Makonda, Ruge na menejimenti nzima ya CMG akiwemo Mkurugenzi Mtendaji, Joseph Kusaga, kuketi na kumaliza tofauti

The Bourne

JF-Expert Member
Aug 24, 2017
1,077
1,319
NAOMBA USIKIVU WA MAKONDA, RUGE, CMG

Agoati 5, mwaka huu, Rais John Magufuli akiwa Tanga kwenye mkutano wa pamoja na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, juu ya uzinduzi wa bomba la mafuta, aliwaita Paul Makonda na Ruge Mutahaba jukwaani na kuwasuluhisha, akisema wote anawapenda.

Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Ruge ambaye ni Mkurugenzi wa Vipindi na Utafiti, Clouds Media Group (CMG), wamekuwa kwenye mgogoro tangu Machi 17, mwaka huu, Makonda alipovamia kituo cha Clouds TV akiwa na askari wenye bunduki.

Sababu ya Makonda kuvamia Clouds TV, ilielezwa alikwenda kulazimisha kurushwa hewani maudhui yaliyokataliwa na wahusika kwenye kipindi Shilawadu. Pamoja na kulazimisha, vilevile alidaiwa kuwatisha watangazaji na mwandaaji wa kipindi kuwaingiza kwenye orodha ya wauza dawa za kulevya.

Tangu tukio hilo la uvamizi, uhusiano wa kirafiki kati ya Makonda na CMG uliingia dosari. Baadaye ikavuma zaidi kuwa mgogoro kati ya Makonda na Ruge kuliko Makonda na CMG. Wakati fulani Makonda alihojiwa na vyombo vya Sahara Communication na kumwita Ruge tapeli.

Hivyo, ni dhahiri upatanishi uliofanywa na Rais Magufuli haukukidhi viwango. Kama Rais na kama Baba Mkuu kwenye nchi, alipoona kuna umuhimu wa Ruge na Makonda kupatana, alipaswa kuwakalisha chini na kuwasuluhisha, kuliko alivyofanya kuwashitukiza, matokeo yake hakumaliza kiini.

Tangazo la juzi la Makonda kukazia sheria inayokataza shughuli za burudani kuzidi saa 6:00 usiku, huku ikifahamika kuwa Jumamosi ya wiki ijayo (Novemba 25), kwenye jiji la Dar es Salaam, litafanyika tamasha la Fiesta, ni kipimo dhahiri kwamba uhasama unaendelea.

Fiesta ni tamasha kubwa la burudani nchini ambalo huandaliwa na CMG kupitia kampuni yake tanzu ya Prime Time Promotion. Fiesta inafanyika kwa mwaka wa 16 sasa tangu mwaka 2001, ikiitwa Summer Jam, wakati huo ikifanyika Dar peke yake.

Kuanzia mwaka 2003, Fiesta ilianza kufanya ziara kabla ya kujenga utaratibu kila mwaka kwa tamasha hilo kufanyika mikoa mbalimbali na kuhitimishwa Dar. Miaka yote tangu kuanza kwake, Fiesta imekuwa ikifanyika mpaka alfajiri na hata asubuhi kabisa.

Kufupisha wingi wa maneno ni kuwa Fiesta nyumbani kwake ni Dar. Hadhi ya tamasha hilo kwa Dar huwa kubwa. Ni sawa na kusema ziara za mikoani huwa ni rasharasha, mvua kamili hunyesha Dar. Hutakosea kutamka kwamba mikoani huwa utangulizi na baadhi ya sura, kitabu hukamilishwa Dar.

Hivyo basi, tamko la Makonda kuwa matukio ya burudani viwanjani mwisho saa 6:00 usiku, ujumbe wake umetafsiriwa ni kuikomoa CMG na Fiesta yake. Hata Makonda mwenyewe bila shaka kusudio lake ni hilo ndiyo maana amesema atapiga doria kuhakikisha agizo lake linatekelezwa.

TUZUNGUMZE KITANZANIA

Ni sawa sheria inakataza shughuli za burudani kuvuka saa 6:00 usiku kwenye viwanja vya wazi. Hata hivyo, Fiesta imekuwa ikitikisa mpaka kunapambazuka na hakujawahi kuwa na mgogoro wowote. Mwaka huu baaada ya CMG kutofautiana na Makonda, ndipo msisitizo huo umewekwa.

Makonda aliapishwa kuwa Mkuu wa Mkoa Dar tangu Machi 15, mwaka jana. Hivyo, Fiesta mwaka jana ilifanyika na watu walikesha viwanja vya Leaders Club, Makonda akiwepo, tena alihojiwa na kutoa baraka kwa tamasha hilo, na kuahidi ulinzi wa kutosha.

Haitoshi, Makonda alihudhuria onesho la Fiesta Dar mwaka jana na akasheheni kweli. Alijimwaga eneo la mapumziko ya wasanii (backstage) na kupiga picha na wasanii. Selfie za kutosha kati ya Makonda na wakali walioshuka kutoka Nigeria, Yemi Alade na Tekno Miles zilihusika kikamilifu.

Unaongeza pia kuwa mwaka huu Fiesta imezunguka mikoa mingi na matukio yamefanyika mpaka kunapambazuka. Sheria hiyo ya matamasha kutozidi saa 6:00 usiku, siyo ya Dar tu bali nchi nzima na mwaka jana ilikuwepo.

Ukifika hapo, ndipo unapata ufahamu kwamba kumbe agizo la Makonda mwaka huu la muda wa matamasha kutozidi saa 6:00 usiku tafsiri yake ni kisasi au kuwakomoa CMG ili kuwaonesha yeye ni nani hasa baada ya kuwa mahasimu.

Bila shaka agizo ambalo Makonda amelitoa ni kutaka kuwathibitishia watu mamlaka yake na msuli mkubwa alionao. Ni kuwaonesha CMG kwamba anazo nguvu za kuathiri shughuli zao, hivyo hawana ubavu dhidi yake na kwamba yeye ndiye Makonda mwenye Dar es Salaam yake.

Sababu ya kufika huko ni moja, kwamba CMG baada ya tukio la Makonda kuvamia Clouds TV walimkunjia nafsi. Waliufuta urafiki wao uliokuwepo na kukaribisha zama mpya ambazo zimewafikisha hapa walipo. Zama za kukomoana na kutibuliana biashara.

Hapo ndipo swali hili linakaribishwa, je, huo ndiyo Utanzania? Kwamba kiongozi akitofautiana na raia wa kawaida anatumia mamlaka yake kumkomoa? Kwa hiyo sasa hivi uchunge kiongozi asikuchukie, utajuta!

Kama Taifa, hatupaswi kwenda hivyo. Mazingira ya sasa yenye ishara ya chuki na visasi, yanaleta harufu mbaya mno kwa nchi. Ni wazi sasa watu wanatanguliza mbele udhaifu wao wa kibinadamu kuliko busara na hekima za kiuongozi.

NISEME NA MAKONDA

Nafasi za uongozi si za kujivunia sana. Kiongozi anahitaji kutambua nafasi yake ni kuongoza na cheo ni dhamana tu. Haya si maneno mageni, bali ni mafundisho darasani na yapo kwenye kitabu cha Mwongozo wa Tanu, kwa kunakili falsafa za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Ukiwa kiongozi si sawa kujenga dhamira ya kuwafanya watu wakukome. Unapaswa kuongoza kwa misingi ya haki na usawa. Sheria zipo ili zifuatwe lakini kukiwa na mkazo wa kitabaka kuhakikisha sheria zinafuatwa, hapo ukakasi utaingia tu.

Kwa kumpa ujumbe Makonda, vema kumkumbusha kwamba unaweza kuwa kiongozi lakini ukawa huna uhalali wa nafasi uliyonayo. Kutenda kazi kwa chuki, uonevu na visasi ni kupoteza uhalali wa nafasi yako. Rais anaweza kukulinda kama Mkuu wa Mkoa lakini wananchi wakawa wameshakutema.

Tukiacha hilo, Makonda ni kijana ambaye bila shaka safari yake ya kiuongozi ni ndefu. Hivyo lazima ajitengenezee barabara vizuri. Kwa umri wake, anapaswa kupunguza maadui kila uchwao na kama itawezekana awe anaongeza marafiki.

Ikitokea kuongeza maadui, basi awaongeze wahalifu. Mathalan, majambazi, wala rushwa, wabakaji, wauaji, watekaji na kadhalika. Aongeze maadui ambao watamfanya apate baraka kwa Mungu. Si maadui wa kujitakia kwa uadui ambao hauna sababu yoyote.

Mfano, kutaja watu kuwa ni wauza unga bila kuwa na uthibitisho wowote, huo ni uadui ambao haukuwa na sababu yoyote. Kuvamia Clouds TV kisha kutakiwa kuomba radhi na kugoma, hivyo kuleta taswira ya sasa, ni uadui ambao haukuwa na sababu.

Hakuna mtu ambaye angependa sehemu yake ya kazi ivamiwe na kukosewa adabu hata kama mvamizi huyo ni mkubwa kiasi gani. Tukio la uvamizi Clouds TV itabaki hivyo kwamba CMG hawakutendewa haki na Makonda alikuwa na nafasi ya kusahihisha.

Umvamie mtu ofisini kwake na kulazimisha matakwa yaliyo nje ya maadili ya kazi yake kitaaluma. Baada ya hapo utake wale uliowatendea ndiyo wawe wanyonge kisa wewe ni kiongozi. Kwa hilo ni hapana! Huo siyo utu, siyo uongozi na si Utanzania uliowekewa misingi kupitia na Mwalimu Nyerere.

Zaidi ya hapo ni kuwa ukiwa kiongozi kijana ni lazima ujiepushe na minyukano binafsi na watu ambao ni haohao ungependa kuwaongoza nyakati zijazo. Unatakiwa kuelewa kuwa maisha yanaendelea na deni la kuishi ni kubwa kuliko la mzee.

Mathalan, Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe na kila anachokifanya, kwa umri wake wa miaka 93 alionao sasa, anakuwa anajifahamu kwamba yupo ukingoni. Hivyo hata akijiharibia anajua hana safari ndefu.

Makonda kwa umri wa miaka 35 alionao hivi sasa, ana miaka mingi ya kufanya siasa. Hata kama ataacha siasa, ni ukweli kwamba bado anao umri mrefu wa kuishi kama Mungu atamruzuku uhai zaidi. Hivyo, hapaswi kujisahau na kuishi kama vile dunia inaisha miaka mitatu ijayo.

TUZUNGUMZE KWA MIFANO

Dar es Salaam ilishapata kuwa na Mkuu wa Mkoa maarufu mno. Mzawa wa Dar na mtoto wa mjini wa kweli. Jina lake ni Ukiwaona Ditopile Mzuzuri. Alijua mizungu ya siasa na alijivuna kwa namna alivyokwenda na wakati. Hata hivyo, Aprili 20, 2008, alifariki dunia.

Dito alifikwa na mauti akiwa hana cheo chochote, ikiwa ni takriban miaka miwili tangu alipoingia matatani kwa kumpiga risasi dereva wa daladala iliyokuwa ikifanya safari zake Kawe-Tegeta, Hassan Mbonde. Wakati anaingia kwenye matatizo hayo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora.

Tukio la Mbonde lilimfanya Dito ajiuzulu ili kuruhusu vyombo vya usalama vifanye kazi yake. Dito akawa wa mahakamani na mahabusu. Mahakamani akageuka mcheza sinema za kuficha uso ili waandishi wa habari wasimpige picha.

Huyo ni Dito ambaye mfumo wote wa nchi ulimuelewa. Dito aliyesoma pamoja na Rais wa nchi wakati akiingia matatizoni, Jakaya Kikwete. Dito na Jakaya walichangia bweni Chuo Kikuu Dar (UDSM) na wakawa marafiki wakubwa. Alikuwa Dito kweli.

Na majina yake yale, Ukiwaona Ramadhan Ditopile Mwinshehe wa Mzuzuri, ungempenda kwa mikogo yake akizungumza. Kiswahili alikijua vizuri, kile kilichonyooka na cha mtaani. Alijiamini na alipenda kuwakaririsha watu wa kwa maneno "mimi mtoto wa mjini kweli!"

Mtu wa mizaha aliyeijua vilivyo mizungu ya watoto wa mjini. Watu wakazoea kumwita Brother Dito (Kaka Dito). Alianza kuchipukia kwenye siasa wakati wa Mwalimu Nyerere kama kijana msomi, Serikali za awamu ya pili na tatu chini ya Alhaj Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa alikuwemo kwenye mfumo.

Tukio la Dito linafundisha uongozi na unyenyekevu. Usitake madaraka yako uyatumie kuwafanya watu wakujue wewe nani. Ukiwa kiongozi maana yake umepewa dhamana ya kutumikia watu. Sasa wewe mtumishi wa watu vishindo vya nini? Napenda sana Makonda kama kijana ayaelewe haya ili awe na safari ndefu iliyobarikiwa katika uongozi na maisha.

KUNA MFANO HUU

Libya ina mtu anaitwa Saif Al-Islam. Miaka sita iliyopita kurudi nyuma alikuwa na nguvu na alitambulika kama Waziri Mkuu asiyetamkwa kisheria (de facto prime minister). Hii ni kwa sababu Saif alikuwa na nguvu ya kuamrisha na kuagiza chochote pasipo kupingwa na yeyote.

Saif ni mtoto wa aliyekuwa kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi. Ni kijana msomi mwenye shahada ya udaktari wa falsafa (PhD) katika uhandisi. Baba kiongozi wa Taifa na anang'ang'ania madaraka utafikiri ni mtume aliyeshushwa na Mungu. Mtoto injinia mwenye shahada ya uzamivu.

Gaddafi akamuona Saif ni mtoto mwenye akili kuliko wanaye wengine wote. Akampa upendeleo kiasi kwamba watu wakasema ni Waziri Mkuu ambaye hajahalalishwa kisheria, lakini kivitendo hakuna aliyekuwa na jeuri ya kupinga amri za Saif.

Ilipofika Oktoba 20, 2011, Gaddafi alipopinduliwa na kuuawa na waasi waliosaidiwa na Marekani, Saif alianza zama mpya za kuishi kwenye mateso. Alitafutwa na alipokamatwa aliteswa na kukatwa vidole kisha akafungwa jela miaka mitano kabla ya kusamehewa Juni mwaka huu kwa agizo la Mkuu wa Serikali ya Tobruk, Libya, Kamanda Khalifa Haftar.

Vema kutambua kuwa unyenyekevu ni tiba kubwa. Saif alidhani nchi ni ya baba yake, hivyo kufanya kila aina ya vurugu. Alionea watu, aliua na alitaka atambulike kuwa yeye akiamua kwenye nchi lolote linaweza kutokea. Kimbelembele chake ndicho kilisababusha Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) itoe hati ya kumkamata.

Mapito ya Saif kwa kiburi cha mamlaka ya baba yake, si mfano unaomfaa Makonda, lakini vema kukumbusha kwamba Saif na watoto wengine wa Gaddafi kwa namna walivyotumia vibaya rasilimali za umma na kuishi kifahari mno, ni sababu ya baba yao kuchukiwa.

Hata Makonda anaweza kuwa sababu ya Rais John Magufuli kuchukiwa, maana tafsiri ya wengi ni kuwa vitendo vyake vinaakisi jeuri anayopewa na Rais. Isisahaulike kwamba Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye, aliondolewa Uwaziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa sababu ya kujaribu kusimamia haki juu ya tukio la uvamizi Clouds TV.

Hakuna ubaya wowote kumkumbusha Makonda kuwa siku hizi hasikiki kabisa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Katibu wa Halmashauri Kuu (Nec) CCM, Itikadi na Uenezi, Omar Mapuri. Alizimika na kizazi kipya hakijui kama Mzanzibari huyo aliwahi kutikisa nchi balaa.

KWA RUGE NA MAKONDA

Si afya hata baada ya Rais Magufuli kuwapatanisha kuendelea na uhasama, japo njia ya upatanishi haikuwa nzuri. Ifahamike kuwa namna yoyote ya kudhihirisha chuki ya kila upande ni kumvunjia heshima Rais ambaye aliamua kuwapatanisha hadharani.

Ruge akiwa bosi wa CMG, taasisi yake ilishirikiana vizuri na Makonda alipokuwa kwenye kampeni yake ya Dar Mpya ambayo maudhui yake yalikuwa kujenga ustawi bora wa kimaisha kwenye Mkoa wa Dar es Salaam.

Hivyo ndivyo ambavyo ushirikiano unapaswa kuwa. Inapotokea tofauti, watu kukoseana, ambacho hufuata ni kukaa chini kuzungumza na kusameheana. Haipendezi siku zinapita, chuki inabaki ileile, wakati kulikuwa na ushirikiano mzuri hapo awali.

Makonda atambue kuwa tukio la uvamizi Clouds TV hakumkosea Ruge peke yake, bali taasisi nzima ya CMG na tasnia ya habari kwa jumla. Hakuna mwandishi wa habari mwenye kujitambua anaweza kuchekelea kilichofanyika. Hivyo, ilikuwa rahisi kulimaliza kwa mazungumzo.

Katika hili si ubaya kumkumbusha Makonda kwamba ukuu wa mkoa ni cheo chenye kupita. Anaweza kuondolewa na Rais au Rais ajaye asimtake. Vema unapoishi leo utazame kesho mguu wako utakanyaga wapi.

Itambulike kuwa CMG ni taasisi ambayo imejijenga kwa miaka mingi sasa. Inasaidia kukuza Pato la Taifa na imeajiri watu wengi. Kiongozi wa Serikali kugombana na oganaizesheni ya namna hiyo ni kutokuwaza vizuri. Zaidi CMG ilikuwepo tangu Mkuu wa Mkoa Dar ni Yusuf Makamba na itaendelea kuwepo.

Acha CMG itifuane na EFM kwa sababu ni mgogoro wa kibiashara. Hata vita ya Vinega na miradi yao ya Antivirus ilikuwa biashara, kwamba baadhi ya wasanii waliona wanabaniwa na CMG. Siyo kiongozi wa Serikali kugombana na CMG katika mgogoro usio na chembe ya maslahi ya umma.

Muhimu zaidi kukumbusha ni kuwa nchi haipo sawa upande wa kipato. Leo hii hakuna matamasha ya kutosha ya burudani. Hii maana yake mizunguko ya kifedha kwa wasanii imepungua. Uwepo wa Fiesta unasaidia wasanii wengi kupata vipato.

Sasa basi, kwa maslahi ya sanaa na uchumi wa nchi, kila kiongozi angesaidia kwa namna moja au nyingine Fiesta ifanyike kwa mafanikio na malengo yafikiwe. Ni kweli akina Ruge wanapata, ila wasanii wananufaika pamoja wafanyabiashara mbalimbali kupitia fursa zitokanazo na Fiesta. Usiifikirie Fiesta kwa jicho moja.

USHAURI KWA CMG

Inawezekana kufanya tamasha bora lenye ukomo wa saa 6:00 usiku. Muhimu ni kupanga ratiba ianze mapema. Changamoto ya safari hii wakiitumia vizuri inawezekana kupata kundi kubwa la watu waliokuwa wakiikosa Fiesta miaka yote kwa sababu ya kutomudu kuhudhuria usiku.

Kila kitu ni mipango na ubunifu, eneo ambalo timu ya Prime Time imejijengea sifa ya kulimudu inavyotakiwa. Mapokeo ya Fiesta kila mwaka yanadhihirisha tamasha hilo limegeuka sehemu ya maisha ya Watanzania na wasanii kwa jumla.

Kwa maana hiyo, ikitangazwa kuwa Fiesta inaanza saa 10 alasiri watu wataingia na pengine mahudhurio yatakuwa na kishindo, kwani hata wale wasiopenda kutoka usiku nyumbani, watajipanga waende Fiesta ili warejee katika muda ambao hautakuwa mbaya kwao.

Ni muda sasa wa kuifanya Fiesta iguse tabaka kubwa zaidi mpaka watoto, kwamba badala ya kuwa tamasha la saa 8 mpaka 10 kwa siku, liwe la saa 16 mpaka 18. Milango ifunguliwe asubuhi kwa ajili ya watoto ili nao wawe na sehemu yao kisha wanaondolewa, huku burudani kwa wakubwa zikiendelea mpaka saa 6:00 usiku.

Ipo hoja ya kupunguza wasanii ili kukidhi ya agizo la muda kama ilivyosemwa na Makonda. Hili hapana, vema kuanza mapema ili wasanii wote waliokusudiwa washiriki. Nafahamu ni ndoto ya wasanii wengi kuwepo Fiesta ya Dar. Bora wakose mikoani lakini siyo Dar. Kuwakata ni kuwaumiza kisanii na kifedha.

Mwisho kabisa ni kutaka Makonda, Ruge na menejimenti nzima ya CMG akiwemo Mkurugenzi Mtendaji, Joseph Kusaga, kuketi na kumaliza tofauti. Hakuna lenye kushindikana kwenye meza ya mazungumzo kama kweli nia ipo.

Kila la heri mazungumzo yenye maslahi ya nchi na sanaa. Kila la heri wasanii wote. Kila la heri Fiesta Dar 2017.

Ndimi Luqman MALOTO

1e1ec5e0789be6c615a4c25396aacf17.jpg
 
Hivyo, ni dhahiri upatanishi uliofanywa na Rais Magufuli haukukidhi viwango. Kama Rais na kama Baba Mkuu kwenye nchi, alipoona kuna umuhimu wa Ruge na Makonda kupatana, alipaswa kuwakalisha chini na kuwasuluhisha, kuliko alivyofanya kuwashitukiza, matokeo yake hakumaliza kiini.
We jamaa unachekesha si kidogo...!!

Yaani Rais wa nchi asuluhishe mkuu wake wa mkoa na mtendaji wa radio binafsi kwa kufuata utaratibu maalumu!!!! Are you serious?!

Yaani rais yule yule tunayeambiwa akisema jambo hilo ni agizo linalopaswa kutekelezwa lakini hapa unada alitakiwa kufanya tofauti!!!

Waswahili wana msemo "ukicheza na mbwa, atakufuata hadi msikitini!"

Hii ni aibu kwa Rais John Pombe Joseph Magufuli! Kacheza na Makonda sawa na mtu anavyocheza na mbwa! Kamkingia kifua kwa kila jambo! Imefika wakati, rais anatoa agizo, Makonda kampuuza... kamuona boya tu! Hiyo ndiyo maana ya ukicheza na mbwa utaingia nae hadi msikitini!!!

Kwa waliofuatilia tangu "upatanisho" ule ufanyike wanafahamu ni Makonda ndie hakutaka kusikiliza maagizo ya mkuu wake... mkuu wake ambae ni rais wa nchi!

Baada ya rais kutoa agizo lile, siku chache baadae, Jukwaa la Wahariri likawakutanisha Makonda na Ruge! Bila kupepesa macho wala hofu, pale pale Makonda akaonesha ni namna gani usuluhisho ule hakuwa na haja nao!!!!

Narudia, rais wa nchi, hususani rais anayeongoza kwa kutumia katiba ya Tanzania hana sababu ya eti "...alipaswa kuwakalisha chini na kuwasuluhisha!" Labda kama unazungumzia rais wa TFF au wa taasisi nyingine lakini sio rais wa nchi!

JPM kama rais alichofanya kilitosha kwa 100% hasa ukizingatia mmoja wa wale waliotakiwa kutafuta suluhu ni mtu aliye chini yake... amemteua mwenyewe!
 
Maelezo mazuri.. Ushauri mzuri.

Kwa kufanya hivi, Rais amekubali Makonda amdharau kwa kiasi kilichopitiliza..

Kuna kitu huyu rc anampatia mkulu wengi wetu hatukifamu mpaka hivi sasa..

Matendo yake huyu rc lazima kuna kitu anampa Mkulu na ndio sababu ya Mkulu kukubali dharau zote hizi..

Muda ni msema kweli, hicho kitu kitajulikana tu.
 
MALOTO amepoteza muda nguvu na akili zake nyingiiiii kushauri ujinga usioweza kuleta tija yoyote...kwamfano
Makonda ni nani? Ni malaika na atakaa milele ikulu?
Ruge na cmg ni nani? Mbona nao wamelalamikiwa sana kuwanyanyasa wasanii mpaka wakatokea vinega na sugu kina lady jd....
HAPA NAONA NI MNYOOSHANO WA MADHALIMU NA MAJAMBAZI WAWILI KWA MANUFAA YA WANANCHI NA WASANII WA KAWAIDA...

CMG wafe waishe kama fiesta isipofanyika dar....ila pia na bashite hata asipokufa miaka ya boss wake ikiisha atakaa benchi maisha mengine yataendelea.

MALOTO FANYA KAZIIII....ACHA HIZI HABARI NI NDOGO SANA KWAKO.
 
Clouds wanatakiwa kujua Thamani ya bidhaa au huduma uamliwa na nguvu ya soko au mahitaji si kitu kingine kama unabidhaa bora na nzuri watakuja kwako tu hata kama huduma au bidhaa yako inapatikana kwa masaa mawili tu badala ya masaa 24
 
hawa wanajuana wenyewe tuwaachie watamalizana kama mh rais alijaribu na akashidwa basi hamna namna tuwe watazamaji wa hii ngoma tuone mwisho wake
 
Back
Top Bottom