuma kwamba wapo watu wanaonunua shahada za kupigia kura na kusema kuwa chama hicho kinapinga utaratibu huo, bila kujali anayenunua ni wa chama gani.

  Chizzi alisema kununua shahada ni kutaka kupora haki ya mtu kupiga kura hivyo tayari wametoa taarifa kwa msimamizi wa uchaguzi na polisi kushughulikia suala hilo.

  Mkuu huyo wa Kitengo cha uchaguzi akizungumzia makundi yaliyotokana na kura za maoni, alisema kwa sasa yamekwisha na wanaccm wote wameungana kukihakikisha chama hicho ushindi.

  “Wakati wa kura za maoni ni lazima yawepo makundi lakini baada ya kuteuliwa mgombea mmoja makundi yote yamekufa na kubaki kundi moja la CCM kutwaa jimbo”alisema Chizzi.

  Mapema wiki hii, Meneja wa Kampeni wa CCM, Mwigulu Nchemba ambaye pia ni Katibu wa Uchumi na Fedha wa CCM, alisema chama hicho kinajipanga kukutanisha waliokuwa wagombea wa kura za maoni na wapambe wao.

  “Tuna mpango wa kuwakutanisha hawa wagombea na wapambe wao ili tuweze kuendelea vizuri na kampeni zetu,” alisema Nchemba.

  Meneja huyo, ambaye yuko jijini Arusha kwa takriban wiki moja sasa, amekuwa pia akikutana na mabalozi na viongozi wa chama hicho katika jimbo la Arumeru Mashariki.

  Hata hivyo, jana meneja huyo, licha ya kupigiwa simu yake ya mkononi mara kadhaa hakupokea kuelezea ratiba ya uzinduzi wa kampeni na ujio ya mwenyekiti huyo Mstaafu wa CCM, Mkapa.

  Nape anena
  Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye kwa upande wake alipoulizwa jana alibeza taarifa hizo akiziita kuwa za udaku na mitaani.

  Nape alisema ni vema watu wakawa makini na taarifa za upotoshaji zinazotolewa na baadhi ya wapotoshaji.

  "Sasa ninyi andikeni mzee Mkapa kagoma kwenda kuzindua kampeni halafu kesho mnamuona yuko jukwaani sijui mtasemaje," alisisitiza Nape.

  Alipoulizwa kwamba Mkapa ametoa ushauri wa kumalizwa kwanza tofauti za makundi, alijibu, "Acheni habari za udaku. Ninyi kwani mnaandika udaku?," alihoji.

  Nape alifafanua kwamba hakuna kitu kama hicho akimaanisha kwamba Mkapa kagoma kwenda kuzindua kampeni na kusisitiza, "huo ni udaku."

  Aliongeza, "Tatizo lenu mnapoletewa taarifa ambazo mwisho wa siku hubainika ni za uongo, huwa hamuwarudii na kuwauliza vipi tena?," alisisitiza.


  Ratiba ya upinzani
  Upande wa Chadema mwenyekiti wake, Freeman Mbowe akiwa ameambatana na viongozi wa juu ya chama hicho, wanatarajia kuzindua kampeni za chama hicho kesho Jumamosi katika eneo la Usa river.

  Akizungumza na Mwananchi jana Mkurugenzi wa Bunge wa Chadema, John Mrema alisema kabla ya uzinduzi mwenyekiti huyo anatarajiwa kupokewa kwa maandamano makubwa.

  “Tutazindua kampeni za mgombea wetu Jumamosi na atazindua mwenyekiti na taratibu zote zimekamilika,”alisema Mrema.

  Mwenyekiti wa chama cha TLP, Agustine Mrema pia anatarajiwa kutua katika jimbo hilo, hivi karibuni kuongoza kampeni za mgombea wake, Abraham Chipaka.

  Katibu wa TLP mkoa wa Arusha, Mwamvua Wahanza alisema jana kuwa wakati wowote Mrema atatua katika jimbo hilo ili kuongoza kampeni za chama hicho.

  Nacho chama cha Sauti ya Umma (SAU), kampeni zake zitazinduliwa Machi 12 katika eneo la Kikatiti na Katibu mwenezi wa chama hicho Taifa, Johnson Mwangosa.

  Mgombea ubunge wa jimbo hilo, Shaban Moyo Kirita ambaye pia ni mjumbe wa CC ya SAU, alisema taratibu zote za uzinduzi zimekamilika na kuongeza, "Sisi tutaendesha kampeni za kisasa kabisa Arumeru na tunauhakika wa ushindi.”

  Uchaguzi huo mdogo wa jimbo la Arumeru Mashariki, utafanyika April mosi kufuatilia kifo cha aliyekuwa mbunge, Jeremiah Sumari.


  Wagombea warejesha fomu
  Wagombea wote wanane wa ubunge katika jimbo hilo la Arumeru Mashariki jana walirejesha fomu za kuwania kuchaguliwa, hukua wafuasi wa Chadema wakijitokeza kwa wingi zaidi wakiwa katika pikipiki na magari kumsindikiza mgombea wao Joshua Nasari.

  Wafuasi hao wa Chadema walifunga barabara Kuu ya Moshi- Arusha katika eneo la Usa River na Liganga, wakati wakimsindiza mgombea huyo.

  Nassari aliyekuwa juu ya gari la wazi, alikuwa amesindikizwa na meneja kampeni, Vicenti Nyerere mbunge wa jimbo la Musoma, baadhi ya wabunge wa Chadema na wakurugenzi wa idara mbali mbali za chama hicho.

  Umati huo mkubwa wa watu, ulisababisha msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo hilo Trasias Kagenzi mara kutoka nje kuwaambia wafuasi hao kwamba alikwishapokea fomu za Nassari ili wafuasi hao watawanyike.

  "Jamani nimetoka kuwaeleza kuwa tayari tumepokea fomu za mgombea wetu, tunazifanyia kazi na leo (jana) saa 10 tutabandika ubaoni majina ya wagombea wote muyaone,"alisema Kagenzi.

  Msimamizi huyo alisema kampeni za uchaguzi huo, zinaanza kesho na akawaondoa hofu wanachama wa Chadema kuhusiana na kutotendewa haki katika uchaguzi huo.

  "Mimi ni msimamizi wa uchaguzi huu hivyo ondoweni hofu kuwa haki haitatendeka, tena kama ningepewa nafasi ya kuchagua kusimamia uchaguzi huu au la ningesema mimi hapana lakini kwa kuwa mimi ni mtumishi wa Serikali nitafanya kazi hii kwa uadilifu,"alisema Kagenzi na kushangiliwa na wanachadema.


  Kagenzi alisema majina ya wagombea hao yatabandikwa kwenye mbao za matangazo hadi leo ili kama kuna pingamizi liwekwe.

  Hata hivyo, hadi jana jioni hakuna mgombea yoyote aliyekuwa amewekewa pingamizi ili isishiriki katika uchaguzi huo mdogo.

  Msimamizi huyo alisema kikao cha viongozi wa vyama vyote vya siasa kilitarajiwa kufanyika jana jioni kupanga ratiba ya kampeni za uchaguzi huo.

  "Ratiba ya kampeni tutaitoa kesho (leo) baada ya vyama vyote kukubaliana ili kufanya uchaguzi wetu uwe wa haki na amani,"alisema Kagenzi.

  Mara baada ya Msimamizi kutoa tamko hilo, wafuasi hao wa Chadema pamoja na mgombea wao, waliondoka kwa maandamano hadi katika ofisi za uratibu wa uchaguzi wa chama hicho zilizopo Usa River.

  Katika hali ambayo haikutarajiwa, upande wa CCM ambao walichukuwa fomu kwa mbwembwe jana mgombea wao Siyoi alirudisha fomu katika ofisi ya halmashauri ya Meru huku kukiwa na idadi ndogo ya watu, wakiwepo viongozi wa CCM na wanafamilia, ambao waliongozwa na Chizzi.

  Akizungumzia hali hiyo, Chizzi alisema kusindikizwa na watu wachache mgombea wao kurejesha fomu ni ‘staili’ tu waliamua kuifanya tofauti na mwanzo walipofika kuchukuwa fomu.


  Katibu CUF agombea NRA
  Katika hatua nyingine, mpasuko ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) umezidi kuendelea baada ya katibu wa chama hicho wilaya ya Arumeru, Hamis Juma Kieni kujiengua katika chama hicho na kujiunga na NRA na jana, alirejesha fomu ya kugombea.

  Akizungumza na Mwananchi, Kieni alisema ameamua kujiondoa CUF na kujiunga na NRA baada ya kuona chama hicho, kinatangaza kutosimamisha mgombea bila kuwasiliana na uongozi wa wilaya.

  chanzo. Makundi yatishia kampeni za CCM Arumeru

  "Mimi nilikuwa nimeweka nia ya kugombea ubunge ila ghafla chama changu kikatangaza kutosimamisha mgombea, nikaona chama sasa kinapoteza mwelekeo kwanini hawakuwasiliana na sisi na hivyo nikajivua uanachama,"alisema Kieni.

  Wagombea wa vyama vingine vya Upinzani ambao jana walirejesha fomu ni pamoja na Shabani Moyo Kirita SAU, Chipaka wa TLP, Charles Msuya wa UPDP na Mohamed Abdalah Mohamed wa DP.
   
Loading...