Makamba: Sijaenguliwa, ni utaratibu | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Makamba: Sijaenguliwa, ni utaratibu

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by BAK, Dec 24, 2008.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Dec 24, 2008
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,449
  Likes Received: 81,504
  Trophy Points: 280
  Date::12/23/2008
  Makamba:Sijaenguliwa, ni utaratibu

  Na Jackson Odoyo
  Mwananchi

  SIKU moja baada ya Kamati Kuu ya CCM kumuengua katibu Mkuu wake Yusufu Makamba kuongoza kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Mbeya Vijijini, Yusuf makamba amejitetea kuwa hajaenguliwa, bali huo ndio utaratibu mpya wa chama chake.

  Makamba ndiye aliyekuwa kinara wa kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Tarime ambako CCM iliangushwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), lakini sasa hatasimamia tena kampeni kwenye jimbo la Mbeya Vijijini baada ya Kamati Kuu ya CCM kuamua kuuachia mkoa jukumu hilo.

  Kutokana na kushindwa kwa CCM kwenye jimbo la Tarime, Makamba, ambaye ni katibu mkuu wa chama hicho, alilaumiwa sana akidaiwa kushindwa kuzika tofauti zilizoibuka kwenye uchaguzi wa mwaka 2005, kutumia wapiga debe kutoka Dar es salaam ambao walihamia CCM kutoka vyama vya upinzani, na kushindwa kutumia vizuri vitendea kazi alivyopewa, ikiwa ni pamoja na helikopta mbili kwenye uchaguzi huo unaosemekana kuwa ulitumia fedha nyingi.

  Lakini Makamba, akiongea na Mwananchi, alisema kuenguliwa kwake kunatokana na CCM kubadilishwa kwa utaratibu, akidai kuwa CCM ina utaratibu wake na mbinu nyingi za kufanya kampeni.

  “Huu uliotumika ni moja kati ya taratibu zetu na si kwamba nimeondolewa,” alisema na kuongeza:

  “Mimi sijaondolewa ila mimi safari hii ni mwezeshaji katika kampeni hizo na kazi yangu ni kuangalia mahitaji muhimu wakati wa kampeni, mfano kamati ikiniambia niwapelekee flana nitapeleka; wakiniambia wanataka fedha, nitawapa; wakiniambiwa niwape usafiri wa magari ama helikopta, pia nitawapa.

  “Tarime tulikwenda na tukakaa huko kipindi chote cha kampeni na huo ulikuwa utaratibu wetu. Safari hii tutakwenda kusaidia kampeni na kurudi, huo pia ni utaratibu wa CCM.

  "Mfano mimi ninakwenda Januari mbili, na Januari tatu tutakuwa na mkutano wa kamati ya siasa, January nne ni siku ya uzinduzi baada ya hapo nitaongoza kampeni hadi Januari saba na baadaye nitarejea Dar.”

  Alisema baada ya kurudi ataendelea na majukumu mengine ya kazi na akitaka kwenda Mbeya siku yoyote ataenda na kwamba hakuna wa kumzuia kwa sababu yeye ndiye msimamizi.


  Makamba pia alirejea kauli yake kuwa alikubali kupokea lawama katika uchaguzi wa Tarime kwa sababu yeye ni kiongozi wa chama na kwamba endapo CCM ingeshinda katika uchaguzi huo, ni yeye ambaye angepongezwa.

  Aliongeza kwamba hata katika uchaguzi huo wa Mbeya Vijijini, CCM ikishindwa tena yuko tayari kupokea lawama kwa kuwa ni kiongozi na kwamba wala hawezi kuwazuia wanachama kumlaumu.

  “Kulaumiwa ni kitu cha kawaida kwa kiongozi yeyote na ukiogopa lawama huwezi kuwa kiongozi," alisema.

  Uchaguzi huo unafanyika baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Richard Nyaulawa kufariki dunia wiki chache zilizopita.

  Katika Uchaguzi huo CCM imemsimamisha Mchangaji Luckson Mwanjale.
   
 2. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #2
  Dec 24, 2008
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,449
  Likes Received: 81,504
  Trophy Points: 280
  CCM sasa ngoma nzito Mbeya Vijijini

  • Wabunge wake wagawanyika

  na Mwandishi Wetu
  Tanzania Daima~Sauti ya Watu

  ZIKIWA zimebaki siku tano kabla ya kuanza kampeni za uchaguzi mdogo Mbeya Vijijini, hali ya kisiasa ndani na nje ya vyama vinavyoshiriki kwenye uchaguzi huo inaonyesha kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kipo katika wakati ngumu wa kuendelea kushikilia kiti hicho kilichokuwa chini ya mbunge wake, marehemu Richard Nyaulawa.

  Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima, unaonyesha kuwa moja ya mambo yanayoiweka CCM katika nafasi ngumu kwenye uchaguzi huo ni mgombea wake, Mchungaji Luckson Mwanjale, kutoungwa mkono na wabunge wa mkoa huo kutokana na tofauti za makundi yaliyokuwapo mwaka 2005 wakati wa mchakato wa kusaka mgombea urais.

  Mmoja wa wabunge wa mkoa huo aliyezungumza na Tanzania Daima kwa sharti la kutotajwa, alisema Mchungaji Mwanjale alikuwa mwana mtandao asilia, hivyo hakumuunga mkono Profesa Mark Mwandosya (kutoka Mbeya) aliyewania kiti hicho na kushindwa na Rais Jakaya Kikwete.

  Makundi hayo ndiyo yanayoendelea kuutafuna Mkoa wa Mbeya na ndiyo sababu ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuph Makamba kushindwa kufika mkoani Mbeya katika ziara yake ya hivi karibuni aliyoishia mkoani Iringa, baadaye Dodoma na Arusha.

  Wakati Makamba akiwa mkoani Iringa, iliwahi kuripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa CCM Mbeya hawamtaki Makamba mkoani humo, taarifa ambayo hata hivyo baadaye ilikanushwa na chama hicho tawala.

  Ukiachia mpasuko huo, habari zaidi zinadai kuwa mgombea huyo hana sifa za kutosha kuungwa mkono na wananchi wa jimbo hilo kutokana na elimu yake, ikilinganishwa na wagombea waliopitishwa na vyama vingine vya CHADEMA na CUF.

  "Mwanjale alishaomba kuteuliwa kuwania ubunge katika jimbo hilo kupitia CCM mara tatu na mara zote alishindwa kutokana na kuzidiwa sifa na wagombea wenzake kama alivyozidiwa na marehemu Nyaulawa katika uteuzi wa ubunge, mwaka 2005, sasa safari hii sifa hizo amezipata wapi?" alisema mchambuzi huyo wa siasa ambaye hakupenda jina lake litajwe.

  Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanailezea hali hiyo kuwa inaweza kumwathiri mgombea huyo na chama chake, kwa kuwa wananchi wanaweza kuhofia kumchagua kwa sababu alishathibitika kuzidiwa sifa na wagombea waliopita.

  Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, John Chiligati, aliripotiwa na waandishi wa habari Jumapili iliyopita, akikiri kuwa Mwanjale alishaomba kuteuliwa kuwania kiti hicho katika chaguzi zilizopita lakini hakupitishwa kwa madai kuwa alikuwa hajakomaa kisiasa.

  Chiligati alisema CCM imempitisha mgombea huyo baada ya kuona sasa amekomaa na kudhihirisha uvumilivu na ustahimilivu mkubwa wa kisiasa, kwani angeweza kukimbilia upinzani.

  Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wanauona msimamo huo wa CCM kumtetea mgombea wake, kuwa unakiweka chama hicho kikongwe nchini katika mazingira hatarishi kwenye uchaguzi huo.

  Wanaona kuwa itawawia vigumu wananchi kuamini kwa haraka ukomavu wa mgombea huyo katika kipindi cha kampeni, hasa ikizingatiwa kuwa hakuungwa mkono na chama chake huko nyuma.

  "Hii inaweza kusababisha wananchi kuamua kutafuta chaguo lililo bora kutoka vyama vingine," alisema mmoja wa wataalamu hao.

  Baadhi yao wanakitafsiri kitendo cha CCM kumpitisha mgombea huyo kuwa kimechangiwa na kukosa mgombea mwingine mwenye umaarufu kati ya waliojitokeza, baada ya kuepuka kumpitisha, Jenerali Mstaafu Robert Mboma, kutokana na kushambuliwa tangu awali.

  Mwanjale (58), Katibu wa CCM jimboni humo na mchungaji wa dhehebu la Uinjilisiti, mwenye stashahada ya ufundi, anaonekana kuwa dhaifu mbele ya mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Shambwee Shitambala, ambaye kitaaluma ni wakili, na mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF), Daudi Mponzi, ambaye ni Mhandisi wa Mawasiliano.

  Aidha, katika miaka ya hivi karibuni, CCM inaonekana kupungukiwa wanasiasa wenye mvuto na uwezo wa kulitawala jukwaa la kisiasa katika mikutano ya kampeni zake, hasa baada ya gwiji lake la kampeni, Makamu Mwenyekiti Mstaafu, John Malecela, kutopenda kushiriki kwenye kampeni kama ilivyokuwa Tarime, ambapo CCM ilimteua kuwa mmoja wa wapiga debe wake, lakini hakushiriki.

  Uamuzi wa CCM kupanga kumtumia Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, katika uzinduzi wa kampeni zake, unadaiwa kuwa unaweza kutia doa kampeni hizo, kutokana na tuhuma nyingi za ufisadi kudaiwa kuwa zilianzia katika awamu yake.

  Kwa upande mwingine, umaarufu wa CCM katika jimbo hilo na Mkoa wa Mbeya kwa ujumla unaonekana kupungua, hasa ikizingatiwa kuwa Rais Kikwete, alipofanya ziara mkoani humo, msafara wake uliripotiwa kutupiwa mawe na wananchi wanaodaiwa kuwa na hasira na kutotekelezwa kwa ahadi ya maisha bora kwa kila Mtanzania.

  CCM inatarajiwa kuzindua kampeni zake Januari 4, mwaka 2009.
   
Loading...