Siku chache baada ya kuzikwa kwa aliyekuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Kongwa, Hayati Job Yustino Ndugai, mchakato wa kisiasa wa kujaza nafasi ya ubunge wa jimbo hilo umeanza upya kwa kasi
Mnamo Siku ya jana Agosti 12, 2025, jumla ya wanachama 24 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walichukua fomu kuomba ridhaa ya chama kugombea nafasi hiyo. Kati yao, watatu ni wanawake na 21 ni wanaume
Takwimu hizo zimetolewa na Katibu wa CCM Wilaya ya Kongwa, Joyce Mkaugala, ambaye amebainisha kuwa waombaji hao wanajumuisha wagombea tisa waliopitishwa awali na Kamati Kuu ya CCM Taifa pamoja na Hayati Ndugai, sambamba na sura mpya 10 zilizojitokeza katika kinyang’anyiro hicho
Soma pia:
GE2025 - Kifo cha Ndugai Charudisha Mchakato wa Kura za Maoni Jimbo la Kongwa; Fomu kuchukuliwa leo Jumanne Agosti 12, 2025
Hatua ya CCM kuanzisha mchakato mpya imekuja kufuatia kifo cha ghafla cha Hayati Ndugai, kilichotokea muda mfupi baada ya kushinda kura za maoni za chama mnamo Agosti 4, 2025, ambapo alipata kura 5,690 na kuwashinda wapinzani tisa waliokuwa wameteuliwa kushiriki hatua hiyo. Baada ya maziko yake yaliyofanyika Agosti 10, 2025, CCM Wilaya ya Kongwa ilitangaza rasmi kuanza kuchukua fomu kuanzia Agosti 11, 2025
Job Yustino Ndugai alihudumu kama Mbunge wa Kongwa kwa muda wa zaidi ya miongo miwili, akiwa pia Spika wa Bunge la 11 (2015–2022)
Alijulikana kwa msimamo thabiti wa kulinda kanuni za Bunge na kuhimiza nidhamu kwa wabunge. Kabla ya kuwa Spika, alishika nafasi ya Naibu Spika wa Bunge kuanzia mwaka 2010 hadi 2015
Katika kipindi cha uongozi wake, Ndugai alihusishwa na juhudi za kuimarisha utendaji wa Bunge na kuendeleza shughuli za maendeleo katika jimbo lake, hususan sekta za elimu, miundombinu, na maji.
Mchakato wa uteuzi wa mgombea atakayewakilisha CCM katika uchaguzi mdogo unaotarajiwa utahusisha hatua kadhaa, kuanzia kuchukua na kurudisha fomu, usaili, kura za maoni ndani ya chama, hadi uteuzi wa mwisho na Kamati Kuu ya CCM Taifa
Chanzo: Manara TV