Makosa ya hayati Mwl Nyerere, Rais Magufuli naye anaweza kuyafanya

Mlanje

Senior Member
May 16, 2013
141
77
Ndugu watanzania wenzangu nimependa kuandika mambo haya ya msingi kwa mstakabali wa nchi yetu.

Hayati Mwl Nyerere aliwahi kusema kwa kinywa chake mwenyewe kuwa nanukuu "Katika Urais wangu nimefanya mambo mengi mengine ya kijinga kabisa na mengine mazuri tu,ubaya wenu yaliyo mazuri hamyafanyi ila mnafanya ya kijinga" mwisho wa kunukuu.

Hapa ndipo Mwl Nyerere alidhihirisha ubinadamu wake kwa kukiri kuwa na mapungufu na pia alionyesha dira ya uongozi kwa Taifa letu kuwa tusifuate yote aliyofanya kama ndio msahafu wa kuendesha Taifa letu.Na hii ndio inamfanya Mwl kukumbukwa na kila mwanasiasa hapa kwetu Tanzania,na niseme wazi mimi Mwl Nyerere ndio kiongozi wangu wa kuigwa(My Role Model).Nikuombe radhi msomaji wangu maana nitaandika kwa kirefu kidogo mada hii.

Leo ukimwambia mtu nitajie mambo matatu ya kijinga aliyofanya Mwl Nyerere kwanza utaonekana unamtukana Mwalimu na huenda ukaishia kwenye matatizo makubwa lakini zaidi sana swali lako halitajibiwa.Leo niandike mambo matano tu ya kijinga aliyofanya Mwl Nyerere kama yeye alivyosema kwenye hotuba yake niliyonukuu hapo juu,pia huenda msomaji maneno haya yanaleta ukakakasi lakini ndivyo alivyoyatamka Mwalimu mwenyewe kwenye hotuba yake na nataka kufikisha ujumbe kama ulivyo.

1.Jambo La kwanza
Kufuta vyama vingi vya siasa mwaka 1963 hii ilifanyika kwa lengo la kuleta umoja kwa Taifa changa lililokuwa limepata uhuru miaka miwili tu iliyopita, hivyo aliona si vyema tukawa tunakosoana.Sababu hii ilikuwa na mapungufu makubwa mojawapo iliminya uhuru wa watu kuikosoa serikali na waliodhubutu walipoteza nyadhifa zao mfano akina Kasanga Tumbo wa Tabora alikuwa balozi wa Tanzania nchini Uingereza alijiuzulu nafasi hiyo na kuanzisha chama chake cha siasa lakini kwa kuzuia kukosolewa Mwl Nyerere alivifuta vyama vingi.Akina Aboud Jumbe(Rais wa Zanzibar) alikosoa muundo wa Muungano kilichomkuta alipoteza Urais wake na uenyekiti wa baraza la mapinduzi kule Zanzibar,Oscar Kambona alikosoa mfumo wa ujamaa na kujitegemea.na wengine wengi ambao walidiriki kumkosoa Mwl Nyerere waliishia kuondolewa kwenye nyazifa zao.

Hii ilipelekea Mwl Nyerere kushiriki kwenye uchaguzi peke yake na watu walichagua kati ya kivuli na yeye.Kosa hili Mwl Nyerere alilirekebisha mwaka 1992 ingawa chama chake cha CCM kilikataa kuanzishwa kwa vyama vingi ila yeye kwa kutumia nguvu yake alisisitiza vianzishwe na vikaanzishwa.Madhara yake tulianza upya kana kwamba ni utaratibu mpya nchini.Katika kosa hili hata serikali iliyopo madarakani inaelekea kulifanya kwa kuvinyima nafasi vyama vingine kufanya siasa hii inaungwa mkono na Tamko la Waziri mkuu Cassim Majaliwa la kusema viongozi wa vyama vingine walioshindwa wasiruhusiwe kufanya mikutano ya kisiasa.Hapa serikali inasahau kuwa kuna wananchi takribani milioni 6 walivipigia kura vyama hivi na kufanya Rais aliyepo madarakani kupata asilimia 58% ya kura zote,kwa kuminya uhuru huu inadumaza ukuaji wa vyama vingi vya siasa na demokrasia ambao ni mfumo tuliokubali kuwa nao kwenye katiba na inajikosesha ushirikiano kutoka kwa wananchi hao hivyo kutofikia malengo yake mengi kwa kukosa kuungwa mkono na wananchi wote.

2.Jambo la pili
Kutoliingiza azimio la Arusha kwenye Katiba ya nchi
Kama kuna kitabu Mwl Nyerere alikipenda na hata kutembea nacho ni azimio la Arusha.hii ilitokana na ubora wake kwa kubeba misingi ya utu.Lakini azimio hili halikulindwa kwa kuliweka kwenye katiba na huenda ni kutokana na Mwl kuamini kuwa wana CCM wote walilipenda na wasingeliacha.Lakini cha kushangaza alipoingia madarakani Rais Ally Hassana Mwinyi aliliacha kwa azimiao la Zanzibar lililokinzana na lile la Arusha kwa kuruhusu mambo mengi yaliyokuwa yamekatazwa na Azimio la Arusha na hapa ndio ikaja kauli ya kila kitu ruksa.Lakini azimio hili lingekuwa kwenye katiba isingekuwa rahisi kulibadili.Kosa hili la Mwl Nyerere Mzee Joseph Sinde Warioba anaonekana kutaka kulirekebisha kwa kusema miiko ya uongozi iingie kwenye katiba mpya ingawa amepingwa vikali na chama chake.Changamoto ya serikali ya awamu ya tano ni jee itakubaliana na mapendekezo ya tume ya Mzee Warioba au itaendelea na katiba pendekezwa?Hii wengi wanasubiria kujua hatma ya katiba mpya.

3.Jambo la tatu Kutaifisha na Africanization
Hapa Mwl Nyerere kwa nia njema kabisa alitaifisha mashirika yaliyokuwa ya kikoloni na hata Taasisi kwa kuamini kuwa zikiwa serikalini zitafanya vizuri na pia aliamini baadhi ya mashirika hayo yalipatikana kwa kumnyonya Mtanganyika.Hii ilipelekea wazungu wengi waliokuwa nchini kufukuzwa kazi zao kama ukuu wa shule kwenye shule za kikoloni kama Tabora School(Tabora boys) na kuwapa waafrika wenzetu waziendeshe.Lakini mashirika mengi yalishindwa kuendelea kutokana na waliopewa kazi hizo walikuwa ni makada wa TANU ambao hawakuwa na elimu ya kuziendesha taasisi hizo hasa mabenki.

Hii ndio sababu elimu iliyotolewa wakati wa ukoloni ni bora sana ukilinganisha na ya leo kutokana na usimamizi mbovu wa leo.Leo mashika mengi yamekufa na machache yaliyopo yapo ICU.Hapa ndio Rais Magufuli anapaswa kupaangalia vizuri maana ni hapa ndipo viwanda vilikufa na mashirika,mabenki ya umma yalipouzwa kwa bei ya chini sana.Pia ndipo mikataba mingi inayoligharimu Taifa ilipo kama ule wa IPTL kwa TANESCO

4.Jambo la nne
Kuwahamisha vituo vya kazi watumishi wazembe
Kosa hili lilifanyika mara nyingi huenda ni kutokana na uchache wa wasomi waliokuwepo wakati huo.Lakini kosa hili mpaka leo ambapo tuna wasomi wengi bado linafanyika kwa Mfano hivi karibuni aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni alionekana kufanya makosa na akahamishiwa Babati kama ndio adhabu yake na amerudishwa Kinondoni kuja kujibu makosa yake.Kosa hili linafanya viongozi wabadhilifu na wasiowajibika kutokuwa na wasiwasi wa kupoteza ajira zako.Serikali ya awamu hii ni vyema ikaacha utaratibu huu kwani wasomi wapo wengi na hii itaongeza ufanisi kama tutaacha utaratibu huu.

5.Jambo la tano
Kujijenga yeye badala ya kujenga Taasisi
Hapa Mwl Nyerere alijijenga sana yeye kiasi cha watu kumwogopa sana yeye kuliko taasisi zinazowasimamia.Haikuwa ajabu kusikia mtu akisema nikuogope wewe kwani umekuwa Nyerere?Ingawa wakati wake kuna taasisi chache zilikuwa imara sana kama jeshi letu na vyombo vyote vya ulinzi.Kosa hili hata Rais Magufuli huenda akalifanya ingawa muda wake bado kwa kuwafanya watumishi wa umma na wananchi kumwogopa yeye kuliko taasisi za serikali.

Kwa mfano Mwananchi au mtumishi wa umma anatakiwa kuiogopa taasisi ya PCCB kwa kutokutoa rushwa kuliko kumwogopa Magufuli akigundua ubadhirifu huo ofsini kwake,au anayeingiza madawa ya kulevya na kusafirisha nyara za nchi anatakiwa kuviogopa vyombo vya ulinzi na idara ya uhamiaji kuliko kumwogopa Magufuli,vivyo hivyo mfanyabiashara anatakiwa kuiogopa zaidi TRA kuliko Magufuli kwa kulipa kodi mapema.Kujenga taasisi ni muhimu sana kwa Taifa lolote.Viongozi wengi wa kiafrika walijijenga wao kiasi cha kuamini hakuna wanaoweza kuongoza nchi zao hii ni moja ya sababu za wao kukaa madarakani muda mrefu wakiamini hakuna aliye bora kama wao.

Uchambuzi huu unaonyesha makosa machache ya Mwl Nyerere na kamwe haubezi kazi njema alizolitendea Taifa hili na kulipa sifa lukuki duniani kote na daima anabaki kiongozi wa mfano kwangu mimi na kuna mazuri mengi sana ametuachia ambayo siku nyingine nitayaandika.
 
Nakubaliana nawe kwamba mwalimu kama binadamu wengine alifanya makosa. Lakini kuna hoja sikubaliani nazo hapo juu

1. Kufuta vyama vya siasa - kila jambo na wakati wake. Wakati wa uhuru hatukuwa tayari kwa vyama vingi

2. Kutaifisha - ilikuwa muhimu ili serikali changa iweze kutoa huduma kwa usawa.
 
Watu wengi mmekuwa kama mnakariri 'Azimio la Arusha'
hivi mmewahi kulisoma kweli na kulielewa?

Watu wasiruhusiwe kumiliki mali?
marufuku kuwa na nyumba za kupangisha?

mwenye kopi ya hilo azimio alilete humu...
 
JKN alituambia RAIS anayevunja katiba aliyoapa kuilinda hatufai hata kidogo.Kwa muda mfupi tu aliokaa madarakani kaisha vunja katiba ya nchi.Leo unamteuea Mbunge kabla hajaapishwa kama Mbunge unamuapisha kuwa Waziri wakati sheria inasema aapishwe kama Mbunge baadaye ndipo aaape kama waziri.Tunaliona kama kosa dogo lakini ikiendelea hivi sijui itakuwaje.

Maana msaidizi wake naye kavunja sheria baada ya kuweka katazo la kufanya mikutano ya vyama vya SIASA wakati vyama hivi vinatambulika kisheria.

Ninamkumbuka JKN Katiba yetu ikipata DICTATOR basi kila kitu atafanya maamuzi mwenyewe,hata Bunge pia litakuwa RUBBER STAMP tu
 
Kosa jingine lilikuwa ni kuasisi muungano wa Tanzania katika muundo wenye utata mkubwa. Hadi leo sielewi nini ilikuwa nia ya Nyerere kukataa pendekezo la Karume la kuwa na muungano wa serikali moja. Kosa hili tayari Magufuli amelirithi na hawezi kulirekebisha zaidi ya kutulazimisha tuendelee na muungano huu usio na tija
 
Tunapenda sana kupoteza muda...hivi nani ambaye amefanya yaliyotukuka na akaijari democracy? Awamu ya pili? tatu? Au nne?

Mimi namuunga mkono JPM...siasa za ujuaji na uswahili ndio zimetufikisha hapa tulipo. Fanya kazi JPM. ...time will tell
 
Back
Top Bottom