Makanisa, Waislamu wajadili baraza jipya | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Makanisa, Waislamu wajadili baraza jipya

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by MziziMkavu, Oct 22, 2009.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Oct 22, 2009
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,611
  Trophy Points: 280
  Wasomi wapendekeza liundwe

  Askofu Mkuu Dk. Mokiwa ataka lisiundwe na Serikali

  Askofu Mkuu Dk. Mokiwa ataka lisiundwe na Serikali

  MJADALA kuhusu masuala ya dini na siasa umeanza kuchukua sura mpya kwa kuhusisha wasomi nchini, wakiwamo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambao wamelazimika kuendesha utafiti mahsusi kwa miaka kadhaa ili kutafuta namna ambayo itadhibiti vurugu ambazo chanzo chake ni dini.

  Mapendekezo hayo ya wasomi yamepokelewa kwa hisia tofauti na dini kuu mbili za Kikristo na Kiislamu, ambako viongozi wakuu wa dini hizo wametoa mapendekezo yao.

  Wasomi waliokamilisha utafiti wao miaka mitatu iliyopita wamechapisha kitabu maalumu kinachoitwa Religion and Politics (Dini na Siasa) ambacho hata hivyo, kimeandikwa kwa lugha ya Kiingereza, jambo ambalo linaweza kuwa kikwazo kwa viongozi wa dini na wanasiasa wenye matatizo na lugha hiyo kutafakari kwa uhuru kinachoelezwa kitabuni humo.

  Utafiti huo katika kitabu hicho ambacho licha ya kukamilika mwaka 2006 kilizinduliwa wiki mbili zilizopita katika Ukumbi wa Nkrumah, Chuo Kikuu Dar es Salaam, pamoja na mambo mengine, umependekeza kuanzishwa kwa Baraza Maalumu kwa ajili ya kudhibiti vurugu zinazoweza kutokea ndani ya dini moja au kati ya dini moja na nyingine.

  Profesa Samuel Mushi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Idara ya Siasa na Utawala, anazungumzia mapendekezo ya kuanzisha chombo cha udhibiti kuwa lengo ni kushughulikia migogoro ya kidini, hususan viashiria vya migogoro hiyo.

  “Katika miaka ya kuanzia 1990 na 2000 kumejitokeza matukio ambayo si mazuri ndani ya dini. Kumewahi kuibuka migogoro ya kugombea dayosisi mfano, kule Meru na Mwanga, lakini pia kumewahi kuzuka vurugu za kuteka misikiti. Ndani ya dhehebu moja nako kumeibuka wanamaombi na wengi wenye msimamo wa asili,”

  “Lakini pia wakati fulani kunajitokeza kama aina ya mkwaruzano kati ya dola na dini, mfano vurugu za eneo la Mwembechai, jijini Dar es Salaam. Kwa hiyo, kama wasomi tunadhani si vizuri kuacha viashiria hivi vya vurugu kuzidi kushamiri, kwamba watu wakiamua kuteka misikiti na kufanya mapinduzi wanafanya hivyo, wakiamua kuvurugana makanisani ibaki hivyo,” anasema Profesa Mushi na kuongeza kuwa;

  “Kadiri umasikini miongoni mwa Watanzania unavyozidi, ndivyo watu wanavyohangaika kujitafutia kipato na wapo pia wanaohaha kujiunganisha katika makundi madogo madogo wakijiona wote ni masikini. Lakini wanaweza kujiunganisha kwa kuegemea misingi ya udini, ukabila au uzawa.

  “Kwa hiyo kunakuwa na makundi madogo yenye kudhamiria kujikinga na athari za kidunia kama utandawazi, na hasa huu mchakato wa mabadiliko ya ideology (itikadi) kutoka Ujamaa kwenda kwenye soko huria, wananchi wengi wanaumia. Kwa hiyo tumetafiti na kuona eneo ambalo linaweza kuwa na viashiria vya vurugu ni upande wa dini na siasa, hivyo kuwa na chombo ambacho sijui itaamuliwa kipewe jina gani muhimu.”

  Hata hivyo, wakati wasomi, kupitia kwa Profesa Mushi ambaye ni mmoja wa wajumbe wa jopo lililohusika kuandaa kitabu hicho wakiwa na mtazamo huo, Mwenyekiti wa Baraza la Wakristo Tanzania (CCT), Askofu Dk. Valentino Mokiwa, anaamini hilo linaweza kuwa moja ya mapendekezo mazuri lakini kwa masharti maalumu.

  Anataja masharti hayo kuwa ni lazima chombo hicho kisianzishwe na serikali, ingawa pia serikali inaweza kushirikishwa akiamini kuwa itakuwa ni kuingilia uhuru wa dini kuendesha shughuli zake kama serikali itaanzishwa chombo hicho na kisha kualika viongozi wa dini.

  “Hatutakuwa tayari kuunga mkono chombo hicho kama kitakuwa mali ya serikali…kitaanzishwa na serikali. Lakini itakuwa na maana zaidi kama kitakuwa chombo huru cha wadau husika, na serikali ikishirikishwa. Hapo tutaweza kufanikisha malengo yanayotarajiwa,” anasema Dk. Mokiwa na kuongeza kuwa; “Tunatumaini itakuwa hivyo ili kutopoteza maana inayokusudiwa.”

  Kuhusu hilo, Profesa Mushi anasema; “Tungependa na ndiyo ushauri wetu chombo hiki kiundwe na viongozi wa dini kwa kuishirikisha serikali, lakini kisiundwe moja kwa moja na serikali.”

  Kwa upande wake, Mufti wa Tanzania, Sheikh Shaaban bin Simba, anazungumzia suala la uanzishwaji wa chombo hicho akionekana kuunga mkono lakini pia akiwa na msimamo kama wa Dk. Mokiwa na Profesa Mushi.

  “Ni jambo zuri na jema. Jambo la msingi nchini hapa ni amani…unajua amani inajengwa haiteremki tu kama mvua na ujenzi ni pamoja na kuziba zile nyufa zinazojitokeza. Kwanza mtambue nyufa zinatokea upande gani na kisha muanze ujenzi. Kwa hiyo ili tuwe na amani ya kudumu lazima tuwe wepesi kutambua nyufa na kuziziba, anasema Mufti na kuongeza kuwa;

  Kuanzishwa kwa chombo hicho si jambo baya, bali ni jambo lenye nia njema na kwamba kitakuwa chombo kinachoweza kufanya kazi yake kwa kuongozwa na busara za kiimani zaidi na kwamba matarajio yaliyopo ni kuwa kitakuwa na manufaa kwa taifa zima.

  Akionyesha kutokukubali chombo hicho kiundwe na serikali, Mufti Simba anasema†: ´†Si sahihi kiundwe na serikali. Kwanza katika mfumo wa nchi yetu serikali huweza kubadilishwa wakati wa uchaguzi na kunapokuwa na mabadiliko mipango mingine inaweza pia kubadilika, kwa hiyo ni vema kikaundwa na viongozi wa dini kwa kuwashirikisha wadau wengine.†ª

  Uzinduzi wa kitabu hiki wiki mbili zilizopita, licha ya kuandikwa tangu mwaka 2006 umekuja zikiwa zimepita wiki kadhaa tangu Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ikutane mjini Dodoma na kutoa mapendekezo kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuwataka viongozi wakuu wa kisiasa kukutana na viongozi wa dini kuzungumzia kile kinachoweza kutafsiriwa kuwa hali ya mvutano kati ya viongozi hao wa dini na siasa, na hasa viongozi hao kujisogeza karibu zaidi na waumini wao kwa kuwapa elimu ya uraia, inayolenga namna ya kuchagua viongozi.

  Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya kitaifa wanatafsiri mapendekezo ya kuanzishwa kwa chombo hicho kuwa yanaweza kuleta utata zaidi kwa kuwa shughuli za chombo hicho ni wazi zitakuwa zikichanganya masuala ya dini na siasa, mambo ambayo kwa tafsiri ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania siasa huzaa viongozi wa kisiasa ambao huongoza nchi, lakini dini yenye viongozi wa dini hawana nafasi kwenye uongozi wa kidola ingawa pia wako huru kuendesha shughuli zao.

  http://www.raiamwema.co.tz/index.php?d=103
   
Loading...