Makala: NHIF na gharama za upasuaji wa kujifungua

Makala: NHIF na gharama za upasuaji wa kujifungua

News Tz1

Member
Joined
Nov 28, 2025
Posts
25
Reaction score
30
Makala sehemu ya pili
e07836d5-0b19-4e75-960f-66d5267e1944.jpeg

Kwa akina Mama wengi, ujauzito na kujifungua ni safari inayohitaji utulivu wa akili na uhakika wa huduma bora za afya. Hata hivyo, kwa baadhi ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam, furaha ya kumpokea mtoto imegeuka kuwa mzigo wa hofu na mshtuko wa kifedha, baada ya kujikuta wakitozwa gharama kubwa za kujifungua kwa upasuaji licha ya kuwa na bima ya afya ya NHIF.

Baadhi ya akina Mama kutokea maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam wanaibua malalamiko yao kuhusu kutozwa gharama za kujifungua kwa upasuaji (operesheni) licha ya kuwa na bima ya afya ya NHIF. Wanadai hali hiyo inawakatisha tamaa na kuibua maswali kuhusu ufanisi wa bima hiyo, ambayo imekuwa ikitangazwa kama mkombozi wa wananchi wa kipato cha chini.

Katika hospitali mbalimbali za rufaa na binafsi zinazokubali NHIF, baadhi ya wanawake wamejikuta wakitozwa gharama za ziada, zikiwemo dawa, vifaa tiba na hata malipo ya upasuaji, jambo linalopingana na matarajio yao.

Bi. Asha Issa (32), mkazi wa Temeke, anasimulia uzoefu wake wa kujifungua kwa upasuaji katika hospitali moja jijini Dar es Salaam.

“Nilikuwa na NHIF na nilijua itanisaidia kugharamia kila kitu. Lakini baada ya upasuaji niliambiwa nitoe zaidi ya shilingi laki nne kwa ajili ya dawa na vifaa. Nilishangaa sana, maana nilidhani bima inagharamia kila kitu,” anasema Asha ambaye alijifungulia kwenye hospitali ya Rufaa Temeke
19660658-c544-46c3-a89d-20eaf86d1350.jpeg

Malalamiko kama hayo yamekuwa yakisikika mara kwa mara, hasa kwa wanawake wanaojifungua kwa njia ya upasuaji wa dharura. Wengi wao wanasema hawapewi maelezo ya kina kabla ya kupata huduma, bali hukutana na madai ya malipo baada ya huduma kukamilika.

Makala sehemu ya kwanza Dar: Gharama zinavyowaweka njiapanda akina Mama wanaojifungua kwa upasuaji

Kwa upande wa wanaume, nao hawajasalia nyuma katika kuonesha masikitiko yao. Bw. Johansen J, mkazi wa Ilala, ambaye mke wake alijifungua kwa upasuaji miezi minne iliyopita, anasema hali hiyo ilimweka katika msukosuko wa kifedha.

“Nilikuwa na uhakika NHIF ingetulinda. Lakini baada ya mke wangu kujifungua, niliambiwa nitoe pesa taslimu. Ilibidi nikopeshe kwa haraka. Inaumiza kuona bima uliyochangia kwa miaka haikusaidii wakati muhimu. Tunaomba mamlaka zitazame suala hili, maana kuna familia zinaumia,” anasema J, ambaye mke wake alijifungulia kwenye hospitali ya Lugalo Jijini Dar es salaam.

" Inatokea zaidi huduma zinapopishana na thamani ya kifurushi cha Bima"

Mtaalam wa Afya kutoka katika Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala iliyopo Dar es salaam ambaye hakutaka jina lake kutajwa, anasema changamoto hiyo inatokana na tofauti kati ya huduma zinazotambuliwa rasmi na NHIF na gharama halisi zinazotumika hospitalini.

Anadai baadhi ya hospitali hudai kuwa kiwango cha malipo kutoka NHIF hakitoshelezi kugharamia aina zote za upasuaji, hivyo hali hiyo upelekea akina mama hasa wanaojifungua kwa upasuaji kuongeza gharama. Ambapo alitolea mfano huduma ya ICU.

Hata hivyo, wananchi wanaitaka NHIF pamoja na mamlaka husika kutoa elimu ya wazi kwa wanachama wake kuhusu haki zao, sambamba na kuhakikisha hospitali zinazingatia makubaliano yaliyopo. Wanasema ni muhimu kwa Mama mjamzito kufahamu mapema ni huduma zipi zitagharamiwa kikamilifu na zipi zitahitaji malipo ya ziada.

Mama mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe anadai kuwa binti yake alitozwa gharama ya zaidi ya shilingi laki tatu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, licha ya kuwa na bima ya NHIF. Lakini anatoa ushauri kuwa uwazi uongezwe kama gharama hizo ni halali.
adef8d0e-e427-4f19-b36e-7466d4ee6ad4.jpeg

“Serikali na hospitali zijitahidi kutoa elimu kwa wananchi au kubandika mabango katika maeneo ya hospitali, ili mtu aweze kujiandaa mapema. Nilimpeleka binti yangu nikijua anaenda kujifungua sehemu salama na gharama zitagharamiwa na bima, lakini baadaye tuliambiwa tulipe shilingi laki tatu na elfu sabini,” anaeleza.

“Nilipata huduma kupitia NHIF, sikulipia gharama cash”

Hata hivyo, katika mazingira hayo, baadhi ya akina Mama wanasema wao walinufaika na bima ya afya bila kutozwa gharama yoyote wakati wa kujifungua kwa upasuaji, wakidai kuwa hali hiyo ilitokana na msimamo wao mkali.

“Nilijifungua katika Hospitali ya Rufaa Mwananyamala, na kwa bahati mbaya nilihitaji kufanyiwa upasuaji. Baada ya huduma niliambiwa nilipie shilingi laki moja na elfu ishirini. Kwa kuwa mme wangu ni mfanyakazi wa Serikali, alieleza kuwa bima yangu inatosha. Baadaye nesi alikuja kuniambia naweza kuondoka. Sikutozwa chochote,” anaeleza Jesca, mkazi wa Tegeta.

"Kuna changamoto ya uelewa"

Akitoa ufafanuzi kuhusu madai hayo, Meneja wa Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma wa NHIF, James Mlowe, amesema kuwa wamekuwa wakipokea malalamiko ya aina hiyo. Ambapo amedai kuwa baadhi ya malalamiko hayo yanaweza kufanyiwa kazi na yamekuwa yakitatuliwa kupitia watendaji wao waliopo katika baadhi ya hospitali, huku mengine yakitatuliwa ofisini.

“Ni kweli malalamiko ya aina hiyo yanakuwepo, na baadhi tumekuwa tukiyafanyia kazi kupitia watu wetu waliopo karibu katika kila hospitali kubwa. Hata hivyo, niseme kuwa wakati mwingine changamoto hizi zinachangiwa na uelewa mdogo. Kuna wakati akinamama au mtu yeyote anaweza kuombwa kuchangia gharama na baadhi ya hospitali kinyume, licha ya huduma anazopaswa kupata kuwa zimo kwenye vifurushi vya bima. Anapokosa uelewa, unakuta anatoa fedha. Lakini kuna wengine ikiwatokea hali hiyo hupiga simu na sisi tunawasaidia,” amesema James Mlowe

Ameongeza “Unaweza kukuta kweli mtu ana bima ya afya lakini hajui ni huduma gani zinatolewa kupitia bima yake, kwa sababu bima ina huduma zaidi ya 700. Ni wangapi unadhani wanasoma na kuelewa huduma hizo zote? Aidha, kuna huduma nyingine ambazo zipo kwenye bima, lakini pia bima zetu zinatofautiana. Kuna bima za ‘standard’ ambapo kila mtu anapata huduma kwa usawa, lakini pia zipo bima za hadhi ya juu au zile ambazo watu wamelipia zaidi au wametambuliwa kama ‘fast track’, na hao hupewa huduma kwa utaratibu tofauti.”

Ametoa wito kwa mwananchi yeyote, hususan anayekutana na changamoto ya kutozwa gharama kwa huduma ambazo zipo kwenye vifurushi vya bima yake, kutoa taarifa kwa kupiga simu namba ya bure 0800 787 800. Aidha, amesisitiza umuhimu kwa wanufaika wa bima kusoma na kuelewa mwongozo wa huduma wanazopaswa kunufaika nazo.

Mkurugenzi NHF: Tunachukua hatua

Kutokana na kuwepo kwa madai kuwa changamoto ya kutozwa gharama kubwa au “cash” imekuwa ikitokana na mfuko kushindwa kulipa fedha kwa wakati katika baadhi ya hospitali, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Dkt. Irene Isaka, anakiri kwamba awali kulikuwepo na changamoto hiyo, lakini anasema kwa sasa mfuko huo uko katika hali nzuri.

IMG_7848.jpeg

Pichani: Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Dkt. Irene Isaka

“Ni kweli kulikuwepo na hali mbaya ya mfuko, lakini mpaka tulipofunga mahesabu ya Juni 2025, mfuko una hali nzuri kwa sasa. Mwanzoni ulikuwa na uhimilivu wa miezi saba, lakini kwa sasa una uhimilivu wa mwaka mmoja na miezi sita. Tumeweza pia kupunguza muda wa kulipa madai. Awali tulikuwa tunalipa ndani ya siku 120, lakini sasa tunalipa kwa wastani wa siku 55, ambapo kwa mujibu wa sheria tunatakiwa kulipa ndani ya siku 60,” anasema Irene Isaka.

Aidha, amesema kuwa hawasiti kuchukua hatua dhidi ya vituo au watu binafsi wanaokiuka taratibu au wanaohusika na udanganyifu. Anasema hatua hizo zimekuwa zikichukuliwa ili kuchochea uwajibikaji, huku akieleza kwamba katika utekelezaji wake wanashirikiana kwa karibu na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

“Tayari tumeshavifungia vituo 33 kwa sababu ya udanganyifu. Pia tumechukua hatua dhidi ya wafanyakazi 17, na watoa huduma zaidi ya 39 tumewapeleka kwenye mabaraza yao ya kitaaluma baada ya kuhusika na vitendo vya udanganyifu. Aidha, zaidi ya kadi 14,000 za wanachama zilizotumika kufanya udanganyifu zimefungiwa,” anasema Irene Isaka.


Nini kifanyike?

Katika kuchochea uwajibikaji na kupunguza changamoto zinazodaiwa kuwepo, hususan wanawake wanaojifungua kwa upasuaji wanaolalamikia kutozwa gharama licha ya kuwa na Bima ya Afya ya NHIF, Saguda Gamba, mtafiti wa masuala ya kijamii anayefanya kazi na shirika lisilo la kiserikali la SIKIKA, anashauri mamlaka kuhakikisha bajeti za vituo vya afya zinatolewa kwa wakati ili kuondoa usumbufu huo.

Ameeleza kuwa akina mama wajawazito ni kundi muhimu katika jamii linalopaswa kupewa kipaumbele katika huduma za afya. Amesema ni vyema huduma za uzazi zitolewe bure kama miongozo inavyoelekeza, bila kujali aina ya kujifungua. Ikiwa gharama za upasuaji zinaongezeka, ameshauri serikali iongeze bajeti ili kufidia gharama hizo badala ya kuwaachia mzigo akina mama.

Nini kifanyike?

Katika kuchochea uwajibikaji na kupunguza changamoto zinazodaiwa kuwepo, hususan wanawake wanaojifungua kwa upasuaji wanaolalamikia kutozwa gharama licha ya kuwa na Bima ya Afya ya NHIF, Saguda Gamba, mtafiti wa masuala ya kijamii anayefanya kazi na shirika lisilo la kiserikali la SIKIKA, anashauri mamlaka kuhakikisha bajeti za vituo vya afya zinatolewa kwa wakati ili kuondoa usumbufu huo.

Ameeleza kuwa akina mama wajawazito ni kundi muhimu katika jamii linalopaswa kupewa kipaumbele katika huduma za afya. Amesema ni vyema huduma za uzazi zitolewe bure kama miongozo inavyoelekeza, bila kujali aina ya kujifungua. Ikiwa gharama za upasuaji zinaongezeka, ameshauri serikali iongeze bajeti ili kufidia gharama hizo badala ya kuwaachia mzigo akina mama.

Swali linalokuna kichwa

Kutokana na mkanganyiko huo, katika jamii yamekuwa yakiendelea kuibuka maswali kuhusu uwajibikaji na utekelezaji wa sera na miongozo ya Wizara ya afya hususan katika kipindi ambacho Serikali iko kwenye mkakati wa kuanza kutekeleza mfumo wa bima ya afya kwa wote. Ambapo akinamama wengi wakitaka huduma za uzazi kuwa na kipaumbele ili kuwaepusha na gharama.
 
Tulimpeleka mtoto na kad yake Kuna sindano ya kushusha homa et haipo kwenye Kadi🙄🙄 et mzaz alipie
 
Back
Top Bottom