Maisha ya Mlimwengu Boarding School Episode 7

Maisha ya Mlimwengu Boarding School Episode 7

Mohamed Ismail

JF-Expert Member
Joined
Mar 16, 2014
Posts
227
Reaction score
246
MAISHA YA MLIMWENGU BOARDING SCHOOL

Andrew alikuwa na umbo dogo alipita juu ya dari akadondokea nje ya bweni na mwili wote ulikuwa umejaa vumbi usingeweza kujua sura yake kwa alivyokuwa kutokana na vumbi kutapakaa mwili mzima.
Baraka naye alikuwa na mwili mkubwa alipojaribu kutoka alinasa kwenye dari huku miguu imeelea chini. Alikuwa hawezi kushuka wala kupanda juu na huku anasikia sauti ya mwalimu anakuja kumfuata alipo. Akiwa kanin'ginia darini na akifurukuta kutoka, ghafla ceiling board ilidondoka naye akawa amepata nafasi ya kukimbia. Kitendo cha mwalimu kufika anakuta hakuna mtu na tayari dari imeangushwa. Hapo mwalimu ndio alikuwa mkali kama simba kaguswa sharubu zake.

Kitendo cha kukuta dari imedondoka, hasira zote alizipelekwa kwangu nikapata bakora za kutosha. Huku ukaanza msako wa kuwatafuta wenzangu walipo. Kilichotokea wao walikimbia na kuelekea ziwani kuoga kutokana na vumbi walilolipata huko juu ya dari.
Kwa akili zao walijua wakioga watakuwa wamepoteza ushahidi kumbe tayari mwalimu alikuwa kashawakariri sura zao. Basi walivyorudi waliitwa ofisini wakapata fimbo zao za kutosha. Kipindi hicho fimbo ilikuwa kama salamu ya kawaida kwa wanafunzi watundu ilikuwa lazima matako yapate sugu.
Basi kesi yao ikawa kubwa ya kuvunja mali za umma. Wote wawili wakapewa suspension walete wazazi kwa ajili ya kulipia gharama za huo uharibifu walioufanya. Mlimwengu mimi ikaamriwa nipate fimbo za kutosha pamoja na adhabu ya kufyeka eneo kubwa.
Ndani ya siku tatu nilimaliza na wenzangu walienda nyumbani kwao baada ya siku chache wakarudi na wazazi na wakalipia huo uharibifu uliofanyika na maisha ya shule yakaendelea.

Kadri muda ulivyokuwa unaongezeka shuleni na mimi ndio nilikuwa naizoea shule vizuri. Kipindi hicho shule yetu wakawa wameanza kupokea kidato cha tano kwa mara ya kwanza kwa sababu kipindi cha nyuma ilikuwa O level tu. Vilevile shule ya Mazengo baada ya kubadilishwa na kuwa chuo wanafunzi waliokuwa pale walisambazwa kwenye shule za ufundi na Shule yetu ilikuwa mojawapo ya shule zilizopokea wanafunzi kutoka Mazengo. Basi idadi ya wanafunzi iliongezeka na tabia tofauti ziliongezeka. Wale wa Mazengo walikuwa na aina ya fujo zao zisizoumiza basi wakichanganya na walizozikuta basi shule ikawa haishikiki.

Kipindi hicho makundi ni mengi kuna kundi kutoka Mazengo walikuwa wanajiita MBWA basi hawa nao ilikuwa fujo tupu, mengine walijiita BM , PEWESA, WATU GAZA , WATU PORI, BODI YA MKWAWA na City Boys. Haya ni baadhi ya makundi ambayo yalikuwa yanaendelea kipindi hicho. Basi mimi rafiki zangu walikuwa WATU GAZA na bado tulikuwa watatu tunajiita city boys. Haya makundi bana walikuwa wanataka kama ni Disko lazima wajulikane watataka disko wafungue wao na kila mtu ajue uwepo wao. Na huu ushindani wa haya makundi ndio ulikuwa unapelekea watu wafanye ukorofi na wakifanya ukorofi ndio lilikuwa linaonekana ni kundi bora. Asilimia kubwa ya haya makundi ni kufanya mambo yasiyokuwa na msingi huwezi kukuta wanakumbushana kusoma au wanasaidiana wakati wa shida ilikuwa ni kufanya fujo pamoja na mambo yasiyokuwa na msingi. Laiti kama ingekuwa kama Vicoba sasahivi wangekuwa na biashara kubwa.

Nakumbuka kuna mgahawa shuleni ambao walikuwa wanatuuzia chakula. Kipindi hicho walikuwa wanapika maandazi usiku ili kesho yake iwe ni kuuza tu . Basi rafiki yangu Barry alikuwa ana ufunguo ambao ni kama master key. Huo mgahawa baada ya kufungwa usiku ili wakapumzike, wao wakashtuana muda wa saa sita usiku walienda kwenye huo mgahawa wakafungua mlango na kubeba maandazi yote. Mimi nikiwa nimelala nilishangaa mtu ananiletea maandazi tukaanza kula. Hiki kikosi cha kuiba mandazi walikuwa baadhi ya form 3 wakina Sam pamoja na darasa letu. Mimi hawakunishtua wakijua roho yangu ni ndogo. Maskini mama mwenye mgahawa alirudi anakuta mgahawa hauna kitu ilibidi abadilishe kufuli na ndio akawa amekomesha lakini tayari alikuwa kashatiwa hasara. Ndio maana Mama ntiliye wanaouza maeneo ya shule huwa nawaona kama shujaa katika jamii zetu

Maisha yakaendelea, Kuna siku Bwiru girls walikuwa wamealikwa na Nsumba kwa ajili ya disko. Na sisi wa Boys baada ya kupata taarifa siku yenyewe tulitoroka wengi shule kwenda kujumuika disko la Nsumba. Kuna watu walikuwa wanafuata girlfriend zao lakini mimi ni aina ya watu ambao tunafuata disko ukikosa roho yako inaumia sana . Basi asilimia kubwa ya wahudhuriaji wa disko wote tulienda. Kila mtu alikuwa ana style yake ya kuingia. Maana Nsumba walikuwa hawatutaki kwa sababu tukienda asilimia kubwa ya wasichana tulikuwa tunacheza nao sisi nao wanakosa wa kucheza nao. Sasa hilo lilikuwa linawapa hasira sana. Walikuwa wana scout ukigundulika siyo mwanafunzi wa Nsumba walikuwa wanakupa adhabu. Ila kwa wengine wazoefu ambao tulikuwa tunajua kujichanganya hata chakula cha mchana tulikuwa tunakula kwao.

Wote tuliingia na disko lilikuwa zuri sana maana ulikuwa hukosi wa kucheza naye. Hata disko bana lilikuwa linahitaji connection kam a hakuna anayekujua kucheza na mtoto wa kike na ukashika kiuno ilikuwa kazi sana. Basi kwa wakati huo Mlimwengu mimi nilikuwa nilishapata experience nisingekosa wakucheza naye.Wakati tupo disko Shuleni kwetu wakaitisha lokoo saa 12 sasa walivyoitisha lokoo ilionekana kama nusu shule hawapo kumbe wengi wetu tulikuwa tupo disko. Basi waliitisha lokoo na kuandika majina na kutoa vitisho kwa ambao hawajahudhuria maana waliamini wote tumeenda disko. Kuna aina ya watu shuleni kazi yao kubwa ilikuwa ni kuwatisha watu. Basi tulipigiwa simu hukohuko kuwa shuleni kuna msala. Ukishasikia kuwa kimenuka lazima ukose amani. Disko liliisha salama tukarudi shule.

Picha linaanza siku ya parade Jumatatu asubuh8 tunamuona Headmaster na kipindi hicho ukimuona ujue siku hiyo hapakaliki kama siyo suspension basi ujue adhabu za kutosha lazima zitolewe. Na wanafunzi tulikuwa na tabia moja kuna aina ya nguo akivaa mwalimu mnajua leo itakuwa amani au purukushani. Baada ya kufika parade ikatolewa amri kuwa ambao hawakuwepo lokoo wote waende mbele na ole wako ubaki basi tukaenda wote mbele. Uzuri kilichosaidia siku hiyo watu wengi hata walokole hawakuhudhuria sasa kujua nani kaenda disko inakuwa ngumu. Basi wengi tulitolewa tukapigwa fimbo za kutosha na baadhi tukapelekwa shule ya Bwiru Girls ili wanafunzi wachague watu ambao waliwaona siku ya disko. Tulipangwa mstari kama watumwa wanasubiri kusafirishwa enzi za biashara ya utumwa. Na wote tulikuwa tumeinamisha vichwa chini tunaomba kimyakimya usije ukachaguliwa. Wote sura zetu za upole huwezi kuamini kama ni hawa ambao ikipigwa danso la MOVE kama ni wao ambao huwa wanaruka.
Ule ukaguzi ulipita uzuri na wale wasichana walikuwa wanatujua sema walikuwa hawawezi kutuchoma mbele ya walimu. Zoezi lile la kujua nani alikuwa disko likawa limefeli maana hata waliochaguliwa wakiulizwa wamewajuaje wengi wao walisema kwenye mambo ya dini pamoja na jointmass. Mbinu walizotumia kutukamata zilikuwa za zamani.

Tulirudishwa shuleni lakini mkuu wetu alikuwa hakubali akuache hivihivi tulichapwa fimbo na adhabu juu, na maisha yakaendelea. Kuna siku wanafunzi walikuwa mnarani wanavuta bangi na wengine wanavuta sigara kuna mwanafunzi mmoja alikuwa katoka Mazengo basi naye akawa amejumuika na wale waliokuwa wanavuta bangi. Alivyowasogelea Wakawa wamemshawishi naye akavuta kama pafu mbili alivyovuta ule moshi ukaenda kuvuruga kichwa chake. Ile bangi ikamlewesha akawa amelala basi wenzie walivyomaliza wakamuamsha akawa haamki ikabidi wambebe hadi bweni lake la Lumumba. Wakamfikisha hadi kitandani akawa amelala. Walimuacha wakiamini ndani ya muda mchache atakuwa ameamka. Kilichotokea hadi kesho yake akawa bado amelala fo fo fo na hajitambui. Waliokuwa wamevuta naye wakajua ni bangi lakini wakawa wana mashaka naye labda alitumia kitu kingine ndio kimempelekea alewe zaidi.

Muda ulivyozidi wakachanganyikiwa wakahisi wakikaa kimya sana anaweza hata kufariki baadhi ya watu wanasema apelekwe hospitalini wengine wanasema huyo ataamka. Ikabidi kiongozi wa bweni atoe taarifa kwa uongozi wa shule kuwa kuna mgonjwa ana malaria kali kazidiwa hapo kumbuka bado mtu hajaamka haongei wala hatingishiki. Ile mwalimu anakuja pamoja na dreva kwa ajili ya kumchukua wanafunzi wote wakakimbia. Mwalimu akatahamaki hajui kinachopelekea watu wakimbie. Ikabidi abebwe na kukapakiwa kwenye gari kuelekea hospitalini.
Je nini kitaendelea huko na hospitali watagundua nini?
Tukiwa tunaenda kutimiza miaka 100 tangu Bwiru Boys ianzishwe. Mlimwengu mimi uliyeambiwa kuwa mama yako asipokufunza utafunzwa naye nitakuwa naeleza matukio niliokutana nayo shule.
Episode 7
Stay tuned
#BwiruBoysAlumni
#mlimwenguMimi
#100yearsAnniversary
Screenshot_20190822-214111.jpeg
 
Back
Top Bottom